BAO pekee lililowekwa kimiani dakika 41 na kiungo Fabrice Ngoma limeiwezesha Simba kujihakikisha kuuaga mwaka 2024 na kujiandaa kuingia 2025 ikiwa kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Bara baada ya kuizamisha Singida Black Stars ikiwa nyumbani kwenye Uwanja wa Liti, mjini Singida.
Ushindi huo ambao ni wa tisa mfululizo kwa Simba tangu ilipiotoka kupoteza mbele ya Yanga katika Dabi ya Kariakoo iliyopigwa Oktoba 19 mwaka huu na wa 13 katika mechi 15 za duru la kwanza ilizocheza imeifanya ifikishe pointi 40 ambazo haziwezi kufikiwa hata na watetezi Yanga itakayoshuka uwanjani kesho Jumapili kumalizana na Fountain Gate kwenye Uwanja wa KMC Complex.
Ngoma alifunga bao hilo lililokuwa la tatu kwake msimu huu na la pili mfululizo Simba ikicheza ugenini baada ya kuunganishwa kwa kichwa kona iliyopigwa kiufundi na Jean Charles Ahoua akimzidi ujanja kipa wa Singida, Metacha Mnata aliyetoka bila hesabu nzuri kuwahi mpira huo na kuishia kujigonga kwa Ellie Mpanzu.
kabla ya bao hilo la leo, Ngoma pia alifunga wakati Simba ikiisambaratisha Kagera Sugar kwa mabao 5-2 kwenye pambano lililopigwa wiki mbili zilizopita kwenye Uwanja wa Kaitaba, mjini Bukoba.
Matokeo hayo ya leo yameifanya Simba kufikisha jumla ya mabao 31 na kufungwa matano katika mechi 15 za duru la kwanza, huku Singida ikisalia nafasi ya nne ikiwa na pointi 33 baada ya mechi 16, huku ikiruhusu kufungwa mabao 11 na yenyewe kufunga 22.
Mashabiki wa Simba waliofurika kwenye Uwanja wa Liti, huku wakiwa na presha kutokana na jinsi wenyeji Singida walivyo kwa msimu huu na aina ya wachezaji walionao, kiasi kwa muda mrefu hawakuwa na yale mashamshamu yaliyozoeleka kutoka na wenyeji wao kuungwa mkono na mashabiki wa Yanga uwanjani hapo.
Pamoja na dakika 45 za kwanza kuanza kwa timu zote kucheza kwa utulivu na kusoma mbinu za wapinzani, kabla ya kuchangamka kadri muda ulivyokuwa ukisonga mbele, japo kuna wakati mwamuzi Shomari Lawi kutoka Kigoma kujichanganya na kufanya wachezaji kupaniki hasa wale wa Singida waliohisi wanaonewa.
Hata hivyo, Simba ilionekana kucheza kwa akili kubwa ikisaka ushindi huo wa 13 wa Ligi Kuu kwa kuwabana kwa muda mrefu wenyeji ambao washambuliaji wake tegemeo, Elvis Rupia, Marouf Tchakei, Joseph Bada na Idd Habib wakisaidiwa na Mohamed Domario walishindwa kuonyesha makeke waliyozoeleka mbele ya ukuta wa Simba uliokuwa chini ya Abdulrazak Hamza na Fondoh Che Malone.
Licha ya Singida Black Stars kuonyesha uimara eneo la ulinzi makosa ya kipa wao Metacha Mnata dakika ya 41 yalitosha kuiondoa Simba kwenda mapumziko wakiwa wanaongoza bao 1-0. Hiyo ilikuwa ni asisti ya tano kwa Ahoua mwenye mabao saba hadi sasa katika ligi hiyo inayochezwa leo mechi mbili kabla ya kusimama hadi Januari 20, 2025.
Licha ya kuanzishwa kikosi cha kwanza sambamba na Steven Mukwala, Ahoua na Kibu Denis, nyota mpya wa Simba, Ellie Mpanzu aliendelea kuwa mchezaji machachari kwa kushindwa kufanya mambo licha ya kutengeneza nafasi kadhaa langoni mwa Singida iliyocheza kwa utulivu eneo la ulinzi lilikuwa chini ya Anthony Tra Bi na nahodha Kenendy Juma ambaye alikuwa pia anatumia muda mwingi kulalamika kwa mwamuzi Lawi.
Nyota huyo aliyetambulishwa hivi karibuni, hata hivyo alitolewa kipindi cha pili kumpisha Awesu Awesu ambapo mabadiliko hayo na mengine ya kikosi hicho cha Simba na hata Singida hayakusaidia kubadili matokeo hadi dakika ya 90.
Pamoja na kupoteza mchezo huo, lakini Singida itajilaumu kwa kushindwa kutumia nafasi chache ilizotengeneza ikiwamo ile ya kipindi cha kwanza, wakati Rupia anayeongoza orodha ya wafungaji akiwa na mabao manane, aliposhindwa kufunga baada ya kupokea pasi tamu ya Tchakei na kuzembea hadi kudhuibitiwa na mabeki wa Simba.
Rupia pia alipata nafasi kama hiyo kipindi cha pili, lakini alishindwa kufunga mbele ya kipa Moussa Camara aliyefikisha clean sheet ya 12 katika mechi hizo 15 za duru la kwanza akiwa nidyer kinara hadi sasa.
Simba sasa inageukia maandalizi ya mechi za kimataifa za Kombe la Shirikisho Afrika ikijiandaa kuifuata Cs Sfaxien ya Tunusia Januari 5, kisha kumalizana na CS Constantine wa Algeria na Bravos do Maquis ya Angola.
SIMBA: Camara, Kapombe, Tshabalala/Karaboue, Hamza, Che Malone, Kagoma, Kibu, Ngoma, Mukwala/Ateba, Mpanzu/ Awesu na Ahoua/Debora
SINGIDA: Metacha, Andy, Imoro/Manyama, Kennedy, Tra Bi, Damaro, Habib/Adebayor, Keyekeh, Rupia, Tchakei/Lyanga na Bada