Yanga Omari ‘rais wa Tanga’ afia kifungoni

Dar es Salaam. Aliyekuwa mfanyabiashara maarufu jijini Tanga, Yanga Omari ‘maarufu rais wa Tanga’ amefariki dunia jana mchana (Desemba 27, 2024) akiwa anapatiwa matibabu katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), akiwa chini ya ulinzi wa Jeshi la Magereza.

Yanga alikuwa anatumikia kifungo cha miaka 30 jela baada ya kutiwa hatiani kwa kupatikana na dawa za kulevya.

Kaimu Ofisa Habari wa Muhimbili, Angela Mdolwa amethibitisha kifo cha Yanga akieleza taarifa zaidi watafutwe Magereza.

“Ni kweli huyo mtu amefariki akiwa hapa Muhimbili lakini kwa taarifa zaidi watafuteni Magereza kwa sababu alikuwa chini yao,” amesema.

Alipotafutwa Msemaji wa Jeshi la Magereza, Elizabeth Mbezi pia amethibitisha kifo cha Yanga.

“Ni kweli amefariki akiwa hospitali akiendelea na matibabu, kuhusu ugonjwa uliomuua hiyo ni siri ya mgonjwa au familia inaweza kutoa uthibitisho,” amesema.

Amesema Yanga amekuwa akihamishwa katika magereza tofauti na hadi kifo chake alikuwa katika Gereza la Ukonga.

Uongozi wa Klabu ya Coastal Union FC katika taarifa umetoa pole kwa familia, ndugu, jamaa na marafiki kutokana na msiba wa Yanga aliyekuwa mchezaji wake wa zamani.

“Uongozi unashirikiana nanyi katika kipindi hiki kigumu, tukiwaombea faraja na nguvu wakati huu wa majonzi. Mazishi yatafanyika Jumamosi Desemba 28, 2024 saa 10:00 jioni. Nyumbani kwake Mwambani,” imesema taarifa ya klabu hiyo.

Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), Aretas Lyimo alipotafutwa na Mwananchi jana Desemba 27, 2024 alisema Yanga alikuwa mfanyabiashara mkubwa wa dawa za kulevya na alihukumiwa kifungo cha miaka 30 jela.

“Taarifa za kifo chake sijapata, itabidi niwasiliane na watu wa Kanda ya Dar es Salaam ila ninachokumbuka Yanga tulimkamata, alihukumiwa kifungo cha miaka 30 jela, alikata rufaa na alishindwa,” alisema.

Alisema kutokana na kutiwa hatiani na kuhukumiwa kifungo Serikali ilitaifisha mali zake, yakiwamo mashamba na nyumba ikiaminiwa zilipatikana kwa njia ambayo si halali.

Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Tanga ilimtia hatiani Yanga kwa kusafirisha dawa za kulevya aina ya heroini hydrochloride yenye uzito wa gramu 1,052.63 Oktoba mosi 2018 katika eneo la Bombo, mkoani Tanga.

Yanga na wenzake Rahma Juma na Halima Anuary, walishtakiwa kwa pamoja kwa kosa la kusafirisha dawa za kulevya kinyume cha kifungu cha 15 (1) (a) (3) (1) (i) cha Sheria ya Kudhibiti Dawa za Kulevya (Sura ya 95 kama ilivyorejewa mwaka 2019, ikisomwa pamoja na vifungu vya 57 (1) na 60 (2) vya Sheria ya Kudhibiti Makosa ya Hujumu Uchumi (Sura 200 iliyorejewa mwaka 2019).

Baada ya kusomewa mashtaka, washtakiwa wote waliyakana. Upande wa mashtaka uliita mashahidi saba na kuwasilisha vielelezo kadhaa kuthibitisha kesi yao.

Kwa mujibu wa ushahidi uliowasilishwa mahakamani, mashahidi wa DCEA walipata taarifa za kiintelejensia kuhusu mshtakiwa kusafirisha dawa hizo kupitia Pwani ya Tanga.

Septemba 27, 2018, maofisa hao walifanya ufuatiliaji na baadaye walimkamata mshtakiwa nyumbani kwake usiku wa manani. Walipata vitu mbalimbali likiwemo begi lenye dawa zinazoshukiwa ni za kulevya na fedha taslimu Sh5.3 milioni kutoka kwenye gari lake.

Vielelezo vilikusanywa, kufungashwa rasmi na kupelekwa kwa Mkemia Mkuu wa Serikali kwa uchunguzi uliothibitisha sehemu ya vitu vilivyokamatwa vilikuwa dawa za kulevya aina ya heroini hydrochloride.

Yanga alikana mashtaka akidai vitu vilivyokamatwa vilikuwa ni vyakula na dawa za kuku na si dawa za kulevya. Pia, alipinga taratibu za uhifadhi wa vielelezo, akisema vilifungashwa Dar es Salaam badala ya Tanga.

Jaji Immakulata Banzi wa Mahakama Kuu alimtia hatiani Yanga na kumhukumu kifungo cha miaka 30 jela, huku ikiwaachia huru Rahma na Halima kwa kukosekana ushahidi wa moja kwa moja wa kuonyesha walishirikiana naye kutekeleza kosa hilo. Rehema ni mke wa Yanga na Halima alikuwa mfanyakazi wa ndani.

Yanga hakuridhika na hukumu akakata rufaa Mahakama ya Rufaa ya Tanzania.

Katika rufaa ya jinai namba 132 ya mwaka 2021 aliwasilisha hoja kadhaa zikiwamo mahakama ya chini ilikosea kisheria na kimantiki kwa kuhitimisha kwamba upande wa mashtaka ulikuwa umethibitisha kesi pasipo kuacha shaka yoyote.

Alidai kukosekana kwa ushahidi wa kuthibitisha kwamba alikuwa na uelewa wa uwepo wa dawa za kulevya ndani ya nyumba, kukosekana kwa ushahidi wa moja kwa moja kuhusu umiliki wake wa dawa hizo na kuvunjika kwa mnyororo wa uhifadhi wa vielelezo vya ushahidi.

Kwa kuzingatia hoja zilizowasilishwa mahakamani, majaji watatu wa Mahakama ya Rufaa katika hukumu walikubaliana na uamuzi wa Jaji wa Mahakama Kuu wakieleza hakuwa na kosa katika kutoa hukumu ya kifungo cha miaka 30 jela badala ya kifungo cha maisha, hivyo mahakama ilikataa ombi la kuongeza adhabu.

Kwa kuzingatia ushahidi uliotolewa, Mahakama ya Rufaa katika hukumu iliyotolewa Juni mosi, 2021 iliamua kwamba mashtaka yalithibitishwa pasipo kuacha shaka yoyote ikatupilia mbali rufaa.

Aliendelea kutumikia kifungo hadi mauti yalipomkuta.

Related Posts