Dk Mwinyi ataka programu shindani taasisi za elimu ya juu

Unguja. Wakati wahitimu wa vyuo vikuu na taasisi za elimu ya juu wakitarajiwa kutekeleza miradi na mipango ya kuinua uchumi wa nchi na kutoa huduma bora kwa jamii, Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi amezitaka taasisi hizo kuandaa programu katika mitindo itakayowawezesha wahitimu hao kufikia matarajio ya Serikali na jamii kwa ujumla.

Dk Mwinyi ametoa kauli hiyo leo Desemba 28, 2024 wakati wa mahafali ya 20 ya Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar (Suza) ambapo amesema kwa kutambua umuhimu wa elimu ya juu nchini, Serikali imekuwa ikitekeleza mpango wa kuimarisha elimu ya juu katika maeneo kadhaa muhimu.

“Serikali inategemea wahitimu kutoka vyuo vikuu katika mipango yake, hivyo niwatake wanajumuiya ya Suza kuendelea kuandaa programu zitakazowezesha wahitimu kufika matarajio ya jamii na Serikali,” amesema.

Akizungumzia mipango inayotekelezwa kuimarisha elimu, ameitaja kuwa ni pamoja na kuweka mkazo katika kuboresha miundombinu ya vyuo vikuu kwa kujenga na kukarabati majengo, kumbi za mihadhara na maabara za kisasa ili kuwezesha mazingira bora ya kujifunza.

Pia, imeongeza uwekezaji katika teknolojia ya elimu, ikiwemo ufungaji wa mtandao wa intaneti yenye kasi na vifaa vya kisasa vya kufundishia na kujifunzia.

Kwa mujibu wa Dk Mwinyi ambaye pia ndiye Mkuu wa chuo hicho, Serikali pia imeimarisha ufadhili wa masomo kwa wanafunzi kupitia mikopo na ruzuku, kuhakikisha kuwa elimu ya juu inapatikana kwa watu wengi zaidi bila kujali hali zao za kiuchumi.

Kwa upande wa kuwawezesha wanafunzi kumudu gharama za masomo yao, wanafunzi wa vyuo kutoka Zanzibar wanaosoma katika vyuo vya ndani na nje ya Tanzania, amesema wanaendelea kutumia fursa za mikopo inayotolewa na Serikali ya Muungano na ile inayotolewa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

“Kwa mwaka wa masomo 2024/25 Serikali ya SMZ kupitia Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Zanzibar imetenga Sh33.4 bilioni kwa mikopo ya wanafunzi. Jumla ya wanafunzi 8,870 wamechaguliwa kupatiwa mikopo kwa Bodi ya Mikopo ya SMZ wakiwemo wanafunzi 4,573 wapya na 4,297 wanaoendelea na masomo,” amesema kiongozi huyo.

Amesema takwimu hizo zinaonyesha ongezeko la wanafunzi 2,716 ikilinganishwa na jumla ya wanafunzi 6,154 waliopatiwa mikopo mwaka uliopita 2023/24 ikiwa ni ongezeko la asilimia 44.

Kadhalika, kwa mara ya kwanza SMZ imeweza kuwapatia mikopo wanafunzi 1,420 wanaosoma ngazi ya stashahada katika vyuo mbalimbali vya Tanzania.

Kwa upande wa Suza, wanafunzi 1,720 wameendelea kupatiwa huduma za mikopo kwa mwaka 2024/25 ikiwa inaongoza kwa usawa wa asilimia 19.4 ya wanafunzi wote waliopatiwa mikopo ya SMZ kwa vyuo vya Tanzania.

“Juhudi hizi zilizofanywa na Serikali ya awamu ya nane zimeiwezesha Suza kuongeza idadi ya wanafunzi kutoka wanafunzi 5,000 mwaka 2020/21 hadi wanafunzi 7,045 kwa mwaka wa masomo 2023/24 sambamba na ongezeko la programu nne za masomo kwa ngazi ya shahada na uzamili,” amesema.

Naye Makamu Mkuu wa Suza, Profesa Mohamed Makame Haji amesema jumla ya wafanyakazi 183 wa Suza wamepatiwa mafunzo ya muda mrefu kwa ngazi ya uzamili na uzamivu kwa kipindi cha mwaka 2020 hadi 2024.

Kati ya hao, 72 ni ngazi ya uzamivu, 79 uzamili na 31 shahada ya kwanza na mmoja stashahada. Serikali inalenga kuinua kiwango cha elimu ya juu na kuandaa wataalamu wenye ujuzi na maarifa ya kisasa.

“Kadhalika, wataalamu 12 wamepelekwa katika mafunzo ya muda mrefu wakiwemo vijana 11 kwa mafunzo ya ngazi ya uzamili na mmoja kwa ngazi ya uzamivu (PhD) kwa ajili ya kuwaongezea uwezo zaidi,” amesema.

Katika kuiongezea nguvu dhamira hiyo, chuo kimeandaa mpango kabambe wa kuimarisha chuo hicho katika elimu na utafiti.

“Mpango huu umejielekeza zaidi kwenye mikakati thabiti ya kuboresha miundombinu, kuajiri wahadhiri wenye sifa na ubora wa juu, na kuboresha mazingira ya utafiti na uvumbuzi,” amesema.

Kati ya wahitimu 2,291 asilimia 61 ni wanawake na kwamba idadi yao inaendelea kuongezeka kutoka asilimia 58 ya mwaka jana.

Kwa upande wake, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Lela Mohamed Mussa amesema wataendelea kufanya kazi na kuzingatia maelekezo kuhakikisha elimu ya juu inakua.

“Miaka mingi bodi ya elimu ya juu ilikuwa inatoa mikopo kwa wanafunzi wa shahada ila tangu mwaka jana imeshushwa hadi stashahada,  hii itatoa fursa kubwa zaidi kwa wanafunzi kujifunza,” amesema.

Related Posts