Simbachawene ataka mfuko wa kusawasaidia wasio na uwezo kielimu

Dodoma. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene amekitaka Kikundi cha Mikalile ye Wanyausi ambacho huwakusanya jamii ya Wagogo, kuunda mfuko wa kuwasaidia watoto wasiokuwa na uwezo kielimu.

Akizungumza leo Jumamosi Desemba 28, 2024 katika mkutano mkuu wa kikundi hicho, Simbachawene amewataka wanakikundi  kukaa na wawakilishi wa Dodoma ili wawaeleze zilipo changamoto za sekta ya elimu.

Amesema kwa kutumia misingi ya utamaduni ni vema wana kikundi hicho wakalipa kipaumbele suala la elimu.

“Watu wetu hawana uwezo wa kusomesha watoto. Watoto wanafaulu kwenda kwenye shule za vipaji maalumu, lakini anakuja kukuomba umsaidie abadilishe asome katika shule za kawaida kwa sababu hawana uwezo wa kuwasafirisha kwenda mbali,” amesema.

Simbachawene ambaye pia ni Mbunge wa Kibakwe, amesema namna ya kuwasaidia watoto hao ni kuwa na mfuko ambao utafafanua vigezo vya kusaidiwa.

Amesema hilo linatokana na wanafunzi wanaoacha shule kuwa ni wengi hasa mabinti. Simbachawene ametaka umoja huo kuweka katika maandishi masuala yanayohusu mila, tamaduni na desturi za kabila ya Kigogo ili kizazi cha sasa na kinachokuja kiweze kusoma.

“Dunia ya sasa inaamini katika kuandika na kutangaza vizuri, kusimuliana hadithi hatuna huo muda. Hadithi sasa hazisimuliwi ni lazima sasa tuandike ili watu wayasome. Nimeona niliseme hili ili wenzetu wenye muda mkiweza muyaandike,” amesema.

Naye Waziri wa Madini, Antony Mavunde amesema wawakilishi katika majimbo yote ya Mkoa wa Dodoma,  wameamua kwa pamoja kuwekeza nguvu kubwa kwenye elimu ambayo wanaamini kuwa ndio itamkomboa mtoto wa mkoa huo.

“Vilevile, sisi huwa tunajisikia vibaya pale watu wengi katika mikoa ya nje ya Mkoa wa Dodoma, hasa Mkoa wa Dar es Salaam wanapotafuta mfanyakazi wa ndani simu ya kwanza inapigwa Mkoa wa Dodoma. Hii ni lazima kama viongozi ituume na tuone tuna wajibu wa kuwasaidia watoto wetu,” amesema.

Pia, amesema watu wengi wamekuwa na mtazamo hasi kama Dodoma ni sehemu ya watu wavivu, akisema wakati umefika wa kuiambia dunia Dodoma ina mwelekeo tofauti hivi sasa.

Mwenyekiti wa Mikalele, Grace Lesiwa amesema lengo la umoja huo ni kuendeleza mila, tamaduni na desturi za Wagogo huku wakihamasisha maendeleo kwa ajili ya Taifa.

Amesema lengo lao ni mwakani kuanza ujenzi wa makumbusho katika eneo la Mchemwa ambapo wamenunua eneo kwa madhumini hayo.

“Tulisema Serikali imehamia Dodoma, je, wakitaka kwenda kutembea mwishoni mwa wiki wanaona nini? Wanafaa kuona mahali ambapo Wanyausi walikuwa wanaishi, Wanyausi wakitaka kufanya harusi zao wanafanya hivyo, sherehe zinafanywaje,” amesema.

Grace amesema walipoanza,  waliunda kamati mbalimbali ikiwemo ya elimu na wameshasaidia madawati katika baadhi ya shule zenye changamoto hiyo.

Amesema wameangalia katika sekta ya elimu, changamoto ipo wapi na wakagundua miongoni mwa shida ni uhaba wa madawati na miundombinu ya malazi.

Related Posts