Putin aomba radhi ndege ya Azerbaijan kupata ajali anga la Russia

Russia. Rais wa Russia, Vladimir Putin amemwomba radhi Rais wa Azerbaijan, Ilham Aliyev, kufuatia ndege ya Shirika la ndege la Azerbaijan kupata ajali katika anga la Russia eneo la Chechnya.

Putin ameomba radhi kupitia taarifa ya Ikulu ya Kremlin kwa Umma leo Desemba 28, 2024 akiomba radhi kwa kile alichodai ni kitendo cha ndege hiyo kupata changamoto ikiwa kwenye anga la Russia.

Hata hivyo, Rais Putin hakuzungumzia kabisa madai ya Russia kuhusishwa kwenye chanzo cha ajali hiyo badala yake amesema anaamini vyombo vya uchunguzi kutoka pande zote vitatoa majibu na taarifa sahihi za chanzo cha ajali hiyo.

“Vladimir Putin anaomba radhi kwa tukio la ajali hiyo ya kuhuzunisha iliyotokea kwenye anga la Russia. Anatoa pole kwa familia zilizoathiriwa na ajali hiyo na kuwatakia majeruhi wapone haraka,” imesema taarifa hiyo.

“Wakati ajali hiyo inatokea eneo la Grozny, Mozdok na Vladikavkaz yalikuwa chini ya mashambulizi makali ya droni za Ukraine na anga la Russia lilikuwa likijitahidi kuyazuia,” amesema katika taarifa hiyo.

Pia amesema mamlaka nchini Russia zitatoa ushirikiano kwa wachunguzi wa suala hilo huku akionya kwamba hali ya anga la Chechnya si ya kuridhisha kutokana na eneo hilo kukumbwa na mashambulizi mfululizo ya Droni kutoka Ukraine.

Kwa upande wake, Rais Aliyev, wa Azerbaijan kupitia taarifa ya Ikulu amemjibu Putin kuwa ndege hiyo ilikumbana na hitilafu ya nje kabla ya kuanguka ardhini.

Amesema baada ya ufuatiliaji kwenye mabaki ya ndege hiyo ilibainika kuwepo matundu yanayohisiwa kuwa yamesababishwa na mashambulizi kutokea nje ya ndege hiyo.

Ndege hiyo ya Shirika la Azerbaijan Airlines namba J2-8243 ilipata ajali Jumatano Disemba 25, 2024, ikitokea Jijini Baku Azerbaijan kwenda Grozny Chechnya nchini Russia.

Taarifa iliyotolewa na mamlaka nchini Azerbaijan ilidai kuwa ilipata hitilafu ikiwa katika anga la Russia na kulazimika kwenda kutua kwa dharura kwenye Uwanja wa Aktau nchini Kazakhstan siku ya Jumatano.

Hata hivyo jaribio hilo la kutua kwa dharura kwa ndege hiyo iliyokuwa na abiria takriban 77 kwenye Uwanja wa Aktau halikufanikiwa baada ya kuanguka umbali ardhini wa kilometa 3.2 hadi ulipo Uwanja huo.

Baada ndege hiyo kupata hitilafu ikiwa kwenye anga la Russia, vyombo mbalimbali vya habari na wanasiasa nchini Azerbaijan waliibua tuhuma kuwa mwonekano wa mabaki ya ndege hiyo yanaashiria kuwepo matundu yanayodhaniwa kuwa ya risasi. Matundu hayo yakadaiwa kuwa ilishambuliwa ilipofika kwenye anga la Russia.

Kabla ya kauli ya Putin leo, Mkuu wa Kitengo cha Anga cha Russia, Dmitry Yadrov alizungumza jana na vyombo vya habari na kusema mifumo ya kujilinda ya anga la Russia ilikuwa imezimwa hata kabla ndege hiyo haijagusa anga la Russia.

Badala yake, Yadrov amesema wakati huo droni za Ukraine zilikuwa mguu sawa kufanya mashambulizi dhidi ya Russia huku akigoma kuzungumzia uchunguzi wa madai ya kuhusika na shambulio hilo.

Hata hivyo, kampuni ya ndege hiyo, ilidai kwamba ajali ya ndege hiyo ilitokana na muingiliano wa kiufundi katika mifumo ya anga na kwenye uwanja wa ndege wa ilipotarajiwa kutua japo haikuuweka wazi ni wapi muingiliano huo ulitokea.

Kwa mujibu wa manusura wa ajali hiyo, kabla ndege hiyo haijaanguka walisikia sauti ya nguvu zikikita kwenye mwili wa ndege hiyo ilipokuwa ikikaribia anga la eneo la Grozny.

Mhudumu wa ndege hiyo, Aydan Rahimli amesema baada ya kishindo hicho cha kelele kusikika vifaa vya Oksijeni vilifunguka jambo lililomlazinu kwenda kutoa huduma ya kwanza kwa mhudumu mwenzake, Zulfugar Asadov ghafla wakasikia imegonga ardhini.

Kwa upande wake, Asadov alipohojiwa akiwa hospitalini alisema alisikia sauti kama ya kitu kikikita kwenye mwili wa ndege hiyo, huku akikanusha kuwa vifaa vilivyobeba Oksijeni kuwa vililipuka.

Madai ya ndege hiyo kushambuliwa yamekaziwa na Waziri wa Usafirishaji wa Azerbaijani, Rashad Nabiyev, aliyesisitiza kuwa ndege hiyo imedunguliwa ikiwa kwenye anga la Grozny Chechnya nchini Russia.

Hadi sasa mamlaka nchini Russia, Azerbaijan na Kazakhstan zinasubiria kusikia majibu ya uchunguzi wa wataalam kuhusiana na kisa cha ndege hiyo kudondoka.

Pamoja na hatua hizo, Mbunge wa Azerbaijan, Rasim Musabekov, amedai kuwa kuanguka kwa ndege hiyo ni matokeo ya mashambulizi, huku akiitaka Russia kuomba radhi kwa kitendo hicho.

Alipoulizwa kuhusu kauli hiyo ya Musabekov’, Msemaji wa Ikulu ya Kremlin, Dmitry Peskov alikanusha madai hayo na kusema wenye ukweli ni kamati zilizoundwa kuchunguza sakata hilo.

“Tukio la ajali hiyo linachunguzwa na hatuoni kama tuna haki ya kuanza kuhukumiana hadi pale ripoti ya wataalam itakapoanikwa,” alisema Pescov.

Hata hivyo, Yadrov, ambaye ni Mkuu wa Kitengo cha Anga cha Russia amesema ndege hiyo ilipokaribia kutua mifumo ya ulinzi wa anga ilizimwa kutokana na ongezeko la ukungu kuzunguka uwanja huo wakati ambao droni za Ukraine zilikuwa zikiishambulia Russia.

“Hali iliyokuwepo katika uwanja wa Grozny ni ngumu kwa ndege kutua ndiyo maana unahitajika uchunguzi unaohusisha pande zote,” alisema ofisa huyo.

Tovuti ya masuala ya anga ya FlightRadar24 ilichapisha taarifa kuwa ndege hiyo kabla ya kuanguka ilipata hitilafu katika mfumo wake wa Rada na kudai Mfumo huo wa rada unadaiwa kuathiriwa na mifumo ya kujilinda ya Russia.

Kutokana na ajali hiyo baadhi ya safari za ndege zimeahirishwa kwenda Grozny nchini Russia ikiwemo kampuni ya Qazaq Air, na FlyDubai ambayo ilikuwa na safari leo kutokea Mji wa Sochi kwenda Mineralnye Vody Kusini mwa Russia hadi Januari 5, mwakani.

Imeandikwa na Mgongo Kaitira kwa msaada wa Mashirika

Related Posts