Israel yadaiwa kumkamata mkurugenzi, watumishi wa hospitali pekee Gaza

Gaza. Jeshi la Israel linadaiwa kumkamata Mkurugenzi wa Hospitali ya Kamal, Adwan iliyopo eneo la Gaza nchini Palestina, Dk Abu Safiya na wafanyakazi kadhaa wa hospitali hiyo.

Kukamatwa kwa Dk Safiya na wafanyakazi wenzake kumethibitishwa kupitia taarifa iliyotolewa leo Jumamosi Disemba 28, 2024, Shirika la Afya Duniani (WHO) ambalo limedai ukamataji huo umefanyika jana baada ya wanajeshi kuvamia hospitali hiyo.

WHO imesema Kamal Adwan ambayo ni hospitali pekee iliyosalia na inayotoa huduma eneo la Gaza imekumbwa na matukio ya uvamizi sambamba na mashambulizi mfululizo yanayotekelezwa na Jeshi la Israel (IDF).

Kabla ya kukamatwa kwa mkurugenzi huyo, mashambulizi ya Israel yalisababisha Umeme kukatika ndani ya hospitali hiyo jambo lililosababisha madhara ikiwemo vifo vya watoto na wagonjwa waliokuwa wakipumua kwa kutumia mashine (Ventilator).

WHO inadai hadi sasa, Dk Safiya, na wafanyakazi wenzake hawajulikani walikopelekwa japo mashuhuda wa tukio hilo wamelieleza shirika la habari la CNN kuwa Dk Safiya alishushiwa kipigo kizito kabla ya kuchukuliwa na wanajeshi hao.

Jana Ijumaa Dk Safiya alichapisha kwenye akaunti yake ya X (zamani Twitter) kuwa vikosi vya Israel vimeizingira hospitali hiyo na katika chapisho hilo aliandika: “Wametutaka tuwaondoe wagonjwa wote ndani ya hospitali na tukusanyike nje,” 

Wauguzi wawili waliozungumza na CNN wamesema mbali na Dk Safiya, wanajeshi hao waliwaamuru wagonjwa na wahudumu kutoka nje ya hospitali hiyo, kisha kuwataka wavue nguo zao na waliogoma kutekeleza amri hiyo walishushiwa kipigo.

Taarifa ya kuamriwa kuvua nguo hizo imetolewa na muuguzi katika hospitali hiyo, Shorouq Saleh Al-Rantisi, ambaye amesema jambo hilo lilifanyika jana Ijumaa Disemba 27, 2024.

Baada ya muda kupita walilazimishwa kuhamia kwenye jengo la hospitali iliyokuwa inamilikiwa na raia wa Indonesia ambalo hata hivyo halitumiki tena kutokana na kuharibiwa na mashambulizi ya Jeshi hilo.

Muuguzi mwingine, ambaye hakutaka jina lake lijulikane aliieleza CNN jana kuwa baada ya kutolewa ndani ya hospitali hiyo wanajeshi wengine walianza kuwafanyia mahojiano mmoja mmoja kwenye gari iliyokuwa imeegeshwa pembeni mwa jengo hilo.

“Vijana wote waliokuwemo ndani ya hospitali walichukuliwa akiwemo mume wangu,” alisema muuguzi huyo.

Wizara ya Afya ya Palestina pia imetoa taarifa awali ikimnukuu Dk Safiya kuwa vikosi vya Jeshi la IDF, vimechoma moto jengo la idara ya upasuaji katika hospitali hiyo na kusababisha majeraha kadhaa ya watu miongoni mwao ni wahudumu wa afya.

Hadi kufikia jana Ijumaa hospitali hiyo ilikuwa ikitumika kama makazi ya watu zaidi ya 350 miongoni mwao ni wagonjwa 75 na wahudumu wa afya 180.

WHO imedai kwamba kati yao 25 ni wagonjwa mahtuti wakiwemo waliokuwa kwenye mashine za kusaidia kupumua na kwamba ambao wamesalia eneo hilo ni wahudumu wa afya takribani 60 pekee.

Shirika hilo pia limeomba kusitishwa kwa mapigano hayo; “ Uvamizi wa Israel katika hospitali ya Kamal Adwan mjini Gaza ni mwendelezo wa taifa hilo kuzuia misaada ya WHO kufika eneo hilo kwa kushambulia maeneo ya jirani na ilipo hospitali. 
“Kitendo cha kufanya mashambulizi ndani ya hospitali na kutikisa mfumo wa afya ni sawa na kutoa hukumu ya kifo kwa wagonjwa makumi kwa maelfu wanaohitaji msaada wa matibabu eneo la Gaza.
“Matendo haya yanapaswa kukomeshwa na wapya huduma ya afya walindwe eneo la Gaza,” imesema WHO.
IDF ilitoa taarifa awali ikidai kwamba ilianzisha operesheni kuzunguka eneo la hospitali hiyo kutokana na taarifa za kuwepo magaidi wa kundi la Hamas ndani ya jengo hilo bila kuanika ushahidi wa madai hayo.
Jeshi hilo pia lilitoa taarifa likidai kwamba liliwasaidia wagonjwa na wafanyakazi kuondoka ndani ya hospitali hiyo kabla ya kuanza operesheni yake, hata hivyo CNN ilipotaka ufafanuzi wa suala hilo IDF iliieleza kuwa; “Ndani ya Jengo la hospitali hiyo kulikuwa na moto ambao tayari umeshadhibitiwa.” 
Hata hivyo, IDF imedai kwamba haina taarifa juu ya madai ya kuwa yenyewe ndiyo chanzo cha moto huo. 
Jeshi la Israel lilirejesha mashambulizi yake eneo la Kaskazini mwa Gaza Oktoba mwaka huu baada ya mzozo kati yake na Kundi la Hezbollah kupungua nguvu na hospitali hiyo ya Kamal Adwan imekuwa ni eneo la kukimbilia kwa majeruhi wa mashambulizi ya Israel.
Hata hivyo, Hamas ilikanusha madai kwamba wapiganaji wake wako ndani ya hospitali hiyo na kuuomba Umoja wa Mataifa kufanya uchunguzi juu ya madai hayo ya Israel kwa kile ilichodai IDF inalenga tu kutekeleza uhalifu dhidi ya binadamu katika eneo hilo.
“Adui yetu (Israel) anadanganya tu ili kujipenyeza na kuhalalisha unyama wake dhidi ya binadamu ikiwemo kuwaondoa wagonjwa ndani ya hospitali na kutekeleza majengo ya kutolea huduma kama sehemu ya kuwafukuza katika hospitali hiyo,” imesema taarifa hiyo ya Hamas.
Wizara ya afya ya Palestina inadai kwamba tangu kuanza kwa uvamizi wa Israel eneo la Gaza Oktoba 7, 2023, takriban wapalestina 45,484, wengi wao ni watoto na wanawake wameuawa katika mashambulizi hayo.

Wizara hiyo pia inasema Vita hiyo pia imesababisha watu 108,090 wamejeruhiwa huku zaidi ya milioni 2.3 wakiyakimbia makazi yao kutokana na mapigano hayo.

Imeandikwa na Mgongo Kaitira kwa msaada wa Mashirika

Related Posts