Dodoma. Licha ya kutajwa majina saba katika nafasi ya makamu mwenyekiti mpya wa CCM-Bara, mrithi atafahamika katika Mkutano Mkuu Maalumu wa chama hicho unaotarajiwa kufanyika Januari 18 hadi 19, 2025.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka ndani ya CCM, mkutano huo unalenga kuziba pengo lililoachwa wazi na Abdulrahman Kinana, aliyejiuzulu nafasi ya makamu mwenyekiti -Bara Julai 29, 2024.
Tangu Kinana alipojiuzulu, nafasi hiyo imebaki wazi kwa takriban miezi mitano, jambo ambalo ni la kipekee katika historia ya chama hicho.
Kwa mujibu wa Katiba ya CCM, nafasi ya makamu mwenyekiti ni muhimu katika kumsaidia mwenyekiti wa chama kutekeleza majukumu yake.
Mkutano mkuu wa Januari 2025 umepangwa rasmi kushughulikia suala hili, huku majina saba ya wana-CCM mashuhuri yakitajwa kama warithi wa Kinana.
Mbali ya hilo, ni mara ya kwanza kwa kiongozi aliyeshika nafasi hiyo kujiuzulu, hatua iliyoibua maswali kutoka kwa wachambuzi wa siasa na wanachama wa CCM.
Hata hivyo, tangu kujiuzulu kwa Kinana, sekretarieti ya chama ikiongozwa na Katibu Mkuu, Dk Emmanuel Nchimbi, imeendelea kufanya kazi bila kuyumba, jambo linaloonyesha uimara wa mfumo wa uongozi wa chama hicho.
Katiba ya CCM inaelekeza kufanyika mikutano mikuu mitatu ndani ya kipindi cha miaka mitano. Kati ya hiyo, miwili ni ya uchaguzi na mmoja ni wa kawaida wa kazi.
Mkutano mkuu wa mwaka 2022 uliomchagua Rais Samia Suluhu Hassan kuwa Mwenyekiti wa CCM ulikuwa wa kwanza kati ya kipindi cha uongozi wa 2022–2027.
Mkutano Mkuu Maalumu wa Januari 2025 unatarajiwa kufuata taratibu za kidemokrasia za CCM.
Uamuzi wa mwisho kuhusu nani atachukua nafasi ya makamu mwenyekiti -Bara unabaki mikononi mwa mwenyekiti wa chama hicho, Rais Samia.
Wanaotajwa kurithi mikoba ya Kinana ni Abdallah Bulembo, ambaye ni mwenyekiti wa zamani wa Jumuiya ya Wazazi ya CCM na mbunge. Bulembo ni kada mwenye uzoefu wa muda mrefu katika siasa za chama na Stephen Wassira, mwanasiasa mkongwe aliyeshika nafasi nyingi za uongozi ndani ya Serikali na CCM tangu enzi za uongozi wa Mwalimu Nyerere.
Mwingine ni Mizengo Pinda, Waziri Mkuu mstaafu na mwanasiasa aliyeshika nyadhifa kadhaa za uongozi ndani ya CCM na Serikali, Frederick Sumaye, Waziri Mkuu mstaafu na kada wa CCM mwenye historia ndefu ya uongozi serikalini na ndani ya chama.
Wamo pia Paul Kimiti, kada mwenye historia ndefu ya uongozi ndani ya CCM na Serikali, aliyewahi kuwa msaidizi wa Mwalimu Nyerere katika masuala ya chama na Profesa Mark Mwandosya, kada aliyeshika nyadhifa serikalini ikiwamo uwaziri, pia ndani ya CCM.
Mwingine ni Dk Emmanuel Nchimbi, Katibu Mkuu wa sasa wa CCM, aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Umoja wa Vijana UVCCM. Pia amehudumu serikalini akiwa waziri.
Kinana ni miongoni mwa viongozi wenye historia ndefu ya uongozi ndani ya CCM. Mbali na nafasi za uongozi serikalini ikiwamo uwaziri na ubunge wa Afrika Mashariki.
Mei 28, 2018, Kinana aliandika barua ya kujiuzulu nafasi ya Katibu Mkuu wa CCM kwa Rais wa wakati huo, Dk John Magufuli. Mei 29, 2018, nafasi yake ilichukuliwa na Dk Bashiru Ally.
Kinana alirejea ndani ya CCM Aprili Mosi, 2022 wakati Daniel Chongolo akiwa Katibu Mkuu na Rais Samia akiwa Mwenyekiti wa CCM.
Aliteuliwa kushika nafasi ya Makamu Mwenyekiti wa CCM-Bara, nafasi aliyojiuzulu baadaye Julai 28, 2024.
Wachambuzi wa siasa wanaona nafasi ya makamu mwenyekiti ni muhimu kwa CCM kuimarisha uongozi kuelekea uchaguzi mkuu wa 2025.
Wanasisitiza makamu mwenyekiti mpya anapaswa kuwa mtu mwenye uwezo wa kushirikiana kwa karibu na Mwenyekiti wa CCM Taifa, akihimiza mshikamano wa wanachama.
Mchambuzi wa siasa, Faraji Mayunga anasema: “Hii ni nafasi nyeti. CCM inahitaji kiongozi mwenye maono na anayeelewa mwelekeo wa chama kuelekea uchaguzi wa 2025.”
Jane Ismail, msomi wa sayansi ya siasa anasema nafasi hiyo haijawahi kushikwa na mwanamke ni vema CCM wakati huu ikaitoa kwa mwanamke.
Kwa mujibu wa Ismail, Mkutano Mkuu wa Januari 2025 utatoa dira ya uongozi wa chama hicho kuelekea uchaguzi mkuu mwakani.
“Kwa nafasi hii muhimu, matarajio ni makubwa kwamba Mwenyekiti wa CCM Taifa, Rais Samia ataongoza mchakato huu kwa weledi na busara, kuhakikisha CCM inaendelea kuwa na uongozi imara na thabiti,” amesema.