Zawadi za bibi harusi zinavyomtia unyonge mume, kuyumbisha ndoa

Mliowahi kuhudhuria au kuona sherehe mbalimbali za harusi kwenye mitandao ya kijamii, wazazi, ndugu, jamaa na marafiki wamekuwa wakitoa zawadi kubwa mbalimbali kwa maharusi.

Hii imeenda mbali zaidi kwa wanawake, ambao zamani walikuwa wakipewa vyombo na vitu vingine vya nyumbani, lakini nao sasa wanapewa zawadi za magari, nyumba, viwanja na fedha za kuanzia maisha.

Hata hivyo, inaelezwa kuwa hapa kikubwa ni mwanamke kuendelea kumheshimu mume wake kama inavyotakiwa na sio kutaka kumpanda kichwani kisa zawadi hizo, kwani haya ndiyo mwisho wa siku mwanamume huchepuka kwa kutafuta mahali ambapo ataonekana uanaume wake.

Mshauri wa uhusiano kutoka taasisi ya Mental Hygne Institute, Ramadhan Masenga, anasema zawadi zenye thamani kubwa kwa bibi harusi zinaweza kumfanya mwanamume awe mnyonge na hilo linaweza kuathiri ndoa.

Hivyo endapo hii itakuwa kinyume kwamba mwanamke ndiye yupo juu yake, basi kitu kidogo mke wake akikosea anaona ni kwa sababu kamzidi kwa vitu hivyo.

Masenga anasema kwa asili mwanamume ni mamlaka ndani ya nyumba, lakini mamlaka hiyo hatakuwa nayo kama mwanamke atakuwa na nguvu zaidi kiuchumi na kumiliki mali zilizo chini ya hema lao.

“Hivyo utakuta kwenye ndoa alitoa mahari ya Sh1 milioni, lakini siku ya binti akiagwa kwao kapewa gari yenye thamani ya Sh20 milioni, hii ni wazi atajikuta mnyonge na asiye na sauti kwa mke wake,” anasema Masenga.

Mnasihi, Bosco Bosco wa taasisi ya Mental Health Tanzania, anasema kwa kuwa mwanamume ndio mtafutaji mkuu katika familia kuna namna zawadi hizo zikitolewa kwa mke zinamuathiri.
Bosco anaenda mbali zaidi na kusema zawadi hizo zimekuwa zikiwanyong’onyeza wanaume na wakati mwingine hata kushindwa kufanya tendo la ndoa.

“Mfano kama alikuwa hana gari na mkewe kazawadiwa kwao gari ina maana itabidi akajifunze kuendesha na yeye, kama ni nyumba alijipanga kuchukua ya chumba kimoja na isiyo na uzio itabidi afanye jitihada za kutafuta nyumba yenye hadhi ambayo wataweka na gari alilopewa mkewe na inategemewa wakati huo uwezo huo anao.

“Hivyo kama hana uwezo wa kuyafanya haya yote, itakuwa inamfanya asijiamini ndani ya ndoa, kuishi maisha ya wasiwasi ukizingatia moja ya maisha ambayo tamaduni zetu zinaamini kuwa umejipata ni pamoja na kumiliki gari,” anasema Bosco.

Pia athari ni mwanamume kujilaumu kwa nini alienda kuoa familia yenye uwezo na wakati mwingine kwenda nje ya ndoa kutafuta mwanamke mwingine ambaye yeye kamzidi kiuwezo.
 

Mmoja wa maharusi ambaye hakutaka jina lake itajwe kwenye gazeti, anasema anaamini zawadi aliyopewa na wazazi wake inamhusu mume wake pia.

“Wazazi wangu kunipa zawadi sikuiona kama ina shida, kikubwa tu ni kwamba walikuwa na uwezo wa kunipa shamba la eka tano na mpaka leo tumekuwa tukilima na mume wangu,” anasema.
Mwanamina Haji, mkazi wa Mwanga, anasema alimpa mtoto wake wa kike kila kitu kinachohitajika ndani ili asije kunyanyaswa na mume wake.

“Wanaume hubadilika, akishakuchoka ndani ya nyumba anaweza kukufanyia vituko na kama ulienda kwake huna kitu siku ya kukufuza utatoka bila kitu. Hivyo nimempa mtoto wangu kila kitu, siku wakishindwana, anaweza kuvichukua na kwenda kuanzia maisha mengine,” anasema Mwanamina.
Angel Samson, mkazi wa Gongolamboto anasema wakati anaolewa alimkuta mwenza wake akiwa analala chini, hivyo zawadi alizopewa, ikiwemo kitanda ndivyo vilivyowasaidia kuanzia maisha.
Andrea Njau, mkazi wa Machame wilayani Moshi, anasema kwa muda mrefu amekuwa akichangia shughuli za wenzake wanapoozesha watoto ambapo anashuhudia wakinunuliwa zawadi kubwa, hivyo naye kujenga heshima hiyo, ilibidi afanye na kwa mtoto wake.

Zaina Mohammed, mkazi wa Arusha anasema usasa tu ndio unawasumbua wazazi, kwani mambo hayo wamekuwa wakiyaona mitandaoni, nao wanaiga bila kujua Watanzania wana mila na tamaduni zao wakati wa kuwaoza au kuwaozesha watoto.

“Ni kutokana na kuiga huko, wengine wamejikuta wakiingia katika mikopo ya kausha damu ili awaonyeshe waalikwa katika shughuli ya mtoto wake naye alimpa zawadi kubwa”.

Mtaalamu wa uchumi na biashara, Dk Donath Olomi, anasema utoaji wa zawadi hizo unawafanya waliopewa wasiende kujiamini katika maisha yao, kwani umati uliohudhuria sherehe utakuwa ukijua nyumba, gari wanalotembelea walipewa zawadi na wazazi wao na siyo kununua kwa fedha zao.
Kutokana na hilo, alishauri zawadi kama hizi ni vema wazazi wawape kimyakimya na ukumbini ibaki kuwapa vitu kama Biblia na Msahafu.

“Utaratibu huu, ndio unafanya baadaye mtu analetewa kadi za kuchangia harusi hata sita na kila moja anapaswa kuchangia sio chini ya Sh100,000, huku mshahara wake kwa mwezi hauzidi Sh1 milioni, yote hii ni kwa kuwa naye alichangisha watu ili apate hela za kumnunulia mtoto wake zawadi kubwa.

“Lakini pia watu wamejikuta wanawekeza zaidi kwenye harusi kuliko elimu na afya zao, jambo ambalo siyo zuri katika kujenga uchumi kwa mtu mmojammoja, familia na taifa kwa jumla,” anasema Dk Ulomi.
 

Mtazamo wa viongozi wa dini

Naibu Kadhi na mjumbe wa Baraza la Ulamaa wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata), Sheikh Ally Ngeruko, anasema Uislamu haukatazi kumpa zawadi mtoto anapooa au kuolewa.
“Katika hatua hii, baba au mama inakuwa ni furaha kwa mtoto wake kujitunza hadi kuingia kwenye ndoa, hivyo sioni kama kuna tabu,” anasema.

Anasema kumpa zawadi mtoto kunamsaidia kwenda kuwa na utulivu na kuweza kuishi vizuri na familia anayoenda kuijenga, huku akieleza kwa nchi nyingine huwa wanawaandalia watoto wao zawadi hizo mapema.

Aidha, aliwataka watu kuondoa dhana potofu kwamba kumzawadiwa mtoto kutamfanya asiende kutafuta chake.

Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Karagwe, Dk Benson Bagonza, anasema ndoa za siku hizi thamani yake imejengwa katika vitu na sio katika utu, upendo, heshima na kujaliana.

Ni kutokana na hilo, askofu Bagonza anasema wazazi nao wameingia kwenye mkumbo na kufikiri ndoa nzuri ni ile ambayo ina sherehe ya gharama kubwa.

“Ndoa zinaendeshwa kwa kuangalia vitu na hivyo wanandoa wanakuwa hawana muda wa kuangalia heshima ya ndoa, badala yake wanaangalia mume una nini, mke una nini na vikianza kupungua na uhusiano unakufa, kwa hiyo tusishangae idadi ya talaka ikawa ni kubwa kuliko ndoa zinazofungwa,” anasema

Aidha Askofu Bagonza anasema hili linachangia watu wasio na mali kusita kuingia kwenye ndoa.
“Siku hizi baba mzuri ni yule anayeletea watoto simu za kuchezea, baiskeli mpya, midoli mipya kila siku badala ya kulea watoto zaidi kwa kufanya kazi kwa mikono yao na kuwa na heshima kwa watu wote.

“Hivyo nashauri tuwekeze kwa kizazi hiki kipya cha watoto wadogo, kwani hiki cha watu wazima tayari kimeshaharibika,”anasema.
 

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Chama cha Wanasheria Wanawake Tanzania (TAWLA), Tike Mwambilipile anasema zawadi haijawahi kuwa tatizo, bali changamoto ya malezi aliyopata binti anayepewa zawadi hizo.

“Katika hili mzazi au mlezi unatakiwa ujiulize kabla ya utoaji zawadi hizo, je, umetengeneza mke wa aina gani au mume wa aina gani ambaye hata ukimpa hizo zawadi haziwezi kwenda kuwa sababu ya kuharibu ndoa yake.

“Vitu haviwezi kuutoa utu wa uanaume, isipokuwa kikubwa ni uwepo wa heshima katika nyumba yenu. Kwani hata kwenye vitabu vya Mungu, tumeambiwa mume na mke ni mwili mmoja, hivyo hapa haijalishi bila kujali nani anamiliki nini,” anasema.

Anasema kutokana na mabadiliko ya mfumo wa maisha, siku hizi, tofauti na zamani ambapo wanawake walikuwa wakikaa tu nyumbani kulea watoto, nao sasa wanatoka kwenda katika shughuli za utafutaji.

“Sababu wote tunaenda kuhangaika pamoja, utakuta mwanamume ananunua hiki, mwanamke ananunua kile, jambo ambalo sio baya. Pia hata mwanamume akiamua kuishi katika nyumba aliyopewa zawadi mkewe kwenye harusi, bado haimuondolei mwanamume majukumu yake ndani ya nyumba,” anasema Tike.

Hata hivyo, Tike anasema jamii inapaswa kuelewa ndoa sio kitu cha siku moja, bali ni maisha, hivyo pamoja na zawadi hizo, isimuondolee mwanamume au mwanamke kutimiza majukumu yake.
Mshauri wa malezi na uhusianom Anti Sadaka Gandi, anasema kumpa zawadi kwa kununua kila kitu kwa mwanamume ni kumwambia kijana aende kuanza maisha na vitu vingine.

Hata hivyo, anasema hayo ni matokeo ya vijana kuoa wakiwa hawapo tayari kwa majukumu hayo, hivyo mama anamsaidia kijana wake kununua kila kitu.

“Hii ni tofauti na mwanamke ambaye katika harusi akipewa vyombo vya jikoni ni sawa kwa kuwa kitamaduni inaonyesha alikuwa nyumbani anatumia vyombo vya baba na mama, hivyo anapoolewa anakwenda hana vyombo, lakini hata kama alinunua kuna kautamaduni fulani katika makabila kumtunza mtoto wa kike kwa ajili ya kwenda kuanza maisha yake mapya.

Kwa upande wa mwanamume, Anti Sadaka anasema madhara yake ni kwamba kijana huyo anakuwa hayupo katika daraja la kuwa na vitu hivyom sababu inayomfanya ashindwe kucheza nafasi yake ya uanaume na mwishowe ndoa hiyo huvunjika.

“Ushauri wangu kijana kabla hajaoa, awe ameshaandaa nyumba ya kuishi na mkewe na sio akiwa anakaribia kuoa ndio mama anajikusanya na marafiki zake kuchangishana na kumnunulia vitu,” anasema.

Pia kwa upande wa wanawake anasema nao wanapaswa kuanza kujinunulia vitu vyao, hata kama bado wanaishi kwa wazazi wao kutokana na ukweli kwamba baadhi yao kwa sasa wanapata kazi mapema.

“Ikitokea binti umepata kazi usikimbilie kununua simu za gharama, magari wakati hata sufuria za kupika ndani huna,” anasema.

Wito wake kwa wazazi, mwanasaikolojia huyu amewataka kuwalea watoto wao kuja kuwa waume bora au mke bora na kuacha kuweka thamani ya maisha kwenye ndoa badala ya thamani ya utu wao kwanza.

Anti Sadaka anavitaja baadhi ya zawadi ambazo anaweza kupewa mwanamume ni vitu vyepesi kama picha za ukutani, TV, lakini siyo kitanda.

“Unampaje mtu kitanda wakati ni moja ya msingi wa nyumba ambavyo anapaswa kununua mwenyewe,” anasema Anti Sadaka.

Related Posts