Wazazi tusherehekee ila tusijisahau kuna mahitaji ya shule

Kila mwaka, msimu wa sikukuu huja na shamrashamra nyingi, zawadi, sherehe na hamasa ya kusherehekea kwa familia.

Hata hivyo, msimu huu pia huja na changamoto za kifedha kwa wazazi wengi, hasa wanapojisahau katika matumizi na kusahau kwamba Januari inasubiri na majukumu mazito ya kifedha, yakiwemo ada za shule, sare, vitabu, na mahitaji mengine ya msingi ya wanafunzi.

Na hivi ninavyoandika, tayari sikukuu ya Krismasi ambayo huadhimishwa Desemba 25, ya kila mwaka imeshapita na familia nyingi zimeisherehekea kwa mbwembwe kedekeda.

Lakini cha kujiuliza, je, mzazi kwa mwaka huu ulizingatia kutengeneza bajeti rafiki kwa mwaka mzima inayozingatia vipaumbele? Nikiwa ofisini wiki hii, nilibungua bongo na wenzangu kwa lengo la kutaka kujua hivi wazazi wa Kitanzania wanatambua suala la bajeti ya familia na vipaumbele vyake? Kila mmoja alitoa jibu lake.

Ila nionavyo mimi, ni vema kila mzazi akawa na mpango wa kutengeneza bajeti inayojumuisha mahitaji yote muhimu, yakiwamo haya ya mwisho wa mwaka na mwanzo wa mwaka.
Katika bajeti hiyo, wanapaswa kutenga kiasi maalumu kwa ajili ya sikukuu na kiasi kingine kwa ajili ya mahitaji ya shule.

Hivyo, maadamu tumeshasherehekea sikukuu moja, basi hii ya pili, matumizi yake yasifanyike kwa kiasi kikubwa mkajisahau kwamba kuna jukumu kubwa mbele la mahitaji ya shule kwa watoto wenu.
Ni vema kuyaepuka matumizi yasiyo ya lazima kwa sababu wakati mwingine, wazazi hujihisi wanalazimika kununua kila kitu kilicho kwenye ofa au kinachoonekana kuvutia wakati wa sikukuu.
Kuna umuhimu wa kujifunza kusema ‘hapana’ kwa vitu visivyo vya msingi na mkumbuke matumizi ya sikukuu hayapaswi kuathiri mahitaji ya baadaye.

Wapo wataalamu wa fedha wanaweza kunikosoa kwamba nimechelewe kuyasema haya, lakini niwakumbushe tu wazazi kwa sababu matumizi bado yanaendelea, basi wanapaswa kulitambua hili la kuweka akiba.

Na akiba hii inaweza kusaidia kugharimia baadhi ya mahitaji ya sikukuu bila kugusa pesa zilizotengwa kwa ajili ya ada za shule.

Najua wapo baadhi tayari wanalitambua hilo, lakini wapo wengine hawalijui hili.
Hivyo wanapaswa kujifunza kununua mapema, hasa mahitaji ya shule kabla ya shule kufunguliwa Januari, mfano sare, vitabu, na vifaa vingine vinaweza kununuliwa mapema, kwa kufanya hivyo, utakuwa umeokoa kiasi fulani cha fedha, lakini pia ukaepukana na msongo wa mawazo.

Ni dhahiri kama mzazi una malengo ya kifedha ya muda mrefu itakusaidia kuepuka changamoto za kifedha zinazotokea kila Januari ifikapo.

Hujachelewa shituka, kama ulipanga kufanya matumizi makubwa mwaka mpya, chungulia bajeti yako na utazame hujafanya nini cha mwanao kwa ajili ya shule.
Rudi kwenye kibubu chako tekeleza la mtoto kwa ajili ya shule na kinachosalia, fanya matumizi kwa ajili yam waka mpya.

Ni muhimu kuwashirikisha watoto katika mipango ya kifedha. Kuwafundisha watoto kuhusu vipaumbele vya kifedha kunaweza kuwasaidia hata wao kuelewa kwa nini baadhi ya mahitaji yanaweza kuahirishwa katika shererehe hiyo yam waka mpya. Hiyo itawasaidia kuwajengea nidhamu ya matumizi ya fedha wakingali wadogo.

Tusiruhusu watoto waanze kuona namna mzazi unavyomangamanga kusaka fedha kwa ajili ya mahitaji ya shule wakati juzi tu, mliwapeleka kula starehe wakidhani baba au mama una fedha ya kutosha.

Na katika hili ndiyo pia wazazi hujikuta wakijiingiza kwenye mikopo. Lakini kama ulipanga bajeti ya vizuri, utaepukana na mikopo isiyo ya lazima inayoweza kukuleta mzigo mkubwa.
Kwa kumalizia, msimu wa sikukuu unapaswa kuwa wakati wa furaha na kusherehekea bila kuleta matatizo ya kifedha kwa familia.

Wazazi muwe na na nidhamu ya fedha, kuweka vipaumbele na kuhakikisha mahitaji ya msingi ya watoto kwa ajili ya shule Januari hii yanazingatiwa, kwa kufanya hivyo, familia inaweza kufurahia sikukuu bila wasiwasi wa kesho yao itakuwaje.

Related Posts