WAZEE wa Gusa, Achia twende kwao, leo wanashuka uwanjani kumenyana na Fountain Gate katika pambano la Ligi Kuu Bara ambayo huenda likashuhudiwa mabao mengi kutokana na timu zote kuwa na uwezo wa kutupia mipira nyavuni, huku wageni wakiwa na ukuta mwepesi ambao ukikaa vibaya utaondoka na kapu.
Mchezo huo utakaopigwa kwenye Uwanja wa KMC Complex, uliopo Mwenge Dar es Salaam ni moja kati ya miwili inayopigwa leo kabla ya ligi hiyo kwenda mapumziko hadi Januari 20 mwakani, mwingine utapigwa kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, jijini Arusha kwa wenyeji Coastal Union kuvaana na KMC.
Yanga inakamilisha mechi 15 za duru la kwanza wakiwa pia ni watetezi ambao walikuwa wakiisikilizia Simba jana ilipokuwa ikikwaruzana na Singida BS, ili kujua kama ikishinda leo itauaga mwaka 2024 na kuingia 2025 ikiwa kileleni mwa msimamo au itasalia nafasi ya pili tofauti na pointi alizonazo Mnyama anayeongoza.
Kabla ya mechi ya jana dhidi ya Singida, Wekundu wa Msimbazi walikuwa kileleni na pointi 37, ikiwa ni moja zaidi na ilizonazo Yanga yenye 36 na kama imeambulia sare au kupoteza, inamaana inaipa vijana wa Jangwani leo kupambana ili kutoka na ushindi nyumbani na kukwea hadi juu kwa kufikisha pointi 39.
Hata hivyo, kama Simba imeshinda ugenini mbele ya Singida maana yake ni kwamba hata kama Yanga itashinda kwa kishindo haiwezi kuisaidia lolote kuitoa nafasi ya pili iliyopo wakati watu wanajiandaa kuukaribisha Mwaka Mpya wa 2025.
Kwenye makaratasi unaweza kusema ni mchezo mwepesi kwa Yanga kutokana na rekodi zao bora dhidi ya wapinzani wao hao ambao tangu wameanza kukutana misimu miwili iliyopita, Yanga imeshinda mechi zote huku wakiruhusu bao moja pekee wakati wao wakifunga 11.
Fountain Gate awali ilikuwa ikifahamika kwa jina la Singida Black Stars kisha Singida Fountain Gate ambapo wakati ikiitwa majina hayo ndiyo ilicheza dhidi ya Yanga lakini kwa msimu huu hii tangu ibadili jina ndio mara ya kwanza wanakutana.
Kocha wa Yanga, Sead Ramovic huu utakuwa ni mchezo wake wa tano katika ligi kuiongoza timu hiyo ambapo nne zilizopita ameshinda zote dhidi ya Namungo (2-0), Mashujaa (3-2), Tanzania Prisons (4-0) na Dodoma Jiji (4-0) huku ushindi wa mabao 4-0 mfulululizo ukiwapa jeuri zaidi.
Yanga ambayo hapo kati ilionekana kucheza chini ya kiwango, lakini sasa imeamka ikitandaza soka safi ambalo linaweza kuwafanya Fountain Gate kupoteana mapema leo kama hawatakuwa imara.
Katika kutengeneza mashambulizi yake kuhakikisha wanapata ushindi, Ramovic amekuwa akipata jeuri kubwa kupitia Prince Dube kwani katika mabao 13 yaliyofungwa chini ya kocha huyo ligi kuu, yeye amehusika mara saba akifunga matano ikiwemo hat trick moja na asisti mbili.
Mbali na Dube, Clement Mzize naye amekuwa vizuri kwani hadi sasa amefunga mabao matano, wakati Pacome Zouzoua akiwa mkali wa asisti akiongoza kikosini hapo akifikisha nne na kufunga mabao matatu.
Si eneo la ushambuliaji pekee ambalo limekuwa na kazi ya kufunga, bali hata beki Ibrahim Hamad ‘Bacca’ naye ni mwiba mchungu kwa wapinzani kutokana na kufunga mabao manne.
Yanga itaendelea kuikosa huduma ya Maxi Nzengeli mwenye mabao matatu na Clatous Chama aliyefunga moja kwa sababu bado ni majeruhi kama ilivyo kwa kipa namba moja, Djigui Diarra ambaye nafasi yake yupo Aboutwalib Mshery aliyecheza mechi mbili bila ya kuruhusu bao.
“Tumejiandaa na mchezo huu kama tulivyojiandaa na mchezo uliopita, tunawaheshimu wapinzani, tumewaangalia wapinzani ni wagumu sana, tunachohitaji ni kwenda kuchukua pointi tatu, bila shaka wikiendi hii tunastahili ushindi.
“Ili kupata ushindi lazima upambane kwelikweli, huwezi kushinda kirahisi. Hatuangalii kilichopita, kilichopo mbele yetu ni cha muhimu zaidi,” alisema Kocha Ramovic kuelekea mchezo huo.
Ukiangalia Fountain Gate katika mechi 15 imeruhusu mabao 27 ikionyesha wazi kwamba eneo lao la ulinzi likiongozwa na nahodha Laurian Makame lina shida. Ikiwa eneo hilo lina tatizo, inakwenda kukutana na Yanga iliyofunga mabao 27 kwenye mechi 14, hivyo wana mtihani mkubwa unawakabili.
Katika kulitambua hilo, Kocha wa Fountain Gate, Mohamed Muya, amesema: “Ishu ya kuruhusu mabao inazidi kutuumiza kichwa, tunaendelea kuifanyia kazi ili kujiimarisha eneo hilo. Hata hivyo, kuna wachezaji walikosekana lakini wameanza kurudi.
“Tuna maingizo mapya kikosini, tunafahamu kwamba Yanga ina wachezaji wazuri na wanafunga mabao mengi, tumejipanga kuhakikisha hilo jinamizi la kuruhusu mabao lisitukute.”
Yanga katika mabao yake 27, inaonekana kuwa hatari zaidi kipindi cha kwanza kwani ndiyo imefunga mengi (16) wakati kipindi cha pili ikifunga 11 pekee.
Mbali na hilo, Yanga imekuwa vizuri pia kutumia dakika 15 za kwanza kwani imefanikiwa kufunga mabao matano wakati huo, hivyo wapinzani wanapaswa kuwa makini hapo.
Fountain Gate nao sio wanyonge kwani mabao yao 22 waliyofunga, 20 yamepatikana kati ya dakika ya kwanza hadi 60, hivyo wakati huo ndio kuna nguvu yao kubwa. Mabao mawili pekee yamepatikana dakika 15 za mwisho.
Timu hiyo pia imeruhusu mabao mengi dakika 15 za mwisho kipindi cha kwanza, dakika 15 za kwanza kipindi cha pili kwa maana ya kuanzia 46 hadi 60 na zile 15 za mwisho ambayo jumla yake ni 18. Katika kila muda huo, imeruhusu mabao sita.
Wakati Yanga ikitambia Prince Dube, Clement Mzize na Pacome Zouzoua katika kutengeneza na kufunga mabao yao, Fountain Gate kwa sasa ipo mabegani mwa Salum Kihimbwa ambaye amehusika kwenye mabao nane akifunga matatu na asisti tano, huku Edgar William akifunga matano. Kinara wao Seleman Mwalimu mwenye mabao sita, hatakuwepo leo kwa sababu hayupo fiti.
“Seleman Mwalimu ameumia, bado hayupo vizuri, Nicholas Gyan pia naye aliumia katika mchezo uliopita dhidi ya Namungo, hivyo wachezaji hao hawatakuwepo,” alisema kocha Muya.
Kabla ya mechi za jana, Fountain Gate ilikuwa nafasi ya sita ikiwa na pointi 20 baada ya kucheza mechi 15 wakati Yanga ni ya pili na pointi zake 36 ikizidiwa moja na vinara Simba kabla wekundu hao wajacheza dhidi ya Singida Black Stars.
Huo ni mchezo mwingine utakaochezwa leo kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha ambapo Coastal Union itakuwa mwenyeji.
Timu hizo zinakutana katika mchezo wa pili baada ya duru la kwanza matokeo kuwa sare ya bao 1-1.
Tangu msimu wa 2018/19, timu hizo zimekutana mara 13, huku mechi nane zikienda sare wakati Coastal Union ikishinda tatu na KMC imeshinda mbili.