MIRADI YA MAENDELEO INAYOENDELEA KUJENGWA ZANZIBAR INA LENGO LA KUWABORESHEA WANANCHI HUDUMA BORA NA ZA HARAKA.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Hemed Suleiman Abdulla amesema Miradi ya maendeleo inayoendelea kujengwa Zanzibar ikiwemo ujenzi wa masoko makubwa na ya kisasa ina lengo la kuwaboreshea wananchi upatiakanaji wa huduma bora na za haraka kwa Unguja na Pemba.

Ameyasema hayo wakati wa uwekaji wa jiwe la msingi katika mradi wa ujenzi wa soko la Mboga Mboga lililopo Mombasa Unguja ikiwa ni muendelezo wa shamra shamra za kutimia miaka 61 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar.

Amesema ujenzi wa soko la Mboga Mboga la Mombasa na masoko mengineyo ni maelekezo ya Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020-2025 pamoja na utekelezaji wa ahadi za Rais Dkt Hussein Mwinyi alizozitoa wakati akiomba ridha ya kuwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi mwaka 2020.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amesema Serikali inatambua kuwa upo uhitaji mkubwa wa wafanya biashara wa kuwa na maeneo bora na salama ya kufanyia biashara zao hivyo serikali inaendelea na jitihada za kuhakikisha changamoto hio inaondoka ndani ya muda mfupi ujao.

Amesema kuwa ujenzi wa masoko ya kisasa unaendana na fikra na falsafa za waasisis wa mapinduzi ambao wamekuja kumkomboa mnyonge huvyo serikali ya awamu ya nane ( 8 ) itaendelea kujenga masoko na miundombinu mengine ili wananchi wa zanzibar kuyafaidi mapinduzi kwa vitendo.

Aidha Mhe.Hemed Hemed amefahamisha kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar haitasita kuwachukulia hatua za kisheria na kinidhamu watendaji ambao hawatatimiza majukumu yao ipasavyo na kupelekea kurejesha nyuma jitihada za Rais Dkt Mwinyi za kuwaletea wananchi maendeleo pamoja na kuyaendeleza mapinduzi matukufu ya Zanzibar kivitendo.

Sambamba na hayo Makamu wa Pili wa Rais amewataka wananchi wa Zanzibar kuendelea kuhamasishana juu ya umuhimu wa kuitunza amani iliopo nchini na kuishi kwa umoja na mshikamano kwa maslahi mapana ya vizazi vya sasa na baadaee na Taifa kwa ujumla.

Nae Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Fedha na Mipango Mhe. Dkt Saada Mkuya Salum amesema ujenzi wa soko hilo ni miongoni mwa mikakati ya Rais Dkt Hussein Mwinyi ya kuwaletea wananchi wa Zanzibar maendeleo hasa katika kuwawezesha kiuchumi na kuwakwamua na umasikini.

Dkt. Mkuya amewataka wakandarasi na washauri elekezi wa ujenzi wa soko hilo kuongeza juhudi kwa kufanya kazi usiku na mchana ili soko hilo liweze kukamilika kwa wakati na kwa kiwango kilichokusudiwa ili wananchi waweze kufanya bishara zao katika mazingira mazuri na wezeshi katika kazi zao.

Aidha Dkt. Mkuya amewahakikishia wafanyabiashara wote walioondoshwa kwa kupisha ujenzi wa soko hilo watapewa kipao mbele kuhakikisha wanarudi na kuendelea na biashara zao na nafasi zitakazobakia watapatiwa wananchi kwa utaratibu utakaopangwa na wahusika.

Akisoma taarifa ya Kitaalamu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Fedha na Mipango Dkt. Juma Malik Akili amesema katika jitihada za serikali za kukuza uchumi hasa uchumi wa kati, Serikali kupitia Mfuko wa Hifadhi wa Jamhuri (ZSSF) imeamua kulijenga upya soko la Mboga Mboga na la Mombasa Unguja ili liweze kukidhi mahitaji ya watumiaji wakiwemo wafanya biashara na wananchi kwa ujumla .

Dkt. Juma amesema jumla ya shilingi za Kitanzania Bilioni 14.4 zinatarajiwa kutumika katika ujenzi wa soko hilo kubwa na la kisasa la (G+1) linalotarajiwa kumalizika mapema mwezi Machi 2025 na kuwanufaisha zaidi ya wafanyabishara 2500 ambao watafanya biashara zao ndani ya soko hilo.

Related Posts