SONGEA WAIOMBA SERIKALI KUBORESHA BUSTANI YA WANYAMAPORI RUHILA

Na Mwandishi Maalum,Songea

Wanchi wa wilaya ya Songea mkoani Ruvuma,wameishauri Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii kuboresha Bustani ya wanyamapori Ruhila Zoo ili kushawishi na kuvutia watu wengi zaidi kwenda kutembelea bustani hiyo ya wanyama.

Wamesema,licha ya Mamlaka ya udhibiti wa wanyamapori Tanzania(Tawa) kanda ya Kusini kupeleka wanyama,lakini katika eneo hilo kuna changamoto nyingi ambazo serikali inatakiwa kuzifanyia kazi ili bustani ya wanyamapori Ruhila iwe chanzo kikubwa cha mapato ya Serikali.

Aidan Komba,Mkazi wa mtaa wa Mshangano katika Manispaa ya Songea alisema,bustani ya Ruhila ikiboreshwa kwa kuwekwa miundombinu mizuri na rafiki kama maeneo mengi ya kucheza watoto,mabwawa ya kuogolea na kutembea kwa mitumbwi na wanyama wa kila aina itawashawishi watu wengi kutembelea tofauti na ilivyo sasa.


Komba mfanyabiashara wa vifaa vya ujenzi alisema,kwa muda mrefu Manispaa ya Songea haikuwa na vivutio vya utalii hivyo kuwepo kwa bustani ya Ruhila ni jambo jema hasa kwa wakazi wa Manispaa ya Songea kwa kuwa wamepata sehemu nzuri ya kwenda kufurahi na familia zao badala ya kwenda kwenye Bar ambako mazingira yake hayaruhusu kukaa na familia(mama na watoto).

Agostino Nombo,ameiomba Serikali kutupia jicho bustani ya wanyamapori Ruhila kwa kuweka mazingira mazuri ili kuwavutia watu kwenda kuona vivutio mbalimbali vilivyopo kama vile wanyama,ndege na miti aina mbalimbali iliyozunguka kwenye bustani hiyo iliyoanzishwa tangu mwaka 1973.

Alisema,ni wajibu wa Serikali kupitia wizara ya maliasili kuyaangalia maeneo ya kusini kwani licha ya kuwa na vivutio vingi kama vile Hifadhi ya Taifa ya Nyerere(Selou Game Resave),Ziwa Nyasa,na mto maarufu wa Ruvuma lakini ukanda wa kusini kama umesahaulika na hivyo vivutio vilivyopo kutochangia kiasi kidogo kwenye pato la Taifa.

Asha Abdala alisema,kama bustani ya wanyama Ruhila itaboreshwa na kujengwa kwa miundombinu mizuri,kuongezwa idadi ya wanyama na vivutio vingine itasaidia wakazi wa Manispaa ya Songea na mkoa wa Ruvuma kwa ujumla kuwa na maeneo ya kupumzika.

“Sijui Serikali yetu inashindwa nini kuwekeza nguvu kubwa katika eneo hili mbona kule Mbinga kuna bustani ya wanyamapori na wa kufugwa ya mtu binafsi ambayo inafanya vizuri na wananchi kutoka maeneo mbalimbali ya mkoa wa Ruvuma wanakwenda kutembelea kwa ajili ya kuona wanyama waliopo”alisema.

“Naiomba sana Serikali yetu, hili ni eneo muhimu kwani ni urithi kutoka kwa Mungu ambalo serikali na sisi wananchi ni lazima kulithamani na kuliendeleza kwani kituo peke yake hakiwezi kuendeleza Bustani hii na inahitaji nguvu kubwa ya rasilimali fedha ili watumishi wake waweze kutekeleza majukumu yao vizuri”alisema.

Helen Kavishe,ameipongeza TAWA kwa kuleta wanyama mbalimbali katika Bustani ya Ruhila Zoo ambapo alieleza kuwa, sasa wananchi wa Ruvuma hususani wanaoishi katika manispaa ya Songea wamepata sehemu nzuri ya mapumziko na kuwataka wananchi wenzake kuhakikisha wanakwenda kutembelea bustani hiyo ili waweze kujifunza na kujionea vivutio mbalimbali vilivyopo.

Serikali kupitia mamlaka ya usimamizi Wanyamapori Tanzania(TAWA) chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii imeleta Simba wawili majike waliopewa majina ya Lucy na Liana katika Bustani hiyo kutoka Hifadhi ya Wanyamapori ya Seva jijini Arusha ili kuchochea utalii wa ndani.

Bustani hiyo imeanzishwa kwa ajili ya wananchi wa mkoa wa Ruvuma na Watanzania kwa ujumla, kama mkakati wa Serikali ya mkoa wa Ruvuma katika kumuunga mkono Rais Dkt Samia Suluhu Hassan.

Lengo la kuanzishwa kwa Bustani ya Wanyamapori Ruhila iliyopo katika Manispaa ya Songena yenye wanyama aina mbalimbali kama vile Pofu,nyumbu Pundamilia,kakakuona,sungura,nyani,kuro na swalapala ili wananchi waweze kupata sehemu maalum ya kupumzika.

Related Posts