Unguja. Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson ameitaka Idara ya Uhamiaji kuimarisha vitengo vyake vya usalama ili kudhibiti uingiaji holela wa wageni wanaoweza kuhatarisha usalama wa Taifa.
Dk Tulia ametoa kauli hiyo leo Jumapili Desemba 29, 2024, wakati akiweka jiwe la msingi kwenye Ofisi ya Uhamiaji Dunga, Wilaya ya Kati, Mkoa wa Kusini Unguja, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 61 ya Mapinduzi ya 1964.
“Tunazungumza hapa kuhusu amani, umoja na mshikamano, lakini hatuwezi kuyafikia hayo ikiwa kuna wageni wanaingia bila mpangilio ambao wanaweza kuhatarisha amani yetu. Ni wajibu wenu, Idara ya Uhamiaji, kuhakikisha kuwa mtu anayestahili kukaa nchini anakaa na asiye na sifa hapewi nafasi,” amesema Dk Tulia.
Pia, ameitaka Idara ya Uhamiaji kuendelea kuweka mazingira mazuri kwa wawekezaji wanaokuja nchini ili wafanye shughuli zao bila usumbufu.
Amesema sekta ya utalii imeendelea kukua, hasa katika visiwa vya Unguja na Pemba, hivyo Idara ya Uhamiaji inapaswa kufanya kazi kwa bidii zaidi.
“Ikiwa kuna sheria zinazohitaji kufanyiwa marekebisho ili kuziba mianya ya vitendo vinavyoweza kuhatarisha usalama, msisite kutueleza sisi Bunge. Tupo tayari kuzifanyia kazi ili nchi yetu ibaki salama na tuendelee kunufaika na matunda ya Mapinduzi,” amesema.
Pia, ameshauri ushirikiano na wavuvi kama sehemu ya jitihada za kudhibiti magendo na uingiaji holela wa wageni wasiostahili kupitia njia za panya au baharini.
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Daniel Sillo amesema kwa miaka 61, idara hiyo imepiga hatua kwa kupanua wigo wa utoaji huduma na kuboresha vitendea kazi.
Kwa sasa, idara hiyo ina ofisi 17, vituo vya kazi tisa na majengo 15 ya wafanyakazi katika mikoa yote ya Unguja na Pemba, ikiwa na wafanyakazi 805 ikilinganishwa na wafanyakazi 25 waliokuwepo wakati wa mapinduzi na kati yao wazawa walikuwa wanne.
“Kwa dhati, tutaendelea kuishi katika kaulimbiu ya mapinduzi ya mwaka huu inayosema, Amani, Umoja na Mshikamano kwa Maendeleo Yetu,'” amesema Sillo.
Katibu Mkuu wa Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Dk Seif Islam Salum amesema mradi huo wenye ghorofa moja, umegharimu Sh1.82 bilioni.
Amesema tayari mkandarasi ameshalipwa Sh977 milioni, sawa na asilimia 53.61 ya gharama zote za mradi ulioanza kujengwa Aprili mwaka huu na unatarajiwa kukamilika Aprili 2025.
Kamishna Jenerali wa Uhamiaji, Dk Anna Makakala amesema Serikali imetenga eneo la zaidi ya mita za mraba 200,000 kwa ajili ya kujenga chuo cha uhamiaji katika Mkoa wa Kusini Unguja.
Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja, Ayoub Mohamed Mahmoud, amesema miradi hiyo inakumbusha mahali walikotoka, walipo sasa na wanakokwenda.
Amesisitiza kuwa, kila mmoja ana wajibu wa kulilinda Taifa huku akibainisha kuwa katika shamrashamra hizo, kutazinduliwa na kuwekwa mawe ya msingi katika miradi 17 yenye thamani ya Sh194 bilioni.
Wakati huohuo, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ)imesema itaendelea kujenga nyumba za maendeleo ili kuboresha taswira ya miji ya Zanzibar.
Waziri wa Uchumi wa Buluu na Uvuvi, Shaaban Ali Khamis, amesema Serikali imejidhatiti kuhakikisha makazi bora yanapatikana kwa wananchi, jambo litakalosaidia kufanikisha miji ya Zanzibar kufanana na miji mingine duniani.
Amewataka waliopata nafasi ya kuendesha shughuli za makazi na biashara katika nyumba hizo kuzitunza, kuzifanyia usafi na kuzitumia kwa mujibu wa mikataba.
“Msiache kuwachukulia hatua za kisheria wale watakaofanya uharibifu wa nyumba hizo. Wakishindwa kufuata mkataba, ni bora waziache zikiwa salama,” amesisitiza.
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba Zanzibar (ZHC), Sultan Said amesema ujenzi wa mradi huo wa ghorofa tatu umekamilisha nyumba nne za makazi na maduka manne ya biashara.
Mradi huo ulipangwa kutumia Sh650 milioni lakini umegharimu Sh400 milioni kwa kutumia makandarasi na washauri elekezi wa shirika hilo.
Said amesisitiza umuhimu wa wapangaji kulipa kodi kwa wakati na kutumia majengo hayo kwa mujibu wa sheria na miongozo ya mikataba ili kuepusha usumbufu.
Naibu Waziri wa Ardhi na Maendeleo ya Makazi, Salha Mwinyijuma amesema ujenzi huo ni sehemu ya kuunga mkono jitihada za Serikali za kuimarisha Mji Mkongwe na utalii kwa jumla. Amesema mji huo ni sura ya Tanzania na Afrika Mashariki, hivyo kuna haja ya kuhakikisha majengo yake yanavutia na yanaendana na hadhi ya urithi wa dunia.