Dar es Salaam. Wakati Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, Profesa Mohamed Janabi akiwaomba Watanzania wenye uwezo kumjengea nyumba Tabora, Hadija Shaban (24), mama wa pacha waliotenganishwa kutokana na hali yake duni ya maisha, Mwananchi imejionea hali halisi.
Hadija alirejea nchini Novemba, 2024 baada ya watoto wake Hussein na Hassan Amir, wenye miaka mitatu kutenganishwa nchini Saudi Arabia, Oktoba 5, 2023.
Ni safari ya kilomita 916 kutoka jijini Dar es Salaam mpaka Kijiji cha Kifulumo wilayani Igunga Mkoa wa Tabora, yalipo makazi ya wazazi wa watoto hao.
Ilikuwa alasiri mvua ikinyesha katika Kijiji cha Kifulumo, ndipo timu ya Mwananchi ilifika katika makazi ya Amir Jumanne (25), baba wa watoto Hassan na Hussein.
Ni nyumba ya chumba kimoja na jiko, jirani kuna zizi la ng’ombe.
Jumanne aliyefunga ndoa na Hadija mwaka 2017, anasema mtoto wao wa kwanza ana umri wa miaka saba, kabla ya mkewe kupata ujauzito mwingine ambao alijifungua pacha walioungana.
Ameishukuru Serikali kwa kuwasimamia watoto wake ambao walitenganishwa na sasa wanaendelea vizuri.
Hadija, mkewe Jumanne na madaktari wakieleza baba huyo wa watoto alimtelekeza walipokuwa Muhimbili, mwenyewe anaeleza yaliyotokea.
Jumanne anasema mkewe alipojifungua hakuwa na fedha na malipo ya huduma hospitalini yaliyomsababishia deni.
“Baada ya upasuaji waliniambia natakiwa kulipa Sh468,000, nikalipa. Wakaniambia nilipie chumba cha watoto nikalipia Sh200,000 na bado kulikuwa na gharama nyingine za kutoka nyumbani na kwenda hospitali kila siku,” anasema.
Jumanne anasema alikuwa anawasiliana na mkewe mpaka alipokwenda Muhimbili, yeye akabaki ili alipe deni.
“Nilibaki huku kwa kuwa tulikuwa na madeni, kwa hiyo nikawa nahangaika kufanya vibarua ili kulipa, maana hela nilizolipia matibabu tulikopa.
“Nilivyomaliza deni nilikwenda kumuona Muhimbili, wakaniambia nimechelewa, kwamba wamepiga picha tumetuma Saudi Arabia, hivyo sitaweza kuambatana naye, ilinibidi nirudi nyumbani,” anasema.
Jumanne anayejishughulisha na kilimo, anasema mkewe aliposafiri alikwenda kwa mwalimu mmoja kijiji cha pili ili awasiliana naye.
“Sikuwa na simu kubwa ‘smartphone’ nilikuwa napata msaada wa kuazimwa simu na mwalimu kijiji kingine ndiyo nawasiliana naye, aliporudi ndiyo nikampigia,” anasema.
Rashid Amir, mjomba wa Jumanne anasema alilazimika kumsaidia kulipa deni hilo, japo kwa tabu.
“Tunashukuru kupata msaada wa watoto kutenganishwa, baada ya kutoka hospitali deni lilifika Sh800,000 kutokana na matibabu ilituchukua muda kulipa, nilimchangia lakini haikutosha.
“Bahati mbaya nikauguliwa na mke wangu ambaye baadaye alifariki dunia, hatukuchukua muda mrefu nami nikaugua hili jicho (anaonyesha) nikafanyiwa upasuaji mara nne, kwa hiyo tukawa mbali na yule mama, msaada ukawa mgumu maana kule kuna shida na huku kuna shida,” anasema na kuongeza:
“Niwashukuru madaktari wa Hospitali ya Nkinga, Muhimbili na waliowatenganisha watoto. Tunaomba waendelee kuwapa matibabu ambayo sisi hatuwezi na wawe karibu na hospitali.”
Regina Masanja, mama mzazi wa Hadija anayeishi Kijiji cha Mizanza anasema kupungua mawasiliano kati ya mwanawe na mumewe hawezi kujua, ingawaje kijana huyo awali alikuwa na mawazo ya kukimbia kutokana na mshtuko.
“Mumewe alipoambiwa watoto wameungana alikuwa analia tu akisema anaweza kukimbia, tulimfariji nikamweleza wewe baba unalia, mkeo tumeshindwa tunataka hali yake iwe sawa ndipo tumweleze. Akasema nitawapeleka wapi,” amesema.
“Walinifuata usiku anaumwa, nikaambiwa amekataa kwenda hospitali. Nikamkuta hapo nyumbani nilimsihi twende kwenye huduma. Kufika Nkinga akapasuliwa baadaye naonyeshwa watoto wameungana,” anasema Regina.
Anasema hakujua la kufanya kabla ya mwanamke mmoja kumshauri wamtafute mbunge wa Manonga, Seif Khamis Gulamali ambaye aliwasaidia kabla ya kupewa uhamisho kwenda Muhimbili.
Regina anasema kabla ya kumfahamisha binti yake kuwa watoto wameungana alimuhurumia.
“Nikimwangalia mwanangu nilikuwa namuonea huruma, ndiyo maana sikumwambia siku nne baadaye nikamweleza. Alilia sana akasema kwa nini mlishindwa kuzaa wameungana mimi ndiyo nizae wameungana, nikamwambia mwanangu Mungu ndiyo ameamua akupe hao watoto.
“Baadaye aliniomba nimpeleke awaone, kufika akaanza kulia tulikuwa na mama mmoja mchungaji kutoka Mwisi alitufariji. Mimi, bibi yake na binti tukaanza kusali akimsihi Hadija asimkufuru Mungu, kitu ambacho kilimpa ujasiri,” anasimulia. Anasema kwa kipindi chote alitumia simu ya walimu kijijini hapo kuwasiliana na mwanawe.
“Ile siku watoto wanatenganishwa kwa kweli nilikaa hapo mwalimu mkuu alinisaidia, alinipa simu kubwa nilikaa kuanzia saa nne hadi saa 12:00 jioni,” anasimulia.
Regina anaiomba Serikali iendelee kumsaidia binti yake, kwani mazingira ya kijijini hapo si rafiki.
“Binti yangu natamani wamsaidie, Serikali wamjengee nyumba watoto wawe karibu na huduma, ninafikiria nitafute hela kidogo nikipata nitafika Muhimbili kumuona. Changamoto ni nauli. Pia huu ni msimu wa kilimo,” anasema.
Samson Kahola, baba wa Hadija anasema bila msaada wa Serikali wasingeweza. Naendelea kuiomba Serikali na wadau mbalimbali waendelee kumshika mkono binti yetu, nikisema wale watoto warudi huku mazingira ni shida.
“Tunaomba wale watoto wakae karibu na hospitali kubwa, sisi ni binadamu wakiugua watibiwe na wataalamu wanaojua tatizo lao, watengenezewe makazi karibu ili waendelee kupata huduma,” anasema. Kahola anasema binti yake aliishia darasa la saba akaolewa, kazi aliyowahi kufanya ni kulima pekee.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Mizanza, Kitongoji cha Kati, Peter Semba anasema familia hiyo ina maisha magumu haiwezi kumudu gharama za kuwatunza watoto hao.
“Mzazi wa hawa watoto ametoka familia hii na katika mazingira haya, hivyo bila msaada huu wa awali huenda leo tungeongea habari nyingine, uwepo wao sababu ya kudra za Mwenyezi Mungu,” anasema.
Hospitali ya Rufaa Nkinga iliyopo wilayani Igunga ndiko walikozaliwa Hassan na Hussein mwaka 2021.
Inaelezwa na wataalamu wa afya kwamba walizaliwa kabla ya wakati baada ya mama yao kupata uchungu ujauzito ukiwa na umri wa wiki 34.
Daktari bingwa wa magonjwa ya mfumo wa mkojo na uzazi, Geofrey Chiloleti aliyemfanyia upasuaji Hadija Agosti 25, 2021 ameieleza Mwananchi kwamba alipata mshangao alipoona watoto wameungana.
Anasema walipompokea Hadija walimpa huduma ya kwanza kumpima kujua hali ya mtoto aliye tumboni wakabaini amelala vibaya.
Dk Chiloleti anasema waliamua kumuwahisha chumba cha upasuaji baada ya kubaini amekaa katika hali ya uchungu muda mrefu.
“Njia ilishafunguka karibia sentimita 10, lakini hajifungui. Wakati tunamtoa mtoto katika tumbo la mama ndipo tukaona ni pacha walioungana. Walitoka wakiwa na miguu miwili na mmoja ni mdogo.
“Kikubwa ni kwamba walilia mapema, kwa hiyo hawakupata changamoto yoyote wakati wa kuzaliwa. Timu ya watoto wachanga ikawachukua kwa ajili ya huduma nyingine,” anasema.
Anasema mama alipohojiwa hakuwa na historia ya kuhudhuria kituo chochote cha afya wakati wa ujauzito.
Daktari bingwa wa magonjwa ya watoto katika hospitali hiyo, Jackline Suba anasema.
Walizaliwa na uzito wa kilo 3.6 tukawalaza kwenye chumba cha watoto njiti kwa kuwa walikuwa na dalili zote za kuzaliwa kabla ya wakati.
“Tuliwawekea mpira wa chakula tuliendelea kuwasiliana na madaktari bingwa wa Muhimbili, wakatuambia wanaweza kutenganishwa. Tunamshukuru Mganga Mkuu wa Wilaya na Mganga Mfawidhi wa hospitali walifanikisha watoto kufika Muhimbili,” anasema.
Dk Suba anasema changamoto ya wanawake wa eneo hilo ni kuwa hawahudhurii kliniki na wengine hufika ujauzito ukiwa mkubwa.
Habari hii imedhaminiwa na Bill & Melinda Gates Foundation.