Raia wa Russia mbaroni akidaiwa kupiga picha na kuzituma Ukraine

Russia. Raia wa Russia (jina halijawekwa wazi) amekamatwa na maofisa wa vikosi vya ulinzi na usalama nchini Russia akituhumiwa kufanya vitendo vya uhaini nchini humo.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Jumapili Desemba 29,2024 na Shirika la Ujasusi nchini humo (FSB), mtuhumiwa huyo alikutwa akipiga picha miundombinu ya nishati katika Mkoa wa Moscow na kuzituma nchini Ukraine.

Taarifa hiyo ya FSB imesema mwanaume huyo  (41) anadaiwa kutekeleza vitendo hivyo chini ya usimamizi wa Kurugenzi ya Ujasusi nchini Ukraine (GUR), ambayo ilimpa ahadi ya donge nono la zawadi iwapo angetimiza takwa hilo.

Kupitia ripoti ya tovuti ya Russian Today, FSB pia imesema mtuhumiwa huyo alikuwa akiisaidia Ukraine kukusanya taarifa za maeneo muhimu ya miundombinu ya Russia kisha kuzituma nchini Ukraine.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, mwanaume huyo alikuwa akiwasiliana na msimamizi wake kupitia mtandao wa Telegram. Tayari ameshapandishwa kizimbani na kufunguliwa kesi ya jinai yenye shtaka la uhaini.

“Raia mmoja wa Russia amekamatwa akidaiwa kutenda vitendo vya uhaini kwa kuitumikia Ukraine,” ilisema taarifa hiyo ya FSB.

Taarifa ya kukamatwa kwa raia huyo imekuja siku moja tangu Rais wa taifa hilo, Vladimir Putin aliposaini mabadiliko ya sheria ya uhaini. 

Mabadiliko hayo yanatoa hukumu ya hadi miaka 15 jela kwa raia wa kigeni atakayetiwa hatiani mwa kosa la uhaini.

Mabadiliko ya sheria hiyo pia yanaboresha tafsiri ya neno ‘Uhaini’ ambapo sasa hata wanajeshi ama raia watakaohama nchi kwenda katika taifa lenye uhasama na Russia atahesabika kuwa na kosa la uhaini.

Imeandikwa na Mgongo Kaitira kwa msaada wa Mashirika

Related Posts