IKIWA imesalia siku moja kuuaga mwaka 2024 na kuukaribisha 2025, baadhi ya mastaa wa Tanzania wanaocheza nje ya nchi wako nchini kula likizo za sikukuu.
Baadhi ya wachezaji ligi zao zimemalizika na wengine zikiwa zinaendelea wakipewa likizo ya muda kusalimia familia zao.
Nyota hao ni pamoja na Kelvin John mshambuliaji wa Aalborg FC ya Denmark, Aisha Masaka anayekipiga Brighton ya England, Abdallah Shaibu ‘Ninja’ ambaye ameachana na FC Lupopo, Shaffih Omary wa Tuzlaspor ya Uturuki.
Akizungumza na Nje ya Bongo, Kelvin John alisema wachezaji wamepewa likizo ya wiki mbili kwa ajili ya sikukuu za Krismasi na Mwaka mpya.
“Niko nchini na nitakuwa kwa wiki mbili kwa ajili ya kutembelea familia hasa kwenye hizi sikukuu za Krismasi,” alisema John.
Masaka ambaye tangu apate jeraha la bega kwenye mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Arsenal (W) Novemba 9 mwaka huu alionekana kwenye mbuga za wanyama za Ngorongoro mkoani Manyara akiinjoi maisha.
Shaffih anayekipiga Uturuki maarufu kama TFF First League alisema ameomba mapumziko ya wiki tatu kusalimia familia yake iliyopo Tanzania.
Licha ya hao kupewa likizo lakini nyota wengine wameendelea kukomaliwa kwenye timu zao wakila sikukuu ugenini akiwamo Simon Msuva (Al Talaba ya Iraq) na Mbwana Samatta (PAOK) ya Ugiriki.