Othman ahimiza uwekezaji hifadhi za misitu

Unguja. Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Othman Masoud Othman amesema ipo haja kuwekeza katika miradi ya uhifadhi misitu ili kuongeza mapato ya Serikali kupitia utalii.

Othman amesema hayo leo Jumapili Desemba 29, 2024 katika Msitu Masingini wakati akiweka jiwe la msingi la Mradi wa Utalii Rafiki na Mazingira ulioanzishwa na Jumuiya ya Zanzi Eco- Tourism ikiwa ni shamrashamra za kuelekea maadhimisho ya miaka 61 ya Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964.

Amesema dunia inapambana na athari za mazingira zinazotokana na mabadiliko ya tabianchi, hivyo kuwa na miradi mingi ya misitu itasaidia Zanzibar kukabiliana na majanga hayo.

“Uhifadhi ni muhimu, ipo haja kutunza misitu ili kuendelea kupata matokeo mazuri katika miradi hii ya uhifadhi,” amesema Othman.

Amesema ni muhimu kuendeleza jitihada za kuwawezesha wananchi kiuchumi ili kuzitumia fursa za uwekezaji zilizopo katika sekta ya utalii na kuchangia kukuza uchumi na maendeleo ya nchi.

Kiongozi huyo amesema Zanzibar kupitia rasilimali za asili kama vile misitu, upo uwezekano wa wananchi kuwekeza na kupata faida na kwamba kampuni iliyoanza kuwekeza kwenye Msitu wa Masingini imeonesha njia.

“Suala la hifadhi ya mazingira ni muhimu kwa maisha ya wanadamu, hivyo ni vyema kupanua wigo wa kuwekeza sehemu nyingine katika visiwa vya Unguja na Pemba,” amesema Othman.    

Ameitaka Wizara ya Kilimo na mamlaka zinazohusika na uwekezaji kutafuta wawekezaji wengine ili kuwekeza katika miradi rafiki na mazingira kwenye misitu tofauti ya hifadhi iliyopo Unguja na Pemba kwa kuwa, kufanya hivyo kutaweza kuleta tija zaidi kiuchumi kupitia maliasili hiyo.

Waziri wa Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo Shamata Shaame Khamis amesema mradi huo awamu ya kwanza utasaidia kukabili tatizo la uharibifu wa mazingira kwa kurejesha shukrani kwa wananchi kwa kuwapa gawio la faida linalotokana na uwekezaji huo.

Pia, amesema mradi huo unaongeza vivutio na fursa zaidi za utalii ili kufikia matumaini ya Taifa katika suala la kukuza ajira kwa wananchi.

Mmiliki wa mradi huo, Alan Peter Nnko amesema mbali mradi huo utakuwa na faida kubwa kwa wanawake ikiwamo ajira.

Related Posts