KIUNGO wa Zed FC, Mtanzania Maimuna Hamis ‘Mynaco’ amesema Ligi ya Misri imekuwa ngumu kiasi ambacho ukipoteza mchezo mmoja unasogea hadi nafasi ya chini.
Nyota huyo amezidi kuwa na kiwango bora msimu huu na ndio kiungo tegemeo ndani ya Zed FC iliyopo nafasi ya nne kwenye msimamo.
Akizungumza na Mwanaspoti, Mynaco alisema hadi sasa timu hiyo inaendelea vizuri akitaja ukidondosha pointi unashuka hadi nafasi mbili hadi tatu za chini kutokana na timu kulingana pointi.
“Ligi inaendelea vizuri na ushindani ni mkubwa sana sababu timu zenye nafasi ya juu hupishana kwa point tatu ama magoli kwa hiyo inaonyesha ni kiasi gani ligi ni ngumu,” alisema Mynaco
Al Ahly inaongoza Ligi hiyo ikiwa na pointi 60, FC Masar iliyopo nafasi ya pili ikiwa nazo 58, Wadi Degla ya tatu na pointi 45 huku chama la nyota huyo likiwa nafasi ya nne na alama 41.