MIGUEL Gamondi, aliyewahi kuinoa Yanga na kujizolea sifa kibao kwa mafanikio aliyoyapata akiwa na timu hiyo, inadaiwa ameikaushia ofa aliyopewa na AS Far Rabat ya Morocco na kukubali kutua kwa Mabingwa wa nchi hiyo, Raja Club Athletic.
Awali, kulikuwa na uvumi AS FAR ilikuwa inataka kumleta Gamondi kama Mkurugenzi wa Michezo, nafasi ya kiutawala ambayo ingempa kocha huyo jukumu la kuboresha miundombinu ya michezo na kutoa miongozo ya kimkakati kwa timu.
Ingawa ilikuwa wazi klabu hiyo ilikuwa ikifanya jitihada kubwa kumshawishi, Gamondi alionekana kuwa na mvuto zaidi kwa nafasi ya ukocha. Gamondi mwenyewe alizungumzia kwa uwazi kuhusu kipaumbele chake, akisema:
“Kurejea katika majukumu ya ukocha ni kitu ambacho nilikuwa nikikiweka kipaumbele zaidi kuliko nafasi nyingine yoyote. Soka ni sehemu ya maisha yangu, na kuendelea kuifundisha timu ni jambo ambalo linanivutia zaidi kuliko majukumu mengine yote.”
Kwa hivyo, bila kujali tetesi zinazozunguka, Gamondi alijua alichotaka, kwani baada ya kujipima kwa makini, alikataa ofa ya AS FAR na kukubali mkataba wa mwaka mmoja na nusu wa Raja Club Athletic, ambayo inashiriki katika Ligi Kuu ya Morocco na Ligi ya Mabingwa Afrika.
Mkataba huu ulitiwa saini kwa njia ya mtandao akiwa nyumbani Hispania, ambapo alikamilisha taratibu zote za kisheria. Taarifa zinaonyesha kuwa alifanya mchakato huu kwa uangalifu mkubwa, akiwa tayari kuwasili Casablanca kwa ajili ya kumaliza taratibu za mwisho na kutangazwa rasmi kama kocha mkuu wa timu hiyo.
Raja Club Athletic kwa sasa iko katika harakati za kurejesha hadhi yake kwenye soka la Afrika.