Ruto aahidi kukomesha utekaji Kenya 

Kenya. Wakati vit3ndo vya utekaji raia vikikithiri nchini Kenya Rais wa nchi hiyo, William Ruto ameahidi kukomesha vitendo hivyo vilivyolaaniwa na makundi ya kutetea haki za binadamu na wanasiasa.

Kwa mujibu wa tovuti ya Deutsche Welle, Sauti ya America (VOA) na Tuko, vyombo vya usalama nchini humo vimekuwa vikituhumiwa kuwashikilia wakosoaji wa serikali kinyume cha sheria tangu maandamano ya Juni mwaka huu.

Aidha, inaelezwa utekaji unawalenga zaidi vijana wanaomkosoa Rais Ruto kwenye mitandao ya kijamii huku polisi wakikana kuhusika na vitendo hivyo. 

Katika kukabiliana na hali hiyo Rais Ruto amesema Seerikali yake itakomesha vitendo hivyo. 
Ruto ameyasema hayo Desemba 27, 2024 wakati akizungumza huko Homa Bay.

“Tutakomesha utekaji nyara ili vijana waishi kwa amani,” amesema Ruto akinukuliwa na vyombo mbalimbali vya habari.
Aidha Chama cha Wanasheria wa Kenya (LSK) kimesema, “Ikiwa kweli polisi hawahusiki, wanapaswa kuchunguza na kuwashitaki wale waliohusika haraka,” 

Aliyekuwa Naibu Rais wa Kenya Rigathi Gachagua juzi Ijumaa amesema vitendo hivyo havifai huku akisema kimya cha Rais Ruto kinaashiria anaidhinisha utekaji nyara.

Amesema kuwa vitendo vya kikatili dhidi ya raia wanaokosoa serikali vinaashiria kuwa vyombo vya usalama vimeshindwa kutekeleza majukumu yao ya kuwalinda wananchi. 

Akizungumza na wanahabari nyumbani kwake Nyeri Ijumaa, Desemba 27, Gachagua amedai kuwa ukimya wa Rais Ruto unamaanisha kushiriki kwake kwa njia isiyo ya moja kwa moja katika vitendo hivyo vya utekaji, akimtaka awajibike kikamilifu. 

“Lazima awajibike kikamilifu na kushughulikia uvunjaji huu wa haki mara moja. 
Kubaki kimya au kutofanya chochote kunaashiria kuwa vitendo hivi vinafanywa kwa idhini.”

Related Posts