Lipumba: Rais Samia ajisahihishe Uchaguzi Mkuu 2025

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba amesema uchaguzi mkuu mwakani ni nafasi nzuri kwa Rais Samia Suluhu Hassan kusahihisha makosa ya uchaguzi wa serikali za mitaa uliofanyika mwaka huu.

Kwa mujibu wa mwanasiasa huyo, kinyume na kusahihisha makosa hayo, kuna hatari ya kutokea madhira kama inavyoshuhudiwa katika mataifa mengine Afrika kutokana na wananchi kuchoshwa na utawala unaominya demokrasia.

Kauli ya Profesa Lipumba inakuja kama msisitizo wa kukemea kile kilicholalamikiwa katika uchaguzi wa serikali za mitaa uliofanyika Novemba 27, 2024.

Katika uchaguzi huo ambao CCM ilipata ushindi wa asilimia 99.01, vyama vya upinzani vililalamikia kuenguliwa kwa wagombea wao na ukiukwaji wa misingi ya haki na uhuru.

Kutokana na malalamiko hayo, vyama hivyo vya upinzani vimekwenda mbali zaidi na kutaka uchaguzi huo urudiwe kwa madai ulikuwa batili.

Hata hivyo, katika moja ya mikutano yake na waandishi wa habari, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Mohamed Mchengerwa alisema kila kilichofanyika katika uchaguzi huo ni kwa mujibu wa sheria na kanuni.

Profesa Lipumba ametoa kauli hiyo leo Jumapili, Desemba 29, 2024 jijini Dar es Salaam alipozungumza na wanahabari, ikiwa ni salamu za kuuaga mwaka 2024 na mambo ya kutafakari kuelekea mwaka mpya 2025.

Amesema Rais Samia anapaswa kusahihisha makosa ya uchaguzi wa serikali za mitaa katika Uchaguzi Mkuu 2025, akirejea ahadi zake za kulinda demokrasia.

Amesisitiza ili kulinda heshima yake na amani ya nchi, Rais Samia ahakikishe yaliyofanyika katika uchaguzi wa mwaka 2024 hayajirudii katika uchaguzi mkuu mwakani.

“(Rais Samia) anayo nafasi ya kurekebisha dosari kwa kudhamiria kutembea katika ahadi zake za kuimarisha demokrasia na bila kujali ana ukaribu kiasi gani na wateule wake wanaomuangusha anapaswa kuwawajibisha,” amesema.

Kwa mujibu wa mwanasiasa huyo aliyebobea katika taaluma ya uchumi, uchaguzi wa 2024 ulitarajiwa kuponya majeraha ya mwaka 2019 na 2020, lakini umezidisha maumivu na kuondoa matumaini ya kuwepo kwa uchaguzi huru na haki.

“Tunaamini ilikuwepo fursa ya kuliwezesha Bunge kutunga sheria itakayoipa INEC mamlaka ya kumsimamia uchaguzi huo. Kidonda tulichooneshwa dalili za kupona na kukauka, kimeanza kurudi upya na kuvuja damu,” amesema.

Hata hivyo, Profesa Lipumba amesema haamini yaliyotokea katika uchaguzi wa serikali za mitaa wa mwaka huu ni maelekezo ya Rais Samia, bali ni hujuma za wateule wake na anapaswa kuwawajibisha.

Amesema CUF itakuwa mstari wa mbele kuhakikisha inashinikiza tume huru isimamie uchaguzi huru na haki wa mwaka 2025.

Kwa sababu maendeleo ya demokrasia yamedorora duniani, amesema Watanzania wasitegemee nchi za magharibi kushinikiza kuwepo kwa demokrasia nchini, badala yake wawajibike wenyewe kuitafuta.

Amewataka viongozi wa chama hicho kuongeza kasi ya kuimarisha chama katika ngazi zote, ili kujiweka tayari kwa uchaguzi mkuu mwakani.

Amesema ni muda kwa chama hicho kupata kura nyingi za mgombea wa urais, wabunge na madiwani ili kukiongoza nchi kwa misingi ya haki sawa.

Amemtaka Rais Samia aunde kamati ya wataalamu itakayokuwa na jukumu la kukamilisha upatikanaji wa Katiba mpya kama alivyoahidi kufanya hivyo.

Kuhusu maandalizi ya Dira ya Taifa ya mwaka 2050, Profesa Lipumba ameonya CCM isihodhi mchakato huo, ishirikishe wadau na kwamba Baraza Kuu la Uongozi la CUF litakutana kuijadili.

Kuhusu uchaguzi wa ndani wa chama hicho, amesema kati ya wajumbe 45 wa baraza la uongozi, 21 ni wanawake.

Katika hatua nyingine, Profesa Lipumba amesema hadi sasa kwa mujibu wa Benki ya Dunia, Tanzania imewekeza wastani wa asilimia 46 ya pato la Taifa, kiwango alichodai ni kikubwa.

Lakini, ameeleza pamoja na uwekezaji huo mkubwa kiwango cha ukuaji wa uchumi cha asilimia 5.7 kila mwaka, hakiakisi uwekezaji uliofanyika.

“Hiyo maana yake, uwekezaji hauna tija, kwa sababu iwapo uwekezaji ungekuwa na faida uchumi ungekuwa kwa asilimia 10,” amesema.

Amesema uwekezaji unapaswa kufanywa katika eneo dogo hadi limalizike, kisha lianze kufanya kazi badala ya kuhangaika na maeneo mengi bila kumaliza.

“Kuna uwekezaji umefanywa katika maeneo mengi, ikiwemo majengo lakini yamesitishwa yamebaki kama magofu sasa hivi,” amesema.

Akizungumzia hilo, mtaalamu wa uchumi, Dk Timoth Lyanga amesema kinachopaswa kufanywa ni kuhakikisha kila uwekezaji unaofanyika unamalizika kabla ya kuanza mwingine.

Ameeleza hiyo inatoa nafasi kwa nchi kuona matunda ya kila uwekezaji.

Kadhalika, ameshauri Serikali ihakikishe inawekeza kwenye eneo dogo inaloona itamudu gharama zake, ili ianze kunufaika badala ya kuwekeza kwenye eneo kubwa ikatumia muda mrefu kuanza kunufaika.

 “Kama ni ujenzi wa barabara, Serikali iangalie ina kiasi gani cha fedha kinaweza kujenga kilomita ngapi, basi ijenge hizo kulingana na fedha ilizonazo, itamaliza haraka na kuanza kuona matunda yake haraka,” amesema.

Related Posts