Ludewa wapata ‘ambulance’ pikipiki kuboresha afya

Njombe. Wananchi wilayani Ludewa mkoani hapa wameishukuru Serikali kwa kuendelea kuboreshea huduma bora za matibabu na kunusuru maisha yao, baada ya kukabidhiwa vyombo vya usafiri ikiwemo pikipiki mbili na gari moja la kubebea wagonjwa.

Wakizungumza wakati wa makabidhiano hayo leo Desemba 29, 2024 wananchi hao wamesema msaada huo utawaondolea changamoto kubwa iliyowakabili wanawake wajawazito na wagonjwa wengine ya kukosa usafiri wa haraka ili kuokoa maisha yao pindi wanapoumwa.

Baadhi ya wananchi wa wilaya ya Ludewa akiwemo Mary Mlelwa ameishukuru Serikali kwa kuwapatia gari la kubeba wagonjwa, kwani litasaidia kuwafikisha wagonjwa hospitali na kupata matibabu haraka hivyo kupunguza vifo visivyo vya lazima.

“Hii gari itatusaidia sana wananchi wa Ludewa hasa kinamama wajawazito na wagonjwa wengine hata ikitokea dharura mgonjwa atapata matibabu haraka,” amesema Mlelwa.

Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Ludewa, Dk Isack Chussi amesema wilaya hiyo ina vituo vingi vya afya ambavyo uhitaji wa usafiri wa vyombo vya moto ni muhimu zaidi kutokana na jiografia ilivyo.

“Hospitali, vituo vya afya na zahanati kwa ujumla vipo 81 hivyo imerahisisha kwamba mgonjwa anapopata changamoto au dharura na kutakiwa kuletwa hospitali ya wilaya usafiri huo unamfikisha haraka” amesema Chussi.

Kaimu Mganga Mkuu wa Wilaya ya Ludewa, Godlove Katemba amesema jumla ya watumishi waliopo katika sekta ya afya wilayani humo ni 450 lakini wanaohitajika ni 1400.

“Jumla ya watumishi wote tulionao ni 450 lakini wanaohitajika karibu 1400 kwa hiyo tuna upungufu mkubwa,” amesema Katemba.

Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ludewa, Castory Kibasa amesema gari na pikipiki hizo vimetolewa na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa ili kupunguza changamoto ya kusafirisha wagonjwa kutoka eneo moja la huduma hadi lingine.

“Achilia mbali magari ya kubebea wagonjwa lakini kuna pikipiki zimetolewa kwa CMT kwa ajili ya huduma za ufuatiliaji,” amesema Kibasa.

Naye Mbunge wa Ludewa, Joseph Kamonga pamoja na kuishukuru Serikali kwa kutoa gari la wagongwa pia ameahidi kuendelea kushirikiana na wananchi ili kusukuma mbele maendeleo ya wilaya hiyo.

“Mimi nilipokwenda Ludewa nilijitahidi sana kutafuta magari siyo ya halmashauri tu hata ya taasisi nyingine kwa hiyo ndugu zangu hamkufanya makosa kunituma mimi bungeni kwenda kuwasemea” Kamonga.

Related Posts