Wanandoa wafa, ajali iliyoua walimu wanne Nyasa

Songea. Wanandoa wawili ni miongoni mwa watu sita waliofariki dunia katika ajali ya gari iliyotokea wilayani Mbinga Mkoa wa Ruvuma.

Ajali hiyo ilitokea jana saa 1:10 asubuhi, baada ya gari walilokuwa wakisafiria kuanguka katika mteremko wa Chunya wilayani humo.

Wanandoa hao waliofariki dunia ni Michael Mkinga, aliyekuwa dereva na mke ni Judith Nyoni ambaye ni mwalimu.

Hayo yameelezwa leo Jumapili, Desemba 29, 2024 na Adarick Milinga ambaye ni kaka mkubwa wa Michael.

Amesema familia imepokea misiba hiyo kwa majonzi na hawajui namna watakavyowalea watoto watatu walioachwa na marehemu.

“Tupo kwenye wakati mgumu tunaomba mtuombee, ni pigo kwa wanafamilia, kwani marehemu na mkewe walikua wanategemewa na familia yetu na wameacha watoto watatu wanaosoma,” amesema.

Amesema kwa sasa wanasubiri majibu ya DNA kutoka kwa Mkemia Mkuu wa Serikali na tayari ndugu wamekusanyika wakisubiri kuihifadhi miili hiyo.

Mganga Mkuu Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga Mji, Dk Kung’e Nyamuryekung’e amesema walipokea miili sita na kuihifadhi.

“Nawaomba ndugu waendelee kuwa wavumilivu, tayari timu ya polisi mkoa imefika jana jioni na kushirikiana na madaktari kuchukua sample za miili ya marehemu na kuzituma Dar es Salaam kwa Mkemia Mkuu wa Serikali kwa ajili ya uchunguzi na majibu yakirudi ndugu watakabidhiwa miili ya wapendwa wao kwa maziko,” amesema.

Kaka wa mwalimu Dominica, Hediat Ndau amesema dada yake alikwenda Songea Desemba 24, mwaka huu kumsalimia akiwa na watoto na hiyo ilikuwa kama amekwenda kumuaga.

“Dada ni kama alifika kuniaga, Desemba 24 alikuwa hapa na aling’ang’ania kuondoka kwenda kula sikukuu Mbinga kwa wazazi…Nilimzuia sana, ila aligoma na kuondoka, masikini kumbe alikuwa anakifuata kifo,” amesema.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma, Marko Chilya amewataja waliofariki dunia katika ajali hiyo kuwa ni Judith Nyoni, Damas Nambombe, John Mtui na Dominica Ndau, wote ni walimu.

Wengine ni Michael Milinga, aliyekuwa dereva wa gari aina ya Prado yenye namba za usajili T647 CVR na Bosco Mapunda.

Related Posts