Josiah aachiwa msala Tanzania Prisons

KLABU ya Tanzania Prisons imefikia makubaliano ya kumpa mkataba hadi mwisho wa msimu huu aliyekuwa kocha wa Geita Gold, Amani Josiah, ikiwa ni muda mfupi tangu timu hiyo ya Maafande iachane na Mbwana Makata na msaidizi wake, Renatus Shija.

Taarifa kutoka ndani ya Geita Gold zimeliambia Mwanaspoti, Josiah amewaaga viongozi na wachezaji wa kikosi hicho, huku akiwatakia kila la heri katika michezo ya Ligi ya Championship iliyosalia, ili itimize malengo ya kupanda Ligi Kuu Bara.

“Ametuaga na kututakia kila la heri na sisi tumempa baraka zetu zote, bado tulikuwa tunamuhitaji ila kama unavyojua haya ni maisha tu, tumemruhusu na tunamshukuru kwa utumishi wake kikosini kwetu,” alisema mmoja wa viongozi wa Geita Gold.

Kwa upande wa Josiah alipotafutwa na Mwanaspoti kuzungumzia suala hilo, alisema hawezi kuweka wazi moja kwa moja kama kweli anaenda kujiunga na Prisons, kwani hadi sasa hakuna mazungumzo yoyote ingawa yakitokea kila mtu atafahamu.

“Nasikia tu hizo taarifa kama unavyoniambia mdogo wangu, nikiri kukiwa na hayo mazungumzo ya kwenda huko utakuwa mtu wa kwanza kujua ila hadi sasa hakuna jambo hilo, tuvute subra kwa sababu muda ukifika kila kitu kitajulikana tu,” alisema.

Licha ya kauli ya Josiah, ila Mwanaspoti linatambua kocha huyo wa zamani wa Biashara United amefikia makubaliano hayo na muda wowote kuanzia sasa atatangazwa kwa ajili ya kukiongoza kikosi hicho cha Maafande wa Mbeya hadi mwishoni mwa msimu.

Hadi anaondoka Geita Gold, Josiah ameiongoza timu hiyo katika michezo 14 ya Ligi ya Championship ambapo ameshinda tisa, sare mitatu na kupoteza miwili, akiiacha nafasi ya pili na pointi 30, nyuma ya vinara Mtibwa Sugar yenye pointi zake 35.

Licha ya Prisons kutoa taarifa ya kuachana na Makata juzi, ila Mwanaspoti linatambua kocha huyo alitimuliwa Desemba 20, baada ya timu hiyo kuchapwa mabao 2-0, dhidi ya Singida Black Stars, mechi iliyopigwa Sokoine jijini Mbeya Desemba 16.

Baada ya Makata kuondoka timu hiyo ikakabidhiwa kwa kocha msaidizi, Shaban Mtupa aliyesimamia katika michezo miwili ya Ligi Kuu akianza na kichapo cha mabao 4-0, dhidi ya Yanga Desemba 22, kisha ushindi wa bao 1-0 na Pamba Jiji Desemba 26.

Makata alikiongoza kikosi hicho katika jumla ya michezo 14 ya Ligi Kuu Bara kwa msimu wa 2024-2025, ambapo kati ya hiyo alishinda miwili tu, sare mitano na kupoteza saba, ambapo alikiacha kikiwa nafasi ya 15, kwenye msimamo na pointi 11. 

Related Posts