Arusha. Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Monduli mkoani Arusha wameonyesha kutoridhishwa na uongozi wa katibu wa chama hicho wilayani humo, Rukia Omary wakimtuhumu kukigawa chama hicho na kusababisha migogoro.
Hata hivyo, akijibu tuhuma hizo, Rukia amesema vita hiyo inatengenezwa na baadhi ya viongozi wenye nia ya kugombea ubunge mwaka 2025.
“Wala hakuna shida ndani ya CCM wilaya, hiyo sarakasi zote unazoona ni kampeni za mapema zinazofanyika na baadhi ya watu ambao ukiwakataza ndio wanaona unawanyima fursa wanatengeneza vikundi vya watu kufanya mambo haya,” amesema.
Hata hivyo, amesema ana ushahidi wa kila kitu kati ya hivyo wanavyomtuhumu navyo.
Hayo yametokea jana katika kikao cha kawaida cha Halmashauri Kuu ya CCM wilayani humo, kilicholenga kujadili ajenda ya utekelezaji wa ilani ya chama hicho na hali ya siasa.
Hata hivyo, ajenda zilizopangwa hazikujadiliwa baada ya wajumbe kutaka katibu huyo atoke kwa kile wanachomtuhumu kuwa, chachu ya migogoro ndani ya chama hicho.
Awali, Mwenyekiti wa CCM wilayani humo, Wilson Lengima aliamua kusikiliza hoja hizo binafsi, badala ya zile zilizopangwa.
Mmoja wa wajumbe hao, Ngalama Napena alisema ni vigumu kujadili lolote kabla Rukia hajaondoka wilayani humo na kwamba hawamtambui.
Alidai kuwa, uongozi wake unakiuka kanuni za chama hicho na anasababisha migogoro kati ya viongozi wa CCM wa kata na mitaa.
“Hatuna imani naye, amekuwa akikanyaga katiba kwa kupendelea baadhi ya viongozi na kusababisha migogoro kati yetu na mbaya zaidi baada ya kumwambia hatumhitaji akasema hawezi kuondoka,” amesema.
Alisema wameshapeleka malalamiko yao kwa viongozi wa ngazi ya mkoa na Taifa na wameahidiwa linafanyiwa kazi.
Katibu wa CCM Kata ya Naalarami, Saning’o Laizer amesema mwenendo wa katibu wao umekidhoofisha chama hicho ngazi ya wilaya na kuwagawa viongozi.
“Mfano anakuja kata anazungumza na katibu wa tawi, lakini haisemwi kwa mwenyekiti wa chama mtaa au kata, pia haongei na mwenyekiti wetu wa wilaya wala kushiriki shughuli zote anazoitisha hii inatufanya tuchukiane sisi kwa sisi,” amesema Laizer.
Katibu wa CCM Kata ya Lemooti, Saning’o Lootha amesema hawaridhishwi na kiongozi huyo kwa kuwa amekusanya fedha za kodi ya shamba kwa mwaka na kujipangia matumizi bila kuwashirikisha.
“Na hata ukimuuliza mapato na matumizi hakupi majibu mazuri zaidi matokeo yake ofisi ya kata ina kitega uchumi lakini hainufaiki kwa chochote,” amesema.
Akizungumzia hilo alipozungumza na Mwananchi leo, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Arusha, Thomas Ole Sabaya amesema tayari suala hilo linashughulikiwa.