Bagamoyo. Bagamoyo ni miongoni mwa miji yenye historia kubwa nchini, na hii inatokana na umaarufu wake ulioanzia karne ya 18.
Simulizi mbalimbali zinaonyesha kuwa mji huo ulikuwa ni kituo cha kusafirisha watumwa waliokuwa wakitoka mikoa mbalimbali na hata nchi jirani kueleka Ulaya kupitia Zanzibar.
Hata hivyo, inaelezwa kuwa awali eneo hilo halikuitwa Bagamoyo kama linavyotamkwa hivi sasa bali wenyeji walilitamka kwa jina la Bwagamoyo.
Kadri siku na miaka ilivyozidi kwenda jina la Bwagamoyo liliendelea kufutika midomoni mwa watu na kubaki na Bagamoyo.
Hashimu Mwalimu mwenye umri wa miaka 77 ni mmoja wa wazawa wa Wilaya ya Bagamoyo, anayesema eneo hilo ni miongoni mwa maeneo yaliyotumiwa na wageni kupitisha mizigo mbalimbali ikiwemo pembe za ndovu, na kwamba waliosababisha jina la Bwagamoyo kubadilika na kuitwa Bagamoyo ni Waingereza.
“Historia fupi niliyoipata na kuisikia wakati mwingine kwanza unajua Bagamoyo huko nyuma walipita Waarabu baadhi ya maeneo wakayatawala ikiwemo eneo linaloitwa Kaole”anasema.
Anasema kuwa mbali na hivyo pia eneo hilo ilikuwa njia kuu ya biashara ya pembe za ndovu na biashara ya watumwa ambayo hata hivyo ilikuja kuzuiwa na Wajerumani.
Anasema wakati wa utumwa, kuna watumwa waliokuwa wakipata mwanya wa kuwatoroka Waarabu na kuingia kwenye makazi ya wazawa.
Anasema kuwa baadhi ya wazawa walipokuwa wakiwahifadhi watumwa hao, walizoea kuwaambia kuwa wamefika mahala salama hivyo wabwage mioyo.
“Wenyeji ambao ni babu zetu walikuwa wanawaambia watumwa waliotoroka kutoka mikononi mwa Waarabu, wakisema ndugu zetu msiwe na wasiwasi bakini ndani bwageni miyoyo kwani mko mikononi salama, msiwe na wasiwasi, “anasema.
Anasema kuwa jina hilo lilidumu kwa kipindi kirefu hadi wazungu walipofika na kutawala na kwamba kilichowashinda ni lafudhi ya Bwa na wao wakatamka Ba, hivyo kuitwa Bagamoyo mpaka sasa.
“Walishindwa kutamka Bwagamoyo wakawa wanasema Bagamoyo na ndilo jina likashika mzizi hadi leo vizazi na vizazi vimeendelea kuita Bagamoyo,” anasema.
Anasema kuwa raia hao wa kigeni waliiacha Bagamoyo na mwonekanao tofauti, kwani walijenga majengo mbalimbali waliyoyatumia kwa shughuli zao.
Anasema wakati Mjerumani anatawala, ikulu ya Tanganyika ilikuwa Bagamoyo na walijenga jengo kubwa, ambalo mpaka sasa lipo na hata kuacha makaburi yao yaliyoko eneo la Mwakalenge mjini humo.
Winifrida Msaki ambaye ni mhifadhi wa malikale, anasema kuwa wakoloni walijenga majengo mbalimbali ambayo yameendelea kutumika na kuleta mchango kwa Serikali kwa nyanja za uchumi na kijamii.
“Mbali na pato kwa Serikali, hata wananchi wananufaika na uwepo wa majengo haya kwa kuwa watalii wakija hapa Bagamoyo, wananchi wanapata jira ya kuwaongoza na hata kuuza bidhaa mbalimbali,” anasema.
Anasema jina la Bagamoyo lina mchango wa kuitambulisha Tanzania kimataifa, hasa kupitia watalii.