Rekodi zambeba Mzize Yanga | Mwanaspoti

HAZUNGUMZWI sana, lakini namba alizonazo katika timu ya Yanga zinambeba, Clement Mzize aliyegeuka kuwa mshambuliaji hatari na muhimu wa kikosi hicho kilichopo chini ya kocha Sead Ramovic.

Mshambuliaji huyo mzawa licha ya kuletewa mastaa wengi wa kigeni ndani ya timu hiyo, bado ameonekana kuuwasha na namba alizonazo kulinganisha na mastaa hao anaocheza nao nafasi moja Jangwani.

Akiwa na msimu wa tatu tangu alipopandishwa akitokea timu ya vijana, Mzize amezidi kuwa mtamu akimfunika hadi Kennedy Musonda anayelingana muda wa kuitumikia timu hiyo, ikipita mikononi mwa makocha Nasreddine Nabi na Miguel Gamondi kabla ya kuja kwa Ramovic ambapo amezidi kuwa mtamu.

Katika misimu mitatu ya Ligi rekodi zinaonyesha Mzize amemkimbiza Musonda ambaye amekuwa akiimbwa kwenye kikosi hicho, kwani amehusika katika mabao 25 (kabla ya mechi ya jana), akifunga mabao 16 na asisti tisa, wakati Musonda akifunga jumla ya mabao 11 na asisti mbili ndani ya misimu hiyo mitatu kwa Ligi Kuu.

Katika msimu wa Mzize msimu wa kwanza wa 2022/23 alikuwa sehemu ya kikosi kilichoipa timu hiyo taji la Ligi Kuu akifunga mabao matano na kutoa pasi moja iliyozaa bao, hivyo alihusika kwenye mabao sita kati ya mabao 43 yaliyofungwa na timu hiyo huku Fiston Mayele (Yanga) na Saidoo Ntibanzonkiza (Simba) wakiibuka wafungaji bora baada ya kupachika mabao 17 kila mmoja. Kwa Musonda rekodi zinaonyesha msimu huo akiingia katika dirisha dogo, alifunga mabao manne bila ya asisti, ilihali katika msimu wao wa pili, Mzize alifunga mabao sita na kuasisti saba, akimuacha mbali Mzambia huyo aliyefunga mabao matano na asisti mbili.

Kwa msimu huu wakati Musonda ndio kwanza akianza kurejea tena kutoka kwenye majeraha ana mabao mawili bila ya asisti, wakati Mzize akiwa ameshafunga mabao matano na asisti moja (kabla ya mechi ya jana), japo kwa rekodi za mechi za kimataifa kwa misimu hiyo mitatu wawili hao hawachekani, japo Mzambia ametisha zaidi.

Related Posts