Marekani. Rais wa 39 wa Marekani na mshindi wa Tuzo ya Amani ya Nobel, Jimmy Carter amefariki dunia usiku wa jana Desemba 29, 2024 akiwa na umri wa miaka 100.
Kwa mujibu wa tovuti ya CNN, Carter alikuwa chini ya uangalizi wa madaktari kwa kipindi cha zaidi ya mwaka mmoja.
Mbali na sifa nyingine za Carter, pia aliwahi kuandika historia ya kupanda Mlima Kilimanjaro mwaka 1988, ambapo kwa mujibu wa tovuti ya Los Angeles Times, mwaka huo alifanikiwa kufika katika kilele cha Gilman.
Carter alikuwa Rais wa Marekani kwa kipindi cha muhula mmoja, kuanzia 1977 hadi mwaka 1981, huku akisifika kwa kuwa msuluhishi wa migogoro duniani, jambo lililomfanya atunukiwe Tuzo ya Amani ya Nobel mwaka 2002.
Historia inaonyesha kuwa Carter aliyekuwa kada wa chama cha Democrats, ndiye Rais pekee wa Marekani aliyevunja rekodi ya kuishi umri mrefu.
Ifuatayo ni baadhi ya migogoro ambayo Carter alihusika katika kuitatua: Mgogoro kati ya Israel na Misri uliohusu vita, eneo la Sinai, na hatima ya Palestina mwaka 1978, mgogoro wa Korea Kaskazini mwaka 1994 kuhusu matumizi ya nishati ya nyuklia.
Mgogoro mwingine aliohusika kuusuluhisha ni ule wa mwaka 2005 wa Vita vya wenyewe kwa wenyewe kati ya Sudan na vikosi vya Sudan Kusini.
Baada ya kutoka madarakani, Jimmy Carter aliendelea kushiriki kazi za kibinadamu kupitia Carter Center, ambapo alifanikisha pia usuluhishi wa migogoro midogo, kufuatilia uchaguzi wa kidemokrasia duniani, na kupambana na magonjwa kama Guinea Worm Disease.