Bashe atangaza vita dhidi ya ‘cartel’ kwenye tumbaku

Dar es Salaam. Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe, , ametoa maelekezo yenye lengo la kukabili ‘cartel’ kwenye zao la tumbaku, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha magunia yenye thamani ya zaidi ya Sh1.4 bilioni yanarejeshwa kwa wakulima.

Magunia hayo yamekamatwa katika operesheni ya Serikali kwenye mikoa ya Tabora na Shinyanga baada ya kuuzwa tena kwa wakulima badala ya kurudishwa kwao kama wamiliki halali.

Waziri Bashe pia ameelekeza watuhumiwa 15 wanaoshikiliwa na vyombo vya usalama kuhusiana na uuzaji haramu wa vifangashio hivyo washughulikiwe kama wahalifu wa uhujumu uchumi.

Ameelekeza kusimamishwa kwa viongozi wa vyama vya ushirika vya singi (Amcos) na wa vyama vya ushirika wanaoshikiliwa kuhusiana na kadhia hiyo kupisha uchunguzi.

Aidha, ameelekeza wakurugenzi wa kampuni za ununuzi wa tumbaku kusaidia kutambua watumishi wao waliohusika katika uuzaji wa mara ya pili wa vifungashio hivyo maarufu mkoani Tabora kama ‘majafafa’ na maghala yaliyohifadhi bidhaa hiyo yafungwe kwa kusaidia kufanikisha uhalifu.

Waziri Bashe amesisitiza kwamba hakutakuwa na makato yoyote kutoka kwa malipo ya wakulima kwa ajili ya vifungashio katika msimu wa biashara ya tumbaku wa 2024.

Maelekezo hayo yametolewa kwa viongozi wa mikoa ya Tabora na Shinyanga, vyombo vya ulinzi na usalama vilivyoendesha awamu ya kwanza ya operesheni hiyo likiwemo Jeshi la Polisi, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Ofisi ya  Makosa ya Jinai Mkoa (RCO), Usalama wa Taifa (TIS) Mkoa, Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na Jeshi la Akiba.

Operesheni hiyo imelenga kupambana na mifumo ya unyonyaji kwa wakulima katika sekta ya tumbaku nchini.

Akizungumza na waandishi wa habari mkoani Tabora, Bashe amesema ‘cartel’ hiyo imehusisha wadau wakuu katika uchumi wa tumbaku mkoani humo, licha ya kuonywa na Serikali.

Amesisitiza kuwa vifungashio vya tumbaku (magunia) ni mali ya wakulima na vinapaswa kurudishwa kwao kupitia Amcos husika baada ya wanunuzi kufikisha bidhaa walizonunua viwandani mwao.

“Ni wizi kuuza tena magunia kwa wakulima ambao wanapaswa kuyapokea kama mali yao,” amesema Bashe.

Amebainisha kuwa wakulima wa tumbaku katika mikoa inayozalisha zao hilo wametumia kati ya Dola za Marekani milioni 5 hadi Dola za Marekani milioni 7 kwa mwaka kuagiza vifungashio toka nje ya nchi.

Ameongeza kuwa wakulima wanakatwa kilo moja kwa gunia kama gharama ya ziada kwa ajili ya vifungashio hivyo.

Vifungashio hivyo vimeandikwa majina ya wakulima na dokezo kuhusu Amcos wanazotoka ili kurahisisha ufuatiliaji na kuhakikisha vinarudi baada ya mazao kufikishwa sehemu iliyokusudiwa.

Mfumo huu umeundwa ili kurahisisha urejeshwaji wa vifungashio na pia kudhibiti ubora wa bidhaa inayouzwa hivyo kulinda soko la tumbaku nchini.

Jinsi ‘cartel’ inavyofanya Kazi

Bashe amesema wafanyabiashara, viongozi wa Amcos na vyama vya ushirika na wanasiasa wametengeneza ushirikiano katika kufanikisha uuzaji mara ya pili wa vifungashio hivyo kwa bei ya hadi Dola 4 za Marekani kwa gunia badala ya kurudisha kwa wamiliki halali (wakulima).

Amesema zaidi ya magunia yenye thamani ya Sh1.4 bilioni yamekamatwa katika operesheni hiyo, na kwamba watu 15 wanaotuhumiwa kuhusika na biashara hiyo wanashikiliwa na vyombo vya ulinzi na usalama.

“Operesheni dhidi ya ‘cartel’ hii imekuwa ngumu kwa miaka miwili iliyopita,” amesema Bashe, na kuongeza, “swali kubwa kwa Bodi ya Tumbaku ya Tanzania (TTB) na Tume ya Maendeleo ya Ushirika ya Tanzania (TCDC) likiwa mahali mifuko iliyotumika misimu iliyopita inakoenda.”

“Endapo mifuko 100,000 ilitumika msimu uliopita, mifuko 20,000 pekee inapaswa kuagizwa msimu mpya kwani zaidi ya 80,000 inapaswa kurudi kwenye mzunguko toka msimu uliopita,” ameongeza Waziri Bashe, na kubainisha kuwa tumbaku ni tofauti na mazao mengine ambayo vifungashio vinakuwa mali ya mnunuzi.

Awamu ya pili ya operesheni

Katika mkutano huo, Bashe ametangaza kuanza kwa awamu ya pili ya operesheni, ambayo itajikita katika kubaini viongozi wa vyama vya ushirika wanavyowanyonya wakulima, kupitia mikopo wanayochukua kwa ajili ya ununuzi wa pembejeo na vifungashio.

Amesema awamu ya pili ya operesheni itahusisha mikoa mingine inayolima zao hilo ikiwemo Katavi, Mbeya, na Kigoma, ambapo wahasibu watakagua kiasi cha fedha  kilichopendekezwa na wakulima, kiwango kilichopitishwa na viongozi wa Amcos, na maombi ya fedha yaliyotumwa kwenye taasisi za kifedha na viongozi wa juu wa ushirika.

“Tumegundua kuwa viongozi wa vyama vya ushirika, wanaoidhinisha mikopo ya wakulima, wamekuwa wakiidhinisha kiasi kikubwa tofauti na maombi ya mkulima kwa faida zao binafsi, hivyo kuwapa wakulima mzigo mkubwa wa makato ya mikopo hiyo,” amesema Waziri Bashe.

“Katika awamu hii, wahasibu watalinganisha pembejeo na vifungashio vilivyopokelewa na wakulima, kiasi kilichoombwa, kiasi kilichoidhinishwa na Amcos na viongozi wa ushirika kwenye taasisi za kifedha,” ameongeza.

Uchunguzi huu unalenga kuhakikisha uwajibikaji na kupunguza unyonyaji katika sekta ya tumbaku.

Kuongezeka kwa uzalishaji wa tumbaku

Uzalishaji wa tumbaku nchini umeongezeka kutoka tani 50,000 hadi tani 122,858 katika mwaka wa 2023/2024.

Kufikia Desemba 2023, thamani ya mauzo ya tumbaku nje ya nchi ilikuwa Dola za Marekani milioni 316 huku lengo likiwa Dola za Mrekani milioni 400.

Uzalishaji unatarajiwa kufikia tani 200,000 msimu wa 2024/2025, huku matarajio ni kuzalisha tani 300,000 mwaka 2025/26.

Related Posts