BONDIA wa ngumi za kulipwa nchini, Hassan Mgaya, amefariki dunia usiku huu muda mchache baada ya kupewa rufaa ya kupelekwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kutoka Hospitali ya Mwananyamala.
Kifo cha bondia huyo kimetokea baada ya juzi Jumamosi Desemba 27, 2024 kupigwa katika pambano lililofanyika kwenye Ukumbi wa Dunia Ndogo, Tandale jijini Dar es Salaam.
Mweka Hazina wa Chama cha Mabondia, Cosmas Cheka ameeleza kuwa Mgaya amepatwa na umauti wakiwa katika harakati za kumuhamisha kwenda Muhimbili kutokana na hali yake kubadilika baada ya mchana wa leo Desemba 28, 2024 kupelekwa Hospitali ya Palestina iliyopo Sinza, kisha Mwananyamala.
Inadaiwa chanzo cha bondia huyo kuwa katika hali mbaya kabla ya kufikwa na umauti ni baada baada ya jana kupigwa ngumi nyingi za kichwa katika raundi ya tano na mpinzani wake Paul Elias kabla ya kuanguka kisha kung’ata ulimi kuzama.
Baada ya tukio hilo, alipatiwa huduma ya kwanza na kurejea katika hali yake ya kawaida ambapo asubuhi ya leo Jumapili hali ilibadilika na kukimbizwa hospitali.
Bondia huyo anakuwa wa pili kufariki dunia hapa nchini kwa siku za karibuni baada ya pambano kufuatia mwezi uliopita mchezo wa ngumi kumpoteza bondia Abbasi Mselem aliyefariki kufuatiwa kupigwa katika pambano lake Zanzibar.