MIONGONI mwa makipa mahiri Afrika kwa sasa ni Djigui Diarra anayeidakia Yanga na timu ya taifa ya Mali akisifika kwa ubora wa kuanzisha mashambulizi, pia kuokoa michomo inayolenga lango lake.
Pamoja na ubora huo, Diarra amekuwa akikutana na kadhia kutoka kwa mshambuliaji wa Simba, Kibu Denis wanapokutana kila mtu akiwa kazini kwake.
Kibu ndiye mchezaji wa Simba aliyefunga mabao mawili kwenye mechi mbili mfululizo za watani wa jadi na mabao yote akimfunga Diarra anayekuwa langoni kwa Yanga.
Staa huyo aliyetua Msimbazi msimu wa 2021/2022 akitokea Mbeya City hakuifunga Yanga katika msimu wake wa kwanza, lakini msimu uliopita aliitungua sambamba na msimu huu.
Kibu anayesifika kwa kasi na ubora kwenye kurudi nyuma kukaba alianza kuifunga Yanga Aprili 16 mwaka jana kwenye mechi ya duru ya pili ya Ligi Kuu na chama lake lilishinda 2-0 akifunga bao la pili dakika ya 32 ya mchezo baada ya beki Henock Inonga kufunga bao la kwanza dakika ya kwanza.
Bao hilo alilofunga kwa kiki kali ni miongoni mwa mabao mawili aliyoyafunga Kibu msimu uliopita lingine akiifunga Geita Gold katika ushindi wa mabao 5-0.
Kabla ya hapo msimu uliopita 2021/22 Kibu alikuwa ameifungia Simba mabao manane na kuwa kinara wa kupachika mabao kwenye kikosi hicho.
Msimu huu, yupo tena kikosini Simba na tayari ameifunga Yanga na kipa ni yule yule Diarra bao la kufutia machozi kwenye kichapo cha 5-1 ilichokipata katika mechi ya ligi duru la kwanza na wikiendi hii mchezo wa mkondo wa pili atakutana tena na Yanga ambayo langoni kwake atakuwepo Diarra. Nini kitatokea? tusubiri kuona kwenye dabi Aprili 20.
Ikumbukwe tangu ameifunga Yanga kwenye ligi Novemba 5 mwaka jana, licha ya kupata nafasi mara kwa mara kwenye kikosi cha Simba lakini Kibu hajafunga bao tena kwenye ligi. Ana bao moja tu.
Inspector Haroun amtabiria
Akiongea na mwanaspoti kwa njia ya simu, nyota wa muziki wa Hip Hop nchini Haroun Rashid Kahena ‘Inspector Haroun’ amesema mchezo wa dabi ya Kariakoo anaona kabisa Kipu akiitungua tena Yanga kwani ana uwezo huo na nguvu.
“Mchezo wa mwisho watani zetu walitufunga ingawa Kibu Dennis alifunga. Amekuwa strong na anafanya vizuri licha ya kutokufunga kwenye baadhi ya mechi za ligi na zile za kimataifa ingawa ana bahati kwenye mechi za Yanga na Simba.