Neema ya Kariakoo Dabi kiuchumi

Achana na burudani wanayopata mashabiki wa soka nchini inapokuja Dabi ya Kariakoo, lakini ukweli, pambano hilo la watani wa jadi nchini, limekuwa na neema kubwa kwa wachuuzi na wafanyabiashara waliopo kando ya Uwanja wa Benjamin Mkapa na maeneo ya jirani.

Wakati leo pambano hilo likitarajiwa kupigwa kuanzia saa 11:00 jioni tayari wafanyabiashara wadogo wadogo na wale wakubwa wanaomiliki baa na hata waendesha bodaboda wameshakaa kaa tayari kutengeneza pesa kupitia pambano hilo la marudiano la Ligi Kuu Bara litakalopigwa Kwa Mkapa.

Biashara kama wakaanga chips, mama Ntilie, wauza maji, wachoma nyama, wauza jezi zinazohusiana na klabu hizo mbili nao wameshaa mkao wa kula kwa kutambua siku ya neema imewadia na wale wanaendesha baa zilizopo eneo hilo la Mkapa huenda hata oda zao safari hii zitakuwa ni zaidi ya zile za kawaida kwani wanajua wanywaji na walaji wapo na wameongezeka kabla na baada ya pambano hilo la 112 kwa timu hizo katika Ligi Kuu Bara tangu 1965.

Katika mchezo huo wa leo, Yanga ndio wenyeji baada ya mchezo wa kwanza uliopigwa Novemba 5 mwaka jana watani wao, waliubeba na kufumuliwa mabao 5-1 na kusababisha mabosi wa Msimbazi kumtimua kazi, Kocha Mbrazili, Roberto Oliveira ‘Robertinho’ na kumleta Abdelhaki Benchikha kutoka Algeria atakayeiongoza kwa mara ya kwanza Simba katika pambano hili.

Mwanaspoti limefika hadi nje ya Uwanja wa Benjamin Mkapa na kushuhudia hali halisi na kuzungumza na wafanya biashara wa chipsi, bodaboda, machungwa na jezi, walikuwa na haya ya kusema.

Muuza chipsi aliyejitambulisha kwa jina la Hamis Emmanuel anasema bei ya vyakula inaongezeka na wanapata wateja wengi, hivyo kwao inakuwa ni siku ya neema.

“Mfano chipsi kavu tunauza Sh2500 kutoka 2000, chipsi mayai Sh3000 kutoka 2500, kipaja cha kuku cha Sh2000 kinauzwa 2500, wakati kidali cha Sh2500 kinauzwa Sh3000, kutokana na watu kuwa wengi na wanakuwa hawana muda wa kuhoji bei, akili zao zinakuwa kwenye mechi,” anasema Emmanuel

Anasema kila inapokuja Dabi huwa wanafika saa 12:00 asubuhi kuweka mazingira sawa na kama walikuwa wananunua gunia moja la viazi, wanaongeza idadi yanaweza kuwa mawili hadi matatu.

“Huwa tunajua kuna ongezeko la wanunuzi, hivyo hata mzigo unaongezwa na kusema kweli Dabi imekuwa ikituongezea mapato na hata pale kunapokuwa na mechi kubwa hapa Kwa Mkapa,” anasisitiza.

Mama Lishe aliyejitambulisha kwa jina la Mama Happy anayeuza msosi nje ya uwanja huo, anasema;

 “Angalau mechi za dabi nakuwa na uhakika wa kupata pesa ndefu, kama nilikuwa nauza kilo nne kwa siku basi naweza nikanunua 10, tayari nimeanza kujipanga kuweka mazingira yangu vizuri.”

Mwanaspoti limetembelea kijiwe cha bodaboda, kilicho nje ya uwanja huo, wamekiri kupata changamoto na faida zikicheza Simba na Yanga.

Muendesha bodoboda aliyejitambulisha kwa jina la Faris Yasin ambaye ni shabiki wa Simba, anasema mechi ya dabi anapata kiasi Sh40,000 hadi 50,000, tofauti na siku za kawaida ambapo inakuwa ni ngumu kupata pesa hiyo.

“Changamoto ukimpata mteja ambaye timu yake imefungwa, ukimtajia kiasi ama ukimuuliza maswali mengi anakuwa mkali, hata njiani yeye ndiye anakuwa anakwambia kata kona kule, nenda huku hadi ukifika anapokwenda unakuwa umechoka sana,” anasema Yasin.

Anaulizwa unaona mchezo wenyewe utakuaje na vipi matumaini kwa timu yako? Anajibu “Dabi ni Dabi haijalishi Simba inapita kwenye changamoto gani, dakika 90 zitaamua mchezo.”

Bodaboda mwingine Said Mohamed anasema japo anaishabikia Simba kibiashara Yanga ikishinda wanapiga pesa ndefu, kwani mashabiki wake wanakuwa wanakaa baa hadi saa 7:00 asiku.

“Pamoja na ushabiki, lakini lazima nyumbani uache pesa ya kula, familia inakutegemea, ni kweli nakuwa naumia Simba ikifungwa, ila kibiashara bora Yanga ishinde nakuwa napata pesa ndefu ambayo inakimu majukumu yangu,” anasema Mohammed na kuongeza;

“Simba ikishinda mashabiki wake wanaondoka muda huo huo, ndio tunakuwa tunapata wateja ila siyo kama Yanga ambao wanabakia baa hadi usiku wa manane, hivyo lazima watahitaji usafiri.”

Kwa upande wa muuza machungwa aliyejitambulisha kwa jina la Mohamed Saleh anasema Simba na Yanga zikicheza inakuwa neema kwao, walaji wanakuwa wengi, ingawa kuna wakati mwingine wahuni wanakuwa wengi, umakini ukiwa mdogo wapo wanaoweza kula bila kulipa.

“Japo sijawahi kuibiwa, ila nimeona wenzangu wakilizwa hadi simu, kikubwa ni umakini, ili kuhakikisha biashara inakwenda sawa,” anasema.

Kwa upande wa muuzaji wa jezi, aliyejitambulisha kwa jina la Khamis Ally ambaye ni shabiki wa Yanga, anasema;

“Biashara za jezi haziwi nzuri siku ya dabi, kwani kunakuwa na presha kubwa ya watu kununua tiketi, tofauti na siku za kawaida watu wananunua.”

Related Posts