Arusha. Wilaya ya Longido inatarajia kutumia Sh8 bilioni kufunga kamera za barabarani kwa lengo la kukabiliana na uhalifu na kuimarisha usalama.
Taa hizo zitafungwa kuanzia ulipo mpaka wa Tanzania na Kenya wa Namanga hadi eneo la Engikaret.
Hayo yalisemwa jana jioni, Desemba 29, 2024 na Mkuu wa Wilaya ya Longido, Salum Kali alipozungumza kwenye maombi maalumu ya kuombea amani ya wilaya hiyo na Taifa kwa ujumla, yaliyofanyika katika viwanja vya Polisi Longido.
Amesema barabara hiyo ambayo pia wanyamapori hupita, itawekwa kamera hizo ili kuongeza usalama.
“Tunajenga mtandao wa kamera za barabarani kuanzia Namanga hadi Engikaret, ukimkanyaga tembo tunakuona hata ukikimbia pesa utatupa na lazima ufuate mashrti ya kupita kwenye hii barabara. Niwaombe tuendelee na maombi kuombea pia Taifa letu,” amesema.
Viongozi wa dini mbalimbali pamoja na wale wa mila waliongoza maombi hayo, huku msisitizo ukiwa katika utendaji haki, ulinzi wa amani ya nchi.
Mwenyekiti wa kamati ya amani wilayani humo, Sheikh Ramadhani Mpangala, aliwataka watumishi, wakiwemo askari polisi pamoja na maofisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), kuwa waadilifu na kuhakikisha hawaruhusu magendo kupita.
“Barabara yetu hii ni kwa ajili ya kuendesha shughuli zetu wala si sehemu ya kupitisha magendo au kitu ambacho kitamdhuru mwanadamu mwenzako.
“Tunaposema magendo ikiwa wewe ni polisi kuwa mwadilifu, ikiwa wewe TRA kuwa mwadilifu, dhibiti hali hiyo na hiyo ndiyo hofu ya Mwenyezi Mungu,” amesema.
Naibu Waziri wa Madini na mbunge wa jimbo hilo, Dk Steven Kiruswa, alisema wako tayari kuungana na viongozi wa dini kumuomba Mungu aendelee kudumisha tunu za Taifa ambazo ni umoja, amani na mshikamano.