Rais Georgia agoma kung’oka ikulu, mrithi wake aapishwa

Georgia. Mikheil Kavelashvili ambaye ni Rais mteule wa Georgia ameapishwa leo kuanza kulitumikia taifa hilo huku mtangulizi wake akigoma kutoka Ikulu ya taifa hilo.

Mikheil ameapishwa jana Jumapili Desemba 29, 2024, katika viwanja vya Bunge la taifa hilo Jijini Tbilisi, huku waandamanaji wanaomuunga mkono Rais anayemaliza muda wake, Salome Zourabichvili wakifurika mitaani.

Wakati Mikheil akiapishwa, Salome alikuwa akihutubia maelfu ya waandamanaji waliokusanyika nje ya Ikulu ya taifa hilo kuwa hamtambui rais mteule huyo kwa kile alichodai hakuingia madarakani kwa njia halali.

“Ulaghai unaoendelea ndani ya ukumbi wa Bunge kwa kweli haukupaswa kuonekana wala kutendwa katika taifa letu,” amesema Salome.

Kwa mujibu wa Salome, uteuzi wa Mikheil kama Rais wa taifa hilo ni batili mwa sababu wabunge waliompigia kura ya kuongoza taifa hilo wametokana na uchaguzi uliofanyika Oktoba mwaka huu uchaguzi ambao anadai uligubikwa na utata.

Salome ambaye ni mfuasi wa sera za mataifa ya Magharibi na waandamanaji wanaomuunga mkono wanaomba ipigwe kura ya kutokuwa na imani na Rais Mikheil anayeunga mkono sera za Russia.

Chama cha Georgian Dream anachotokea Mikheil na Tume ya Uchaguzi ya ya nchi hiyo wanadai kuwa uchaguzi wa Oktoba ulikuwa huru na wa haki.

Mikheil (53) ambaye ni mwanasoka mstaafu aliyewahi kuchezea klabu ya Machester City nchini Uingereza, amekula kiapo chake akiahidi kuilinda Katiba ya Georgia.

Vyombo vya habari nchini humo vimeripoti kuwa wakati wa kuapishwa kwa Mikheil, hakuna waandamanaji waliozingira bungeni badala yale wanaomuunga mkono rais Salome ndiyo walienda hadi ilipo Ikulu ya taifa hilo.

Chama hicho tawala ambacho kinaongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya uwakilishi Bungeni kimesema Mikheil ni Rais aliyeingia madarakani kwa njia halali.

Pia kimetishia kumsweka Salome gerezani endapo atakomalia katika Ikulu ya taifa hilo jijini Tbilisi.

Serikali ya sasa inayoongozwa chini ya chama cha Georgian Dream inatajwa kuelekeza vipaumbele vyake nchini Russia, jambo lililoibua maandamano miongoni mwa wafuasi wa Rais anayeondoka madarakani ambaye kipaumbele chake ilikuwa kuifanya Georgia kuwa mwanachama wa Jumuiya ya Ulaya (EU).

IMEANDIKWA NA MGONGO KAITIRA KWA MSAADA WA MASHIRIKA.

Related Posts