Dodoma. Dereva wa bodaboda, Kelvin Joshua (27) na Tumaini Msangi (28) ambaye ni bondia, wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Dodoma wakikabiliwa na kesi ya mauaji ya kukusudia ya mtoto Greyson Kanyenye (6).
Washtakiwa hao wakazi wa Ipagala, Jijini Dodoma, wamefikishwa mahakamani hapo leo Jumatatu, Desemba 30, 2024 mbele ya Hakimu Mkazi, Denis Mpelembwa.
Akiwasomea mashtaka, wakili mwandamizi wa Serikali, Patricia Mkina amedai wanakabiliwa na shtaka la mauaji ya Greyson Kanyenye, yaliyotokea Desemba 25, 2024 katika mtaa wa Ilazo Kata ya Ipagala, Jijini Dodoma.
Baada ya kusomewa mashtaka hayo, Hakimu Mpelembwa amesema mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza mashauri ya mauaji, hivyo hawatakiwi kujibu chochote.
“Kosa la mauaji halina dhamana, hivyo mtarudi mahabusu hadi kesi yenu itakapotajwa tena Januari 13, 2025,” amesema Mpelembwa.
Mtoto huyo wa mfanyabiashara Zainab Shaban, maarufu Jojo alikutwa amefariki dunia usiku wa kuamkia Desemba 25, 2024 nyumbani kwa rafiki yake ambaye ni Ofisa Uvuvi Mtera, Hamis Mpeta, Ilazo Extension jijini Dodoma.
Awali, akitoa taarifa ya mauaji hayo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, George Katabazi alisema Desemba 25,2024, saa 1:00 asubuhi, Mpeta akiwa na mama wa mtoto Zainab walibaini mtoto huyo kuuawa baada ya kurejea kutoka matembezini.
“Walimkuta mtoto huyo akiwa ameuawa kwa kupigwa na kitu kizito kichwani na shingoni amekatwa na kitu chenye nja kali. Katika tukio hilo ni kwamba mama wa mtoto alimuacha mtoto huyo chini ya uangalizi wa dereva bodaboda anayejulikana kwa jina la Kelvin Gilbert,” alisema.
Alisema walimuacha mtoto huyo na dereva bodaboda saa 6.00 usiku, nyumbani kwa Mpeta, lakini waliporudi walikuta mtoto ameuawa na dereva huyo hakuwepo.