Unguja. Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Zanzibar (ZDCEA) kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama imekamata kilo 798.89 za dawa za kulevya.
Aina ya dawa zilizokamatwa katika operesheni maalumu nne tofauti zilizofanywa kuanzia Oktoba mwaka huu ni pamoja na bangi, cocaine, heroin, methamphetamine na shisha zilizochanganywa na dawa za kulevya aina mbalimbali huku watuhumiwa watano wakitiwa mbaroni.
Wakati kikikamatwa kiwango hicho cha dawa za kulevya, Novemba 11, 2024 mamlaka hiyo ilitoa tamko la kutaifisha mali za watuhumiwa wa dawa za kulevya zenye thamani ya Sh976.05 milioni ambazo zimethibitika kuchumwa kupitia biashara ya dawa hizo.
Akitoa taarifa kwa vyombo vya habari leo Desemba 30, 2024 ofisini kwake, Kamishna Mkuu wa Mamlaka hiyo, Kanali Burhani Zuberi Nassoro amesema katika operesheni hiyo wamevunja rekodi ya kukamata dawa za kulevya aina ya methamphetamine zenye uzito wa kilo 536 kiwango ambacho hakijawahi kukamatwa katika historia ya Zanzibar.
“Operesheni hii ya nne ilifanyika Novemba 15, 2024 katika eneo la Kisauni, Wilaya ya Magharibi B, Mkoa wa Mjini Magharibi.
“Katika operesheni hiyo mamlaka imefanikiwa kuvuja rekodi yake ya Januari 2024, mara hii tumefanikiwa kukamata dawa za kulevya aina ya methamphetamine zenye uzito wa kilo 536 na heroin kilo moja zilizokuwa zimehifadhiwa katika nyumba iliyopo eneo la Kisauni,” amesema.
Kwa mujibu wa mamlaka hiyo Januari mwaka huu alikamata kilo 115 za dawa za kulevya aina ya methamphetamine na bangi.
Amesema dawa hizo zilikuwa zimewekwa katika vifungashio vyenye majina ya bidhaa nyingine kama chocolate, organic coffee, cocoa na green tea ili kukwepa kutiliwa shaka wakati wa kusafirisha.
Kwa mujibu wa Kanali Burhani, dawa hizo zingefanikiwa kuchepushwa na kuingia mtaani zinaweza kutengeneza kete milioni 27, wakati idadi ya watu wote Unguja na Pemba ni milioni 1.8 kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022.
Kete hizo ukigawa kwa idadi ya watu unapata wastani wa kete 14 kwa kila mtu aliyepo Zanzibar.
Operesheni ya kwanza, ilifanyika Oktoba 17, 2024 katika eneo la Bandari ya Majahazi Malindi, ambapo walifanikiwa kukamata watuhumiwa wawili: Haji Suleiman Ali (18) na Mbaraka Rajab Kiee (34) wote wakazi wa Mungani wakiwa na dawa za kulevya aina ya bangi zenye uzito wa gramu 734.95 zilizokuwa zimefichwa katika boti.
Katika operesheni iliyofanyika Novemba 5, 2024, katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume, walifanikiwa kukamata shisha boksi 15 sawa na pisi 300 zenye uzito wa kilo 263 zilizoingizwa nchini kutoka China na mtuhumiwa Alperen Karakurum raia wa Uturuki mkazi wa Dar es Salaam.
“Shisha hizo zilifanyiwa uchunguzi wa kitaalamu katika maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali na kubainika kuwa ndani yake kuna kemikali tofauti ikiwemo ya bufotenin.
“Kemikali hiyo inapumbaza akili ya mtumiaji na kusababisha athari za kiafya ikiwemo magonjwa ya moyo, uraibu, kiwewe na kuchanganyikiwa hali inayoweza kusababisha mtu kujidhuru au kudhuru watu wengine,” alisema
Kanali Burhani amesema kupitia operesheni hiyo, mamlaka imefanikiwa kuzuia kuingizwa nchini kwa shisha nyingine zaidi ya boksi 295 ambazo ndani yake kuna pisi 59,000 zenye uzito wa gramu 500 sawa na nusu tani zilizokuwa tayari zimeshalipiwa na mfanyabiashara huyo kwa ajili ya kuingizwa Tanzania kutoka China.
Operesheni iliyofanyika tarehe hiyo hiyo usiku, eneo la Kilimani Chini alikamatwa mtuhumiwa Ali Mohamed Ali (Ali Macho), akiwa na dawa za kulevya aina ya cocaine zenye uzito wa gramu 87.223 na gari aina ya Toyota Alphad.
Pia, katika eneo la Mtendeni walifanikiwa kumkamata mtuhumiwa Fahad Ali Khamis akiwa na dawa za kulevya aina ya cocaine zenye uzito wa gramu 111.6678.
“Niwahakikishie kuwa, mamlaka ninayoiongoza kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama tumejipanga vyema mwaka 2025 tutaendelea kusambaratisha mitandao mikubwa na midogo ya wahalifu wa dawa za kulevya, vinginevyo wajisalimishe na kuacha uhalifu huo,” amesema.
Khadija Salum Ali, mkazi wa Unguja amesema waathirika wakubwa wa dawa hizo ni vijana ambao ndio nguvu kazi ya Taifa.
“Hatua hizi hatuna budi kuzipongeza, lakini bado kazi ni kubwa ukiangalia vijana wengi ndio watumiaji wa hizi dawa za kulevya hata mitaani tunakutana nao wanavuta bangi, kwa hiyo bado ushirikiano wa pamoja unahitajika kutokomeza kabisa janga hili,” amesema.