Maabara MOI yatunukiwa ithibati ya ubora kimataifa

Dar es Salaam. Maabara ya Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI), imetunukiwa cheti cha ithibati cha ubora wa kimataifa cha utoaji huduma za maabara.

Cheti hicho (ISO 15189:2012) kimetolewa Oktoba 2024 na Shirika la Viwango vya Ubora wa Maabara kwa nchi za Kusini mwa Afrika (SADCAS).

Hayo yamesemwa leo Jumatatu, Desemba 30, 2024 na Mkurugenzi Mtendaji wa MOI, Dk Mpoki Ulisubisya baada ya kutunukiwa cheti hicho, huku akielezea umuhimu wa ubora wa vipimo kwa wagonjwa na nchi kwa ujumla.

Amesema cheti hicho kitavutia utalii tiba, utakaochangia kukuza uchumi, kuongeza mapato ya Serikali pamoja na ajira kwa Watanzania.

Dk Ulisubisya amesema MOI imejiimarisha kwenye vituo vya tiba vinavyotegemewa barani Afrika kwa kuwa inawavutia wagonjwa kutoka nchi za jirani, na hata mataifa mbalimbali kuja nchini kutibiwa.

“Kupata ithibati ya ubora ni hatua muhimu katika kuhakikisha wananchi wa kawaida wanapata huduma bora zinazolingana na viwango vya kimataifa hapa nchini bila kulazimika kusafiri nje ya nchi,” amesema Dk Ulisubisya.

Amesema majibu ya vipimo vya maabara yanayotolewa na MOI yana ubora wa hali ya juu na usahihi uliothibitishwa kimataifa ambayo inajenga imani kwa wagonjwa nchini na kutoka mataifa mengine.

Dk Ulisubisya amesema kupitia huduma za kimataifa, taasisi hiyo itawasaidia kuokoa gharama za matibabu nje ya nchi kwa Watanzania na kuongeza mapato ya Serikali kupitia wagonjwa wanapotembelea Tanzania kwa matibabu.

Kutokana na uwekezaji uliofanywa na Serikali, ikiwemo ununuzi wa vifaa vya kisasa vya maabara, hivyo wagonjwa watatumia muda mfupi kusubiri majibu ya vipimo ili kuongeza tija katika kuwahudumia wagonjwa wengi kwa ubora na viwango vya kimataifa.

Kwa upande wake, Mkuu wa Idara ya Maabara (MOI), Nsiande Ndoso amesema taasisi hiyo ilianzishwa mwaka 1996, kipindi chote haikuwa na ithibati ya ubora.

Ndoso amesema mwaka 2021 walianza mchakato wa kutafuta ithibati hiyo ya kimataifa na mwaka huu wamefanikiwa kupata baada ya kutimiza miongozo iliyotakiwa.

Amesema maabara imepata uthibitisho wa kimataifa juu ya utendaji kazi ya kufanya chunguzi mbalimbali kwa kuwa vipimo vinavyofanyika hapa nchini, ni sawa na vipimo mahali pengine.

Related Posts