NDANI ya Ligi Kuu Bara achana na nani anataka kuwa bingwa, kuna vita fulani zinachukua nafasi taratibu nje na kuwania taji la ubingwa.
Zitazame vita nane ambazo zinapatikana kivyake kwenye msimu huu wa ligi hiyo ukiwa unaelekea ukingoni ambazo zimekuwa zikizalisha ushindani mwingine.
Simba kamchapa Azam juzi kwa mabao 3-0 ukiwa ni mchezo ambao ulikuwa unalenga kutoa picha ya nani anaweza kushika nafasi ya pili ambapo sasa wekundu hao kama watashinda kiporo chao kimoja itafikisha pointi 59 na kuwaacha Azam kwa pointi mbili.
Hapa bado ligi ngumu kwa timu zote kwani baada ya kiporo hicho kila timu itakuwa imesalia na michezo minne kumaliza msimu ambazo zitatoa nani anajihakikishia nafasi hiyo ya kwenda kucheza Ligi ya Mabingwa Afrika msimu ujao na nani atakwenda Kombe la Shirikisho.
Mshambuliaji wa Yanga Joseph Guede ana mabao matano sawa na Freddy Kouablan wa Simba ambaye naye kaweka wavuni idadi kama hiyo, hawa jamaa wawili wote wameingia msimu huu kupitia usajili wa dirisha dogo.
Walianza taratibu sana kiasi cha kuleta presha ya kama ulikuwa usajili sahihi lakini ghafla wamebadilisha upepo fasta na wanaendeleza ligi yao ya nani atakuwa kinara wa mabao kati yao ingawa ni ngumu kuongoza kwa jumla kutokana na kuachwa mbali na vinara Aziz Ki na Feisal Salum ambao kila mmoja ana mabao 15.
Vita nyingine iko kwa makipa wawili, kipa bora kwa misimu miwili mfulilizo Djigui Diarra wa Yanga ambaye mpaka sasa msimu huu ameshajikusanyia cleen sheet 13 akiwa ndiye kinara akifuatiwa na Mkongomani Ley Matampi wa Coastal Union mwenye cleen sheet 11.
Hapo kati Matampi alikuwa akiongoza na wawili hao walikuja kuachana juzi tu baada ya timu zao mbili zilipokutana, Diarra akamuacha hapo na kuendelea kukimbia na mechi zilizobaki zitaamua nani atachukua cleen sheet nyingi zitakazokwenda kuamua nani atakuwa kipa bora mwisho wa msimu.
Mbio zingine ngumu msimu huu zipo kwenye kasi ya kuwania Tuzo ya Ufungaji Bora, hili litaamuliwa na viungo washambuliaji Stephane Aziz Ki wa Yanga na Feisal Salum ‘Fei Toto’ kutoka Azam kila mmoja akiwa na mabao 15.
Aziz Ki alipambana kufunga kwenye mchezo uliopita dhidi ya Kagera Sugar lakini mambo hayakuwa rahisi akatoka kapa, vivyo hivyo kwa Fei Toto ambaye alijikuta akishindwa kufunga bao lake la 16 baada ya kukosa mkwaju wa penalti wakati timu yake ilipokutana na Simba Mei 9. Nani atakuwa mfungaji bora? Hilo litakuwa kwenye uamuzi wao lakini uhakika ni kwamba msimu huu mfungaji bora atakuwa kiungo baada ya wawili hao kumuacha mbali kidogo mshambuliaji pekee Waziri Junior wa KMC alinayefuatia akiwa na mabao 11.
Vita nyingine ipo hapa kwa nani atakuwa kinara wa kutoa asisti msimu huu, anayeongoza mpaka sasa ni Kipre Junior wa Azam mwenye asisti 8.
Nyuma yake wako ndugu zake ambao wanawatumikia wapinzani wao Yanga, Kouassi Yao mwenye asisti saba sawa na Aziz KI, kazi bao inaendelea hapo nani atakuwa bora kuliko mwingine, majibu tutayapata baada ya ligi kumalizika.
Kuna mchuano mwingine mkali wa kuwania nafasi ya nne kwenye msimamo wa ligi hapa nako kutakucha kwani ukiacha wanaokimbizana kwa karibu Coastal Union aliyeko hapo na pointi zake 37 kuna Tanzania Prisons chini yao akiwa na pointi 33 sawa na KMC.
Hata hivyo nje ya timu hizo kuna zingine zinaweza kushika nafasi hiyo ya nne itategemea tu watamalizaje mechi zao zilizosalia na walio juu yao watamalizaje ambazo ni Namungo (30), JKT Tanzania (30), Kagera Sugar (30), Dodoma Jiji (29), Singida Fountain Gate (29) na Ihefu (29).
7. Mashujaa vs Geita Gold
Mchuano mwingine ni ule unaopasua kichwa wa nani atakimbia nafasi ya kucheza play off kati ya Mashujaa waliopo nafasi ya 13 na pointi zao 26 na Geita Gold waliopo nafasi ya 14 na pointi zao 24, kumbuka kwamba watakaomaliza ligi nafasi hii watalazimika kucheza play off kuamua hatma ya kubaki ligi kuu.
Timu hizo zinapigana na vita hiyo ngumu na kuondoka hapo wanatakiwa kutafuta ushindi kwenye mechi zao nne au tano zilizosalia kwenye kumaliza ligi huku wakiwaombea dua mbaya ya kuendelea kupoteza walio juu yao au wale walio chini yao kwenye msimamo.
Vita ya mwisho iko kule chini ya msimamo hapa washindani wawili ni Tabora United aliyepo nafasi ya 15 akiwa na pointi zake 23 dhidi ya Mtibwa Sugar waliopo mkiani kabisa na pointi zao 20 ligi ikimalizika leo timu hizo zikiwa hapo maana yake kwamba zimeshuka moja kwa moja.
Njia ya kukimbia mtego huo ni moja tu wote kushinda mechi zao zilizosalia ambapo kinyume na hapo Tabora itarudi ligi iliyotoka msimu uliopita huku Mtibwa ambao wamekuwa wakinusurika kwa msimu wa pili sasa kutoshuka safari hii Championiship itakuwa imewapenda zaidi.