Songea. Jeshi la Polisi Mkoa wa Ruvuma linamsaka dereva wa kampuni ya mabasi ya Superfeo, Zacharia Mbunda, kwa tuhuma za kusababisha ajali iliyotokea leo alfajiri na kujeruhi abiria wanne.
Majeruhi hao wamelazwa katika Hospitali ya Wilaya ya Tunduru kwa matibabu, hali zao zinaendelea vizuri.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma, Marko Chilya, akizungumza na Mwananchi leo Jumatatu, Desemba 30, 2024, amesema ajali hiyo imetokeo leo saa 10 alfajiri katika Kijiji cha Kadewele, Kata ya Mchangani, Tarafa ya Mlingoti, Wilaya ya Tunduru.
“Basi lenye namba za usajili T.1966 DRT, aina ya Yutong, lililokuwa likiendeshwa na Zacharia Mbunda, likitokea Dar es Salaam kuelekea Songea, liligonga kwa nyuma lori lenye namba za usajili T.955 DGG, aina ya Scania, lililokuwa likiendeshwa na Juma Mohamedi Malindi (21), mkazi wa Dar es Salaam,” amesema kamanda huyo.
Amesema ajali hiyo imesababisha pia uharibifu wa magari yote mawili na majeruhi. Amewataja majeruhi kuwa ni Francis Komba (21), mkazi wa Matarawe, Asia Ponela (75), mkazi wa Namtumbo, Zuberi Ally (55), mkazi wa Songea, na Christopher Kazimoto (13), mkazi wa Songea.
Kamanda Chilya amesema chanzo cha ajali ni uchovu na usingizi wa dereva wa basi, hali iliyosababisha ashindwe kuzuia gari lake kugonga lori kwa nyuma.
Amesema dereva huyo amekimbia baada ya tukio hilo na juhudi za kumsaka zinaendelea.
Kamanda Chilya ametoa wito kwa madereva na wamiliki wa vyombo vya moto kuhakikisha wanachukua tahadhari, hasa kipindi hiki cha mwisho wa mwaka, kwa kufuata sheria na kanuni za usalama barabarani, ili kuepuka ajali zisizokuwa za lazima.
“Nawasihi wamiliki wa mabasi ya safari ndefu, hususani za usiku, kuhakikisha magari yao yana madereva zaidi ya mmoja ili mmoja anapochoka apumzike na mwenzake aendelee na safari, lengo ni kuhakikisha usalama wa abiria,” amesema Kamanda Chilya.