Wanavyuo jamii ya kimasai waunda umoja kutokomeza mila potofu

Mbeya. Wanafunzi wa vyuo vikuu na vya kati mkoani Mbeya wameunda Umoja wa Jamii ya Masai (Memasa), wenye lengo la kupinga mila potofu na kuhamasisha elimu katika jamii hiyo.

Wakizungumza na Mwananchi leo Jumatatu, Desemba 30, 2024, wanafunzi hao wamesema umoja huo utakuwa suluhisho kwa changamoto zinazokwamisha haki ya elimu kwa vijana wa jamii hiyo, badala ya kuendelea kushikilia ndoa za utotoni, shughuli za kilimo na ufugaji kama njia pekee za maisha.

Mwenyekiti wa umoja huo, Mkapa Laizer amesema jamii ya kimasai kwa muda mrefu haijatoa kipaumbele cha kutosha kwa elimu, jambo linalosababisha changamoto nyingi za kimaendeleo.

Amesema kupitia Memasa, watajitahidi kufanikisha mapambano dhidi ya mila potofu zinazokwamisha maendeleo ya elimu.

“Tunawakaribisha wanafunzi wapya katika umoja huu, ambapo pamoja na sherehe, tunakuwa na majadiliano yenye lengo la kila mmoja kuwa balozi wa kufikisha ujumbe kuhusu umuhimu wa elimu kwa wazazi na walezi,” amesema Laizer.

Amesema mila za kuona mtoto wa kike kama mtu wa kuolewa, kulima, au kufanya shughuli za ufugaji zinapaswa kufutwa na badala yake mtoto apewe haki ya kupata elimu, ili akabiliane na mabadiliko ya teknolojia na kujitambua.

Asnath Almas, mwanafunzi wa mwaka wa kwanza Chuo Kikuu cha Mzumbe, amesema matarajio yao ni kuona umoja huo ukileta mabadiliko makubwa, hasa kwa watoto wa kike ambao mara nyingi huwa wahanga wa mila kandamizi.

“Tamaduni potofu kama ukeketaji zinapaswa kufutwa kwa kuwa zinamuathiri msichana moja kwa moja. Kupitia Memasa, tunatarajia kuona usawa wa kijinsia katika jamii yetu,” amesema Asnath.

Yolita Ayoub, mwanachama wa Memasa, amesisitiza umuhimu wa mshikamano katika kufanikisha malengo ya umoja huo. Amesema jukumu lao ni kusaidiana wakati wa changamoto na kushauriana kuhusu masuala ya elimu.

“Mila potofu zitaondoka iwapo tutashirikiana na kuimarisha umoja huu. Ni lazima tubadilike na kwenda sambamba na wakati kwa ajili ya kujenga Taifa imara,” amesema Yolita.

Related Posts