Chunya. Waziri wa Madini, Athony Mavunde amesitisha shughuli ya uchimbaji madini ya dhahabu ndani ya Mto Zira uliopo katika Kijiji cha Ifumbo, Wilaya ya Chunya mkoani Mbeya.
Hatua hiyo imekuja siku chache baada kuibuka mgogoro wa wananchi na mwekezaji wa kampuni ya G&I Tech Traditional Company Limited, kulalamikia uharibifu wa mazingira na uchafuzi wa maji wanayotegemea.
Mbali na kusitisha shughuli hizo, Mavunde amesema ataunda timu ya wataalamu kutoka wizarani kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais Mazingira kufanya tathimini ya uharibifu, ili kuwezesha kuchukuliwa hatua stahiki.
Amesema ataagiza timu hiyo ya wataalamu kufanya tathimini kwa uwazi kwa kushirikisha wananchi wa Kijiji cha Ifumbo, sambamba na kutoa maelekezo kwa mwekezaji kusitisha uchimbaji katika msimu wa masika.
“Nimemsikia diwani amesema wananchi hoja ni suala la mazingira ambalo litaundiwa timu kuja kuchunguza na itapeleka mrejesho wizarani wa hali ya uharibifu, ili kuona hatua zitakazochukulia kama ni kusitisha leseni za uchimbaji,” amesema.
Mavunde amesema zuio hilo halimpi nguvu mtu yoyote kuingia kuchimba madini katika eneo hilo mpaka taarifa ya tathimini ikifanywa na mrejesho kupelekwa wizarani kwa ajili ya kufanya uamuzi wa kufuta leseni.
Diwani wa Ifumbo, Weston Mpyira ameomba Serikali kusitisha leseni za uchimbaji katika Mto Zira ili kulinda rasilimali za maji.
Mwekezaji wa kampuni ya G&I Tech Traditional Company Limited, Seleman Kaniki amesema eneo hilo linamilikiwa kihalali na wana vibali vyote kutoka Baraza la Uhifadhi wa Mazingira (NEMC).
Amesema wamekuwa wakiendesha shughuli za uchimbaji kwa kuzingatia masharti ya leseni ya kuondoa udongo na kuchenjulia nje ya mto, ili kuepuka uharibifu.
“Kwa mimi hatua niliyofikia sijawahi kufanya uharibifu wa kimazingira, kuhusu suala ya uchafuzi wa maji si sahihi ni vema sampuli za maji zichukuliwe na kupimwa ili Serikali ijiridhishe,” amesema.
Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Juma Homera amesema wamefika na kuona uharibifu uliofanywa na wananchi na mwekezaji.
“Mheshimiwa waziri tunaomba busara zako kama mwekezaji atatakiwa kuondoka na wanachi waondoke, na kama mwekezaji atabaki na wananchi wabaki ili kila mmoja anufaike na uwekezaji wa eneo hilo,” amesema Homera.
Kwa upande wake, Ofisa Mazingira Mwandamizi NEMC Kanda, Ezekiel Magamba, amesema mwekezaji huyo alipewa leseni ya kufanya tathimini katika eneo hilo, huku akibainisha leseni saba zimetolewa za uchimbaji katika eneo hilo.
Awali, Desemba 12, mwaka huu wananchi zaidi ya 1,000 wakiwa na silaha za jadi walivamia kambi la mwekezaji na kufanya uharibifu na kuchoma mali zake, wakishinikiza Serikali kusitisha shughuli za uchimbaji wa madini katika Mto Zira.