MATARAJIO ya Azam FC kwa sasa ni kukusanya pointi 12 katika mechi nne zilizosalia za Ligi Kuu Bara huku ikiiombea Simba iteleze kidogo tu ili wao wasiikose nafasi ya pili itakayowafanya washiriki michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu ujao.
Hesabu hizo za Azam zinaonekana kuwa ngumu kidogo lakini wenyewe wana matumaini hayo licha ya kwamba Simba ndiyo inaonekana kuwa na wakati mzuri zaidi wa kuikamata nafasi ya pili.
Hilo linakuja baada ya Alhamisi iliyopita Simba kuifunga Azam mabao 3-0 na kuzifanya timu hizo kutofautiana pointi moja pekee katika nafasi ya pili na tatu Azam ikiwa na 57 ikibakiwa na mechi nne wakati Simba inazo 56 na mechi tano mkononi.
Kutokana na hilo, Kocha wa Azam FC, Youssouph Dabo amewataka wachezaji wake kutokuwa na presha ya kumaliza nafasi ya pili na kukata tiketi ya kushiriki Ligi ya Mabingwa Afrika ambayo imeshiriki mara moja pekee mwaka 2015.
“Ni kweli matokeo yametusikitisha sisi kama benchi la ufundi na wachezaji kiujumla lakini tumekaa chini na kuwajenga kiakili na kisaikolojia tunaamini bado tuna nafasi nzuri hivyo kikubwa ni kuongeza umakini katika michezo yetu ijayo,” alisema Dabo.
Dabo aliongeza kwamba wakishafikia malengo ya kukusanya pointi 12 katika michezo yao minne iliyobaki ndipo wataangalia wapinzani wao wapo katika hali gani.
Katika mechi nne zilizobaki ambazo zimeshikilia hatma ya Azam katika nafasi ya pili, timu hiyo itaanza kushuka dimbani leo Jumapili kucheza dhidi ya KMC kwenye Uwanja wa Azam Complex.
Mchezo wa mzunguko wa kwanza uliozikutanisha timu hizo, Azam ilishinda mabao 5-0, mechi iliyopigwa pia kwenye Uwanja wa Azam Complex Desemba 7, mwaka jana. KMC inatarajiwa kutoa ushindani katika mchezo huo kutokana na kuhitaji kuisaka nafasi ya nne ikiwa imeachwa pointi nne na Coastal Union waliopo hapo.
Baada ya hapo Azam itacheza na JKT Tanzania Mei 20, kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo huku mechi ya kwanza ikishinda mabao 2-1 Desemba 11, mwaka jana. Ikimalizana na JKT Tanzania kazi itakuwa mbele ya Kagera Sugar Mei 25 iliyoinyuka mabao 4-0, mzunguko wa kwanza Desemba 21, mwaka jana ugenini, safari hii itakuwa nyumbani Chamazi.
Mei 28, Azam itamaliza msimu kwa kucheza na Geita Gold ugenini ambapo mechi ya kwanza ilishinda pia mabao 2-1, Februari 16, mwaka huu.
Hata hivyo ikiwa Azam itashinda michezo yake yote minne iliyobakia itamaliza na pointi 69 huku Simba iliyoko ya tatu kwa sasa na pointi 56 ikimaliza mechi zake tano itaishia na pointi 71 zitakazoifanya Azam kushindwa kumaliza nafasi ya pili.
Wakati Azam ikipiga hesabu hizo, Simba yenyewe katika mechi tano zilizobakia leo Jumapili itacheza dhidi ya Kagera Sugar na Dodoma Jiji ambazo zote zitakuwa ugenini, kisha itarudi nyumbani kumalizia mechi tatu dhidi ya Geita Gold, KMC na JKT Tanzania.