Askari Kinapa, mgambo matatani wakituhumiwa kwa mauaji

Moshi. Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, linawashikilia askari wawili wa Hifadhi ya Taifa ya Mlima Kilimanjaro (Kinapa) na mgambo kwa tuhuma za kumuua kwa risasi kijana Octovania Temba.

Temba ni mkazi wa Kijiji cha Komela kilichopo Kata ya Marangu Magharibi, wilayani Moshi, Mkoa wa Kilimanjaro.

Wakazi wa Kijiji cha Komela kilichopo Kata ya Marangu Magharibi, wilayani Moshi, Mkoa wa Kilimanjaro wakiandamana na kuchoma moto magogo na mabomba barabarani kulaani kuuawa kwa kijana Octavian Temba. Picha na Mtandao

Mauaji hayo yanadaiwa kufanyika Mei 9, 2024 wakati mwananchi huyo akikata majani ya mifugo pembezoni mwa hifadhi hiyo. Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa amethibitisha tukio hilo.

Dativa Raymond, mke wa Temba amesema Mei 9, 2024 akiwa nyumbani, mume wake alimuaga anaenda kukata majani msituni.

“Tunaishi karibu na hifadhi, aliondoka nyumbani saa 2:30 asubuhi. Nilikaa hadi saa nne asubuhi sijamwona. Kabla ya hapo tulisikia milio ya risasai huko hifadhini,” anasimulia.

“Nilipanda kuona alikokuwa akikata majani, tulipanda msituni hatukumkuta na simu yake tulipoipiga iliita mara moja ikakatika na baadaye ilizimwa,” amesema.

“Tukaanza kuhisi ile milio ya risasi ni yeye aliyepigwa, hivyo tulijaribu kumtafuta kila mahali hakuonekana, tulienda vituo vyote vya polisi hatukumpata. Baada ya wifi yangu kukaa kituo cha polisi mpaka sasa saba usiku, ndipo tukapigiwa simu jana (juzi), kwamba ameonekana na mwili wake upo Hospitali ya KCMC,” amesema.

Amesema ndugu yao aliyefika hospitali alikuta ni kweli kapigwa risasi kichwani.

Honest Kessy, mmoja wa wanakijiji amelieleza Mwananchi kuwa baada ya wananchi kupata taarifa kwamba Temba ameuawa na askari, waliamua kuandamana kwenda zilipo ofisi za Kinapa kupinga mauaji hayo.

“Nilienda chumba cha kuhifadhia maiti, tulishuhudia tukiwa na ndugu zao kwamba mwenzetu kafariki dunia kwa kupigwa risasi kichwani,” amesema.

Akizungumzia tukio hilo, Kamanda Maigwa jana amesema, “ni kweli kumetokea tukio ndani ya Hifadhi ya Kinapa, kwa sasa tunawashikilia askari wawili na mgambo mmoja kwa tuhuma za kuhusika na mauaji ya raia aliyekuwa ndani ya hifadhi,” amesema.

“Uchunguzi wa tukio hilo unaendelea, mpaka sasa mwili haujafanyiwa uchunguzi kutokana na vurugu zilizotokea jana (juzi), hivyo niwaombe ndugu waje mwili ufanyiwe uchunguzi wa madaktari ili taratibu nyingine za upelelezi ziweze kuendelea,” amesema.

Kamanda Maigwa amesema, “Niwahakikishie wananchi sisi kama Polisi kwa kushirikiana na vyombo vingine vya haki jinai, tutahakikisha kesi inaenda kwa mujibu wa sheria na uhalisi wa tukio ulivyotokea.”

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu amewataka askari kuacha kutumia nguvu kupita kiasi kupambana na wananchi.

“Kulitokea purukushani kati ya askari wetu na wananchi waliokuwa wakikata kuni ndani ya hifadhi, katika purukushani zile ikatokea bahati mbaya mwananchi mmoja akapigwa risasi na amefariki,” amesema.

“Jeshi la Polisi wanaendelea na uchunguzi na wamekamata askari wawili pamoja na mgambo,” amesema Babu.

Babu amesisitiza jambo kama hilo linapotokea na Serikali ikichukua hatua si vyema tena wananchi kuchukua sheria mkononi.

Amesema wananchi zaidi ya 200 walivamia eneo la geti la Kinapa na kufanya uharibifu mkubwa.

“Jana (juzi) kuna baadhi ya wananchi zaidi ya 200 walikwenda kwenye geti la Kinapa wakafanya vurugu na kuharibu miundombinu kwa kukata barabara ambayo imejengwa kwa gharama kubwa, mabomba ya maji na kule mlimani kulikuwa na watalii wa nchi mbalimbali pamoja na Watanzania, hivyo wakazua taharuki,” amesema.

Mbunge wa Vunjo, Dk Charles Kimei amelaani tukio hilo na kuitaka Serikali kuhakikisha haki inatendeka kwa mwananchi huyo.

“Utaratibu wa uhifadhi endelevu uzingatie mahusiano mazuri na jamii zinazopakana na maeneo yanayohifadhiwa,” amesema.

Dk Kimei amewasihi wananchi kuwa watulivu wakati Serikali ikilishughulikia jambo hilo.

Related Posts