‘Tunaweza kufanya 2025 kuwa mwaka mzuri’ – DW – 31.12.2024

Huku Ujerumani ikifunga mwaka wa sintofahamu ya kiuchumi na kisiasa, iliyoambatana na shambulizi la kigaidi kwenye soko la Krismasi mjini Magdeburg na kuua watu 5 na kuwajeruhi zaidi ya 200, Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz amelihimiza taifa kushikamana katika hotuba yake ya Mwaka Mpya.

“Jioni ya furaha wakati wa msimu wa sherehe katika soko la Krismasi la Magdeburg iligeuzwa kuwa jinamizi lisiloweza kufikirika,” Alisema Scholz, akibainisha kuwa wengi walikuwa wakijiuliza “ni wapi mtu anaweza kuanza kupata nguvu ya kuendelea na maisha baada ya janga kama hilo?”

“Tunaweza kuipata nguvu hiyo kwa kusimama imara pamoja. Sisi ni nchi ambayo inasimama pamoja,” Alisema Scholz.

Usalama wa Magdeburg wamulikwa

Kiongozi huyo wa mrengo wa kushoto aliwasifu maafisa waliofika wa kwanza katika eneo la shambulio huko Magdeburg, wakiwemo polisi na wafanyikazi wa matibabu, lakini pia aliwatambua watu wa kawaida kama vile mchuuzi wa soseji ambaye “usiku kucha akiwatengenezea chai majeruhi na wahudumu wa dharura.”

Hotuba yake iliyotayarishwa iliwekwa wazi saa chache baada ya maafisa wakuu wa usalama, akiwemo Waziri wa Mambo ya Ndani Nancy Feaser, kuhojiwa bungeni kuhusu tukio hilo. Ripoti katika vyombo vya habari ziliibua uwezekano wa kudorora kwa usalama ambao huenda ulimruhusu mtaalamu wa magonjwa ya akili mzaliwa wa Saudi Arabia Taleb A. kufanya shambulio hilo kwa namna ya kushangaza sawa na shambulio la lori lililotokea Berlin mnamo 2016.

Shambulizi la soko la Krismasi mjini Magdeburg
Shambulizi la kigaidi kwenye soko la Krismasi mjini Magdeburg liliwaua watu 5 na kuwajeruhi zaidi ya 200Picha: Hendrik Schmidt/dpa/picture alliance

Kansela huyo wa Ujerumani alikanusha uvumi unaoenea mtandaoni kufuatia shambulio la Magdeburg, lakini pia aliahidi uchunguzi.

“Ni wazi, pale ambapo mamlaka za usalama zilishindwa kuchukua tahadhari zinazofaa, hili litachunguzwa na kusuluhishwa,” alisema.

Scholz adokeza njama za Musk kuingilia uchaguzi

Akirudia wito wake wa umoja, Scholz aliashiria kuungana tena kwa Wajerumani kati ya Ujerumani Magharibi ya kibepari na Ujerumani Mashariki ya kisoshalisti takriban miaka 35 iliyopita, akisema kwamba uzoefu huu “unathibitisha kwamba kule inakoenda Ujerumani kutoka hapa kutaamuliwa na ninyi – raia.”

Scholz pia alisema kwamba mustakabali wa Ujerumani “hautaamuliwa na wamiliki wa chaneli za mitandao ya kijamii” akimlenga waziwazi Elon Musk. Mmiliki huyo mtandao wa X amekuwa akipaza sauti akiunga mkono wapinzani wa Scholz wa mrengo mkali wa kulia kutoka chama cha AfD.

Mtandao wa X unaomilikiwa na bilionea wa Marekani Elon Musk
Miito inaendelea kutolewa kwa Umoja wa Ulaya kumuwekea vikwazo Musk kwa kuingilia uchaguzi wa UjerumaniPicha: Algi Febri Sugita/Zuma/dpa/picture alliance

Akizungumzia mdororo wa uchumi unaoendelea, Scholz alidokeza kuwa Ujerumani bado inashika nafasi ya tatu kwa uchumi mkubwa duniani nyuma ya Marekani na China, licha ya kuwa na watu milioni 84 pekee. Scholz alibainisha kuwa “nyakati ni ngumu, hilo ni jambo ambalo sote tunaweza kuhisi.”

“Uchumi wetu unakabiliwa na changamoto. Gharama ya maisha imepanda,” Aliongeza, akiashiria “kuongezeka kwa wasiwasi kuhusu vita vikali vya Urusi dhidi ya Ukraine.”

“Kwa kuzingatia wasiwasi huu, haishangazi kwamba wengi wanajiuliza, kwa hivyo Ujerumani inakwenda wapi kutoka hapa? Tena, jibu langu ni: Ni kwa kusimama pamoja ndipo tunakuwa na nguvu.”

Msaada kwa Ukraine, bila kutaja Israeli au Gaza

Mwanasiasa huyo pia ameahidi kuwa Ujerumani “haitaiacha Ukraine katika hali ngumu” na itadumisha uungwaji mkono wake, huku pia ikihakikisha kwamba vita havisambai. Hotuba hiyo haikurejelea vita vinavyoendelea kati ya Israel na Hamas huko Gaza na maeneo mengine ya mgogoro katika Mashariki ya Kati.

Kansela huyo pia amewasihi wananchi kupiga kura katika uchaguzi ujao Februari mwaka huu, akisema kuwa hali ya sasa duniani inaonyesha kuwa ” uchaguzi huru na wa haki unaleta mafanikio makubwa.”

“Hatma yetu iko mikononi mwetu wenyewe. Tunaweza kufanya 2025 kuwa mwaka mzuri,” Alisema Scholz.

Related Posts