Hoja za wanaopinga ‘home work’ wakati wa likizo hizi hapa

Likizo ya Desemba inaenda ukingoni. Ndani ya likizo mengi yameibuka likiwamo suala la wanafunzi kushughulika na taaluma ama la.

Moja ya mijadala katika hilo ni pamoja na utaratibu wa shule kuandaa kazi maalumu zinazopaswa kufanywa na watoto wakati wa likizo. Makala haya yanaangazia maoni ya wadau wa elimu wanaotoa sababu za kupinga watoto kupewa kazi hizo maarufu Kiingereza kwa jina la ‘home work’

Naibu Katibu Mkuu wa zamani wa Chama cha Walimu(CWT), Ezekiah Oluoch, anasema kitendo cha kumpa mtoto kazi za nyumbani anapofunga shule, ni kumnyima haki yake ya kupumzika.

“Elimu ni sawa na sponji, ambayo ikiloa maji sana hainyonyi tena, hivyohivyo kwa ubongo wa binadamu hufika mahali hautaki tena kusikia na ndio maana kunakuwa na likizo hata kazini,”anasema.

Anasema mtoto anachotakiwa baada ya kurudi nyumbani au kuwa likizo, hatakiwi tena kujihusisha na masomo, isipokuwa anatakiwa kupata muda wa kujifunza elimu ya nje ya darasani ikiwemo masuala ya dini na ya kijamii.

Hata hivyo, anasema wanaotoa mazoezi hayo kwa watoto ni shule binafsi ili kuwaonyesha wazazi wa watoto kuwa watoto wao wanasoma.

Amani Mgheni, aliyewahi kuwa mwalimu kwa miaka 16 katika shule mbalimbali nchini, anasema Serikali ikiwa katika harakati za kuboresha elimu ya nchi hii, kuna haja ya kufanywa utafiti kuhusu kazi za nyumbani wanazopewa watoto.

Mgheni anasema imefika mahali watoto wanapewa maswali magumu ambayo hata wazazi wao walioenda shule wanashindwa kuwasaidia,.

“Kuna maswali mengine mada zake zinafundishwa vyuo vikuu. Lakini leo unakutana na mtoto wa shule ya msingi anapewa. Hapo ndipo unapokuta wazazi wakishindwa kuwasaidia watoto wao na hatimaye kuomba msaada kwenye makundi ya whatsapp…’’ anaeleza.

Kwa mtazamo wake, anasema utoaji wa kazi hizo siku hizi umekuwa kama fasheni, huku baadhi ya wazazi wakiona watoto hawajarudi nazo, wanahoji, jambo analosema si sahihi.

“Ifike mahali tuwaonee huruma hawa watoto. Kwa mfano, hawa wanaoishi Dar es Salaam, wengi wao wanamka usiku kwenda shule kutokana na adha za usafiri na foleni. Wanalazimika kutoka mapema, pia wanarudi kwa kuchelewa,’’ anasema na kuongeza:

“Ukimpa tena na kazi ya kufanya nyumbani ni kumnyanyasa na wakati mwingine huchangia watoto kuchukia shule kwa kuwa anajikuta akilishwa vitu vingi.’’

Anashauri Serikali kusimamia kwa karibu shule binafsi kwa kuwa kuna mambo mengi yanafanyika pasipo kufuata mwongozo wa elimu.

Anasema mtoto ana kipimo chake cha uelewa katika kumfundisha, ndio maana Serikali ikaweka idadi maalumu ya siku za kusoma zisizozidi 180.

‘’Kama sababu ni kufaulisha, mbona kuna waliosoma shule binafsi kwa kufuata ratiba hizo za Serikali na wakafaulu?’’anahoji.

Kwa upande wake, Mhadhiri wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Dar es Salaam (Duce), Dk Mabula Nkuba, anasema tatizo anaona linaanzia kwa walimu wenyewe katika ufundishaji wao.

Anasema haiwezekani mtoto awe ameelewa mada halafu awe anakosa zaidi ya nusu ya maswali, jambo analosema mwalimu akiona hivyo anatakiwa ajiongeze.

“Homewok ina maana ni kurudia kile ambacho mtoto umemfundisha kwa kwa siku ili kujua kwamba amekuelewa. Yaani mtoto kama ulimpa maswali kumi darasani, akakosa akapata mawili, halafu mwalimu unampa tena homework ya maswali ya aina hiyo, kuna shida, ”anasema.

Anachokiona walimu wengi hivi sasa hawana ule wito wa kufundisha na kumfanya mtoto aelewe, kwani wengine wameingia kwenye kazi hizo kwa kukosa ajira.

“Kwa namna ambavyo walimu wanafundishwa vyuoni, wanapaswa kutumia njia mbalimbali kuwalewesha watoto hadi waelewe na si kumsukumia mzazi amsaidie mtoto katika kusimamia homework,’’ anasema.

Anaongeza: ‘Kwa haya yanayoendelea, naunga mkono walimu kufanyiwa mtihani tena kabla ya kuajiriwa, kwa kuwa baadhi unakuta alishapita kwenye kazi zingine kama za bodaboda na nyinginezo na hadi anapata kazi anakuwa amesahau zile njia za kufundisha.’’

Related Posts