Vita ya mabingwa wa CAF yaanza upya!

Achana na Kariakoo Dabi itakayopigwa kuanzia saa 11:00 jioni kwa vigogo Simba na Yanga kuvaana kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, saa moja kabla huko Lubumbashi, DR Congo kutakuwa na vita ya nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika kati ya wenyeji TP Mazembe dhidi ya watetezi Al Ahly ya Misri.

Baada ya pambano hilo la Lubumbashi, saa 4:00 usiku itakuwa zamu y Esperance ya Tunisia itakayowapokea wageni wao Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini katikaa mchezo mwingine wa nusu fainali utakaopigwa mjini Tunis, Tunisia.

Utamu ni kwamba mechi zote mbili za nusu fainali ya michuano hiyo inazikutanisha mabingwa, kwani timu zote nne zina rekodi ya kubeba mataji ya Ligi ya Mabingwa kwa misimu tofauti, huku Al Ahly ikiwa ndio baba lao kwani imeshalitwaa taji hilo mara 11 ikiwamo inalolishikilia kwa sasa.

Pambano la Lubumbashi ni la tano kwa Mazembe kukutana na Al Ahly kuanzia mwaka 2000, kwani zilishavaana mara nne katika mechi za makundi na safari hii ni mara ya kwanza kupambana hatua ya mtoano.

Katika mechi hizo za awali, Al Ahly imeibuka na ushindi mara mbili, huku Mazembe ikitamba mara moja na mchezo mwingine uliishia kwa suluhu na safari hii zinakutana kila moja ikionekana kuwa na kiwango tofauti.

Mazembe imeonekana kuimarika zaidi msimu huu baada ya msimu uliopita kuyumba, huku Al Ahly iliyoing’oa Simba katika hatua ya robo fainali ya michuano hiyo kwa msimu huu, imeonekana kutokuwa na makali yaliyozoeleka, lakini inabebwa na uzoefu iliyonayo katika hatua kama hizi.

Mazembe yenye rekodi ya kubeba taji la michuano hiyo mara tano ikishika nafasi ya pili nyuma ya Al Ahly sambamba na Zamalek ya Misri, imefika hatua hiyo kwa kuing’oa Petro Atletico ya Angola katika robo fainali baada ya awali kushika nafasi ya pili katika Kundi A nyuma ya Mamelodi.

Imekuwa na rekodi nzuri nyumbani dhidi ya watetezi hao, kwani katika mechi mbili zilizopita baina ya Al Ahly, ilishinda 2-0 Sept 2, 2021 na ikatoka suluhu Sept Mosi, 2002, huku ikipasuka mechi zote mbili za ugenini dhidi ya wapinzani wao hao.

Mechi hiyo ya saa 10 jioni ya leo Jumamosi itafutiliwa zaidi kutaka kuona Mazembe itafanya nini tena nyumbani dhidi ya Al Ahly iliyoongoza Kundi D ililokuwa pia na Yanga, kisha kuing’oa Simba hatua ya robo fainali kwa jumla ya mabao 3-0 baada ya kushinda 1-0 ugenini na 2-0 ikiwa nyumbani.

Nyota wa timu zote wanalijua pambano hilo litakalopigwa kwenye Uwanja wa TP Mazembe na kuchezeshwa na mwamuzi Pacifique Ndabihawenimana kutoka Burundi kuwa sio jepesi, huku washambuliaji wa Al Ahly, Percy Tau, Ahmed Koka, Mahmoud Kahraba, Reda Slim na Anthony Modeste wakibeba matumaini ya watetezi.

Wenyeji inajivunia wakali wa kutupia Phillipe Kinzumbi, Glody Likonza, Patient Mwamba, Joel Bey na wengine kuiweka pazuri kabla ya mechi ya marudiano wiki ijayo itakayoamua wa kwenda fainali ili kuvana na mshindi wa jumla wa mchezo wa saa 4 usiku kati ya Esperance na Mamelodi.

Mechi hiyo ya Tunisia itakuwa ni ya saba kwa timu hizo kukutana tangu 2000, huku wenyeji wakibebwa na rekodi tamu za nyumbani mbele ya wageni wao, walioitoa Yanga kwenye robo fainali kwa penalti baada ya mechi mbili za awali kumalizika bila ya bao.

Katika mechi tatu za awali za nyumbani, Esperance imeshinda moja kwa mabao 3-2 mwaka 2000, huku nyungine mbili za mwaka 2001 na 2017 zikiisha kwa suluhu, huku ugenini ikipasuka mara moja mbele ya Wasauzi walipofungwa 2-0 mwaka 2000, na kushinda moja kwa mabao 2-1 mwaka 2017 na ile ya mwaka 2001 ililazimisha suluhu.

Kama ilivyo kwa mechi ya Lubumbashi, hata mchezo huu wa Tunisia sio mwepesi, licha ya wageni kupewa nafasi kubwa ya kuibuka na ushindi kutokana na aina ya kikosi ilichonacho kilichoruhusu bao moja tu hadi sasa katika mechi nane zilizopita za michuano hiyo kwa msimu huu kuanzia makundi hadi robo fainali.

Itakuwa bonge la burudani kwa mashabiki wa soka nchini ambao watazifuatilia mechi hizo za nusu fainali sambamba Kariakoo Dabi itakayopigwa Kwa Mkapa ikiwa ni mechi ya marudiano ya Ligi Kuu Bara baada ya awali Yanga kushinda 5-1 katika mechi ya mkondo wa kwanza iliyopigwa Novemba 5 mwaka jana.

Zilizopita Mazembe Al Ahly

Zilizopita Esperance v Mamelodi

Related Posts