Kocha Yanga atoboa siri, atoa tahadhari

KAMA unadhani Yanga ya Sead Ramovic imemaliza, basi unajidanganya. Wengi wanadhani timu hiyo imefika kileleni, lakini ukweli ni kwamba kuna asilimia 20 ya kiwango ambacho Mjerumani huyu anahitaji ili kuhakikisha kikosi kinakuwa moto zaidi.

Kocha wa viungo wa Yanga, Adnan Behlulov, amesema katika mahojiano na Mwanaspoti kuwa licha ya mwenendo mzuri wa kikosi hicho, bado kuna kazi ya ziada ya kuboresha hali ya miili ya wachezaji ili kustahimili mbinu za Ramovic hasa za soka la kasi analolitaka.

“Wiki chache zilizopita nilikuwa na shaka kidogo kwa sababu nilipofika nikaona hali ya miili ya wachezaji ilikuwa  chini. Tulikuwa mbali na kile kiwango cha juu ambacho timu inahitaji ili kucheza soka la kasi ambalo Ramovic anahitaji,” alisema kocha huyo.

Kila mazoezi aliyoongoza Behlulov yalikuwa na lengo la kuongeza nguvu, kasi na uvumilivu wa wachezaji.

“Tulianza na misingi. Nilijua kuwa fitinesi ni msingi wa kila kitu. Ilikuwa lazima wachezaji wawe na uwezo wa kukimbia kwa kasi kubwa, kubadili mwelekeo kwa haraka na kuhimili presha kubwa kwa dakika zote 90 za mchezo. Hilo lilikuwa ni changamoto kubwa,” alisema ambaye aliweka mkazo mkubwa kwenye mazoezi ya nguvu, kasi na stamina.

“Ramovic anataka soka la kasi, anataka wachezaji wafanye mabadiliko ya haraka katika kushambulia na kulinda, hivyo fitnesi ilibidi kuwa kitu cha kwanza. Kwa hiyo tulikuwa na kazi ya kuongeza kasi na uwezo wa kumudu mabadiliko hayo bila kupoteza nguvu jambo ambalo tumefanikiwa kwa asilimia 80 sasa.”.

Kocha Ramovic alisema: “Tunataka kucheza soka la kasi kubwa. Tunahitaji muda, bado hatujafika katika kiwango kinachohitajika, lakini tumepiga hatua nzuri. Tuko kwenye njia sahihi, Alhamdulillah.”

Related Posts