Kiteto. Mfugaji wa Kijiji cha Kimana wilayani Kiteto Mkoa wa Manyara, Happy Memiruti (38) anadaiwa kufariki dunia kwa kujinyonga na kamba ya kufungia ng’ombe.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Manyara, Ahmed Makarani akizungumza leo Jumanne Desemba 31 mwaka 2024 ofisini kwake, amesema tukio hilo limetokea wilayani Kiteto jana Jumatatu Desemba 30.
Hata hivyo, Kamanda Makarani amesema chanzo cha mwanamke huyo kujiua bado hakijajulikana.
“Polisi wanaendelea na uchunguzi wa kifo hicho, huku mwili wa marehemu ukiwa umehifadhiwa katika chumba cha maiti cha Hospitali ya Wilaya ya Kiteto,” amesema kamanda huyo.
Akizungumzia kifo cha mkewe, Maishiyake Mameruti amesema siku ya tukio walikunywa chai pamoja na watoto kabla ya yeye kuondoka nyumbani hapo na kuelekea kwenye shughuli zake.
Amesema alipata taarifa kuwa mkewe kajifungia ndani na kila akigongewa mlango hafungui.
“Niliporudi nyumbani, kweli mlango ulikuwa umefungwa kwa ndani, tukagonga sana lakini haukufunguliwa, tukachungulia dirishani tukaona ananing’inia amejinyonga, ndipo tukalazimika kuuvunja,” amesimulia Mameruti.
Baadhi ya majirani waliozungumz na Mwananchi akiwamo Neema Sinjori, amesema tukio hilo limewashtua kwa kuwa chanzo cha kujinyonga kwake hakijulikani.
“Hatuelewi kama kuna ukatili au manyanyaso yaliyosababisha ajiue au ni nini kimemkuta, inasikitisha,” amesema Sinjori.
Naye jirani mwingine, Mwasiti Hassan amesema marehemu hakuonyesha dalili za ugonjwa wala kuacha ujumbe wowote kabla ya tukio hilo. “Inawezekana afya ya akili ilikuwa na changamoto, lakini hatuna uhakika,” amesema.
Kaka wa marehemu, Marengoni Saibulu amesema mdogo wake alikuwa mtu mpole na asiye na ugomvi na mtu yeyote. “Tumeshangazwa sana na tukio hili,” amesema.
Marehemu ameacha mume na watoto wanne huku mdogo akiwa na mwaka mmoja na miezi miwili.