Simulizi kata ya Ng’ambi ilivyofanikiwa mapambano mabadiliko ya tabianchi

Mpwapwa. Katika Kata ya Ng’hambi, Wilaya ya Mpwapwa, kama maeneo mengine athari za mabadiliko ya tabianchi zilidhihiri na shughuli za watu kuathiriwa.

Kata hii iliyokuwa na watu 11,926 kwenye kaya 3,014  kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi ya 2022, ilikumbwa na changamoto kubwa za hali ya hewa, zikiwemo ukame wa mara kwa mara na ukosefu wa maji ya kutosha.

Changamoto hizi ziliathiri sekta ya kilimo na ufugaji, huku wakulima wakishindwa kupata mavuno ya  kutosha na ufugaji ukikosa tija kutokana na uhaba wa malisho na maji. Mazingira haya yalizorotesha hali ya kiuchumi na kijamii ya wakazi wa eneo hilo.

“Nilikuwa mkulima wa mahindi, lakini mazao yalikuwa yakiharibika kila mara kutokana na jua kali,” anasema William Samwel, mkulima kutoka kijiji hicho.

William anasema athari za ukame zilisbabisha kukosekana maji ya kutosha kwa matumizi ya nyumbani na mifugo. “Hili lili athriri ustawi wa jamii nzima. Watoto walikosa lishe bora, hali iliyozorotesha afya yao na kuathiri maendeleo yao kwa ujumla” alisema.

Alifafanua zaidi ukosefu wa maarifa na nyenzo za kulima kilimo mbadala ulikuwa kikwazo kwa wakazi wa Ngh’ambi kujikwamua kiuchumi na kuhakikisha usalama wa chakula katika kaya zao.

Mazingira haya magumu yalihitaji hatua za haraka ili kuleta mabadiliko na kuboresha maisha ya wakazi wilayani humo.

Ikiwa imepita wiki kadhaa tangu dunia ilipokutana kwenye mkutano mkubwa wa mabadiliko ya tabianchi (COP 29) uliofanyika huku Baku, Azerbaijan ambao miongoni mwa ajenda ilikua kuongeza hamasa na kuwezesha kuchukua hatua dhidi ya mabadiliko na kuhakikisha mchakato unaojumuisha wote katika kufanya maamuzi.

Tanzania ni katika nchi za mwanzo barani Afrika kuandaa Mpango wa Nchi wa Kuendeleza Programu ya Kuongeza Kasi ya Urekebishaji Afrika (AAAP) – njia ya uwekezaji inayoonyesha vipaumbele vya uwekezaji wa urekebishaji, mahitaji ya kifedha, na mikakati ya kuhamasisha fedha kwa ajili ya kutekeleza hatua za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Ng’ambi wabadili mtazamo wa kilimo

Asasi ya Umoja wa mataifa Tanzania (UNA Tanzania) kupitia mradi kijamii wa ustahamilivu wa mabadiliko ya tabianchi unaotekelezwa na wakazi wa kata ya Ng’hambi chini ya asasi hiyo jamii ilibadilika. Hili lilishuhudia wananchi wakufanya kilimo himilivu na matumizi ya njia bora za uhifadhi.

Katika kutekeleza mradi huu, jamii ya Ng’hambi ilipokea elimu ya mabadiliko ya tabianchi ili kuelewa athari na jinsi wanavyoweza kujihusisha na kilimo endelevu.

Mratibu wa mradi huu Ally Mwamzola anasema “Tulianza kwa kutoa elimu ili jamii iweze kuelewa vizuri athari za mabadiliko ya tabianchi na jinsi ya kujikinga dhidi yake.”

Mafunzo yaliyotolewa yaliwasaidia wakulima kuelewa umuhimu wa kilimo cha mtama, zao lenye uwezo wa kuvumilia ukame badala ya mahindi.

“Kabla ya mradi huu mkulima alikuwa na uhakika wa kuvuna gunia 3-4 kwa ekari moja, lakini baada ya mradi sasa wakulima wana uhakika wa kuvuna hadi magunia 9-10 kwa ekari moja,” aliongeza Mwamzola akionyesha jinsi wakulima walivyobadili kilimo kuendana na hali ya hewa.

Mwamzola aliongeza kuwa ili kukabiliana na changamoto za uhifadhi wa mazao, jamii ilijifuza namna ya kuongeza thamani ya mazao yao na kuhifadhi vizuri.

“…pia walipokea nyenzo sahihi za kilimo, kama mbegu, mbolea na magunia ya kuhifadhia chakula, hii imeongeza hali ya usalama wa chakula” alifafanua.

Lishe kwa watoto, elimu ya kimkakati

Kwa mujibu wa UNICEF Tangu mwaka 2010, Tanzania imepiga hatua kubwa katika kupunguza viwango vya udumavu, ambavyo vimepungua kutoka asilimia 42 hadi asilimia 30.

Katika kupambana na utapiamlo kwa watoto uliosababishwa na lishe duni, familia sasa zimeanzisha bustani za mboga katika Nyumba zao, jambo ambalo limeboresha lishe na afya za watoto wao.

Diwani wa kata hiyo Richard Matonya anaeleza kuwa, “Hivi sasa, karibu kila kaya ina bustani ya mboga, na tunatumia maji kidogo ili kuzitunza. Uanzishaji wa bustani za mboga umesaidia kuboresha afya za familia na kupunguza utegemezi wa mazao ya kilimo kikubwa pekee kama chanzo kikuu cha chakula”.

Mradi huu wa ustahamilivu wakulima 33 na kupanua  juhudi za kuimarisha ustahimilivu dhidi ya mabadiliko ya tabianchi, ambapo asilimia 71.4 sasa wana uelewa wa kina kuhusu mabadiliko ya tabianchi na athari zake.

Vilevile kuzingatia uendelevu wa hali hii elimu ilitolewa mashuleni.

Ng’hambi iliamua kuanzisha Shamba darasa katika shule ya Sekondari Ng’hambi na kuwawezesha wanafunzi kupata chakula wawapo shuleni, lakini pia ilitumika kama sehemu ya kujifunza mbinu na taratibu za kilimo cha kisasa.

“Tunatumia shamba la shule kutoa lishe kwa wanafunzi na kuwafundisha mbinu za kisasa za kilimo ambazo na wao wamekuwa wakiwapatia wazazi wao pia,” alisema Mwalimu Juma Yahaya Mkuu wa shule, shule ya sekondari Ng’hambi.

Mwalimu aliongeza, “kupitia mkakati huo wa shamba darasa wanafunzi sasa wana uhakika wa chakula wakiwa shuleni na hata kutumia ujuzi wanaoupata, juu yambinu bora na za kisasa katika kilimo, na kuurithisha  kwa wazazi na jamii yao inayowazunguka.

Mradi huo unaendeshwa na UNA Tanzania na washirika wao wa karibu LM International na SMC, Mpwapwa sasa imeanza kupata matumaini ya kuendeleza shughuli kuu za kiuchumi na kuhuisha hali ya uendelevu wa sekta za maendeleo ya jamii.

Mwaka 2023 ulirekodi joto la juu zaidi katika historia ya Tanzania kwa mujibu wa Mamlaka ya Hali ya hewa Tanzania (TMA), wastani ukiwa nyuzi 24.5°C, nyuzi 0.6°C juu ya kawaida. Mpwapwa, yenye hali ya nusu jangwa, inakumbwa na ukame; juhudi za mradi zinahusisha kuvuna maji ya mvua kwa kilimo na matumizi ya nyumbani.

Felista Isaya ni mmoja wa wanufaika wa mafunzo ya uvunaji aji wa maji ya mvua anasema, “Nilijifunza kuchimba shimo la kuvunia maji ya mvua na sasa natumia kwa kilimo na hata kuuza maji.”

Pia mradi wa ustahimilivu umejenga mabwawa mawili katika vijiji vya Kazania na Kiegea, kila moja likihifadhi lita milioni tisa, kwa kushirikiana na UNA Tanzania, LM International, na wakazi wa Ng’hambi.

 “Mabwawa haya yanahudumia wakazi zaidi ya 3,040, na yatasaidia kuwepo kwa maji kwa matumizi ya nyumbani na mifugo kutoka msimu mmoja wa mvua hadi mwingine” Alisema Gloria Mafole Mkurugenzi wa LM International nchini Tanzania.

Rais Samia Suluhu Hassan alikubali mwaliko wa Ban Ki-moon ambaye ni katibu Mkuu wa 8 wa Umoja wa Mataifa na Mwenyekiti wa Kituo cha Ulimwengu cha Urekebishaji (GCA) kujiunga na Bodi ya Ushauri ya GCA, hatua inayoakisi mafanikio ya Tanzania katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Miradi wa Mpwapwa unaonyesha umuhimu wa ushirikiano wa wadau licha ya changamoto zilizopo, zinazohitaji juhudi zaidi ili kusaidia jamii nchini kote. Mapambano dhidi ya mabadiliko ya tabianchi lazima yahusishe wote, bila kumwacha yeyote nyuma.

Related Posts