Dodoma. Maisha ya miaka 69 ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali mstaafu, Jaji Frederick Werema yamehitimishwa, akiacha alama nne za kukumbukwa.
Jaji Werema aliyefariki dunia Desemba 30, 2024 katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) alikokuwa akipatiwa matibabu, ameacha alama katika nyanja ya sheria ndani na nje ya nchi ambazo zitaendelea kuishi.
Jaji Werema atakumbukwa kwa namna alivyoandika barua kwenda Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu wa Jinai (ICC) iliyopo The Hague nchini Uholanzi kuhusu kesi iliyokuwa ikimkabili Naibu Rais wa Kenya kwa wakati huo, William Ruto.
Ruto alikuwa akituhumiwa kuchochea ghasia za kabla na baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2007-2008 zilizosababisha vifo vya takribani watu 1,133 na wengine 650,000 kulazimika kuyahama makazi yao.
Mwingine aliyeshtakiwa pamoja na Ruto ni mtangazaji wa redio, Joshua Arap Sang. Wawili hao walitakiwa kuhudhuria kesi wakati wote The Hague.
Septemba 9, 2013, Jaji Werema aliandika barua ICC akipendekeza kesi ya Ruto ifanyike Arusha, Tanzania badala ya The Hague, Uholanzi.
Pendekezo hili lililenga kumwezesha Ruto kuendelea kutekeleza majukumu yake ya kikatiba nchini Kenya.
Mbali ya Tanzania, nchi nyingine zilizoandika barua kwa ICC kuhusu kesi ya Ruto ni Rwanda, Burundi, Uganda na Eritrea.
Nchi hizi zilitaka mahakama hiyo kumpa nafasi Ruto kuendelea kutekeleza majukumu yake ya kikatiba bila kulazimika kuhudhuria kesi The Hague.
Walitumia hoja za msingi kutoka Mkataba wa Roma kutetea kwamba, viongozi wa ngazi za juu katika nchi zao wanapaswa kupewa fursa ya kuendelea na majukumu yao ya kitaifa bila vikwazo vya kesi za kimataifa.
Hata hivyo, baadaye ICC iliifuta kesi hiyo kwa kukosa ushahidi wa kutosha unaoonyesha ushiriki wa Ruto katika vurugu hizo.
Ilikuwa mara ya pili kwa ICC kushindwa katika jitihada za kuwashtaki waliodaiwa kupanga na kufadhili vurugu nchini Kenya.
Ushauri wa kisheria kwa mawaziri
Jaji Werema atakumbukwa kwa kusimamia ukweli. Aliwahi kulalamika bungeni kuhusu mawaziri waliokaidi ushauri wa kisheria aliotoa.
Alisema hali hiyo ilisababisha matatizo katika utendaji wa Serikali, yakiwemo yaliyoibuliwa kwenye Ripoti ya Operesheni Tokomeza Ujangili.
Jaji Werema alisisitiza umuhimu wa kuheshimu sheria akieleza hata yeye angeweza kuwajibishwa ikiwa angekiuka sheria.
“Tunatakiwa kuiga msemo wa Mkuu wa Jeshi la Polisi, Said Mwema (sasa ni mstaafu) kuwa ‘Tii sheria bila shuruti’, Rais tunamshauri na anashaurika kwa nini mawaziri wakatae kuzingatia ushauri?
“Mawaziri hawatakiwi kujifanyia tu mambo yao. Tunawaandikia barua lakini zinakwenda na yanafanyika yaleyale… Hata mimi nikionekana kukiuka sheria na kanuni naweza kuwajibishwa kwa kuwa hakuna aliye juu ya sheria,” alisema.
Alisema watu wanaweza kutofautiana kisiasa, lakini katika mambo yanayohusu haki za binadamu lazima kuunganisha nguvu pamoja ili kuhakikisha sheria za nchi zinafuatwa bila kupindishwa.
Tume iliyoundwa na Rais Jakaya Kikwete Mei Mosi, 2014 kuchunguza vitendo vilivyotokana na uendeshaji wa Operesheni ya Tokomeza Ujangili iliwang’oa madarakani mawaziri wanne.
Mawaziri waliojiuzulu ni aliyekuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Shamsi Vuai Nahodha, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk Emmanuel Nchimbi, Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki na Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Dk Mathayo David Mathayo.
Operesheni hiyo ilianza Oktoba 2013 na kusitishwa na Bunge Novemba 4, 2014 kutokana na ukiukwaji wa sheria na haki za binadamu wakati wa utekelezaji wake.
Tume hiyo iliongozwa na mwenyekiti Jaji na Balozi mstaafu, Hamisi Msumi ilichunguza tuhuma za uvunjifu wa sheria, kanuni, taratibu na hadidu za rejea za utekelezaji wa operesheni hiyo. Tume ilitembelea mikoa 20 na wilaya 38 na kupokea malalamiko kutoka kwa viongozi wa Serikali, mawaziri wanne waliojiuzulu, walalamikaji na waathirika wa operesheni hiyo.
Kujiuzulu kwa masilahi ya Taifa
Jaji Werema atakumbukwa alivyokabiliwa na kashfa ya sakata la rushwa la kuwezesha kuhamishwa Sh306 bilioni kutoka Akaunti ya Tegeta Escrow na uamuzi wake wa kuwajibika licha ya kuendelea kusisitiza, alichoshauri kuhusu fedha hizo ndicho kilikuwa sahihi.
Kutokana na kashfa hiyo, alijiuzulu nafasi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali Desemba 16, 2014 kwa kuandika barua kwa Rais Jakaya Kikwete ya kuomba kufanya hivyo. Jaji Werema alichukua wadhifa huo kutoka kwa Johnson Mwanyika aliyestaafu.
Licha ya ombi hilo kukubaliwa, Jaji Werema kuna wakati alifichua kuwa Rais Kikwete alimgomea kujiuzulu mara tatu.
Hata akiwa nje ya utumishi wa umma, Jaji Werema kuna wakati alikumbuka sakata la Escrow akasema: “Sakata la Escrow lilinisikitisha na kunisononesha.”
Alisema mawaziri aliowashauri walimgeuka akaeleza walivyojiweka kando naye wakati wa sakata la Escrow mwaka 2014, jambo lililomsukuma kujiuzulu kulinda heshima.
Katika barua kwa Rais Kikwete, Jaji Werema alisema aliomba kujiuzulu kwa sababu ushauri wake kuhusu suala la Akaunti ya Tegeta Escrow haukueleweka na umechafua hali ya hewa.
Jaji Werema atakumbukwa kwa namna alivyoshauri majaji na mahakimu kupunguza msongamano wa kesi kwa kufuta kesi zisizo na ushahidi wa kutosha.
Kuna wakati akizungumzia hilo alisema mwaka 1996 akiwa jaji, alilazimika kuwaachia huru washtakiwa 50 kwa siku moja baada ya kupitia majalada na kugundua hakukuwa na ushahidi wa kuwatia hatiani.
Alisisitiza kufanyika marekebisho ya sheria ya dhamana kuipa mahakama mamlaka ya kutoa au kumnyima dhamana mshtakiwa akilenga kuhakikisha haki inatolewa kwa usawa bila upendeleo.
Jaji Werema akizungumzia adhabu ya kifo, alisema haimpi mfungwa nafasi ya kujirekebisha na kuleta mabadiliko chanya maishani mwake.
Jaji Werema aliingia bungeni kwa mara ya kwanza Novemba 4, 2009.
Siku hiyo alijibu swali namba 72 lililoulizwa na Wilson Masilingi, aliyekuwa mbunge wa Muleba Kusini kuhusu hali ya jengo la Mahakama ya Wilaya ya Muleba mkoani Kagera.
Pia alijibu swali la nyongeza la Dk Willibrod Slaa, aliyekuwa mbunge wa Karatu.